Pages

Wednesday, January 28, 2015

MAWAZIRI WAPYA WATISHA

Rais Jakaya Kikwete.
Mawaziri walioteuliwa Jumamosi iliyopita na Rais Jakaya Kikwete, kuongoza wizara kadhaa, jana waliripoti ofisini huku wakitisha.

Mawaziri hao walipokelewa jana jijini Dar es Salaam, kwa nyakati tofauti kwa shangwe na nderemo katika wizara zao na kukabidhiwa ofisi na watangulizi wao, huku katika Wizara ya Nishati na Madini, Naibu Waziri mpya, Charles Mwijage, akimpokea bosi wake, Waziri George Simbachawene.
 
LUKUVI: NIMEINGIA WIZARA YA FITNA
Akizungumza baada ya kupokelewa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema anatambua Wizara aliyopelekwa ni ngumu yenye watu wafitini na majungu, huku wakihusudu wenye fedha katika kutenda kazi.
Alisema wanaodhani watafanya kazi kwa fitna badala ya kutekeleza sera ya utendaji bora, ni bora waachie ngazi mapema kabla fagio lake halijaanza. Alisema anatambua Wizara aliyopelekwa ni kaa la moto na ina watendaji wanaodhani kuwa wao ni bora kuliko wengine na kazi yao ni kukwamisha utendaji kazi wa Wizara. “Natambua kabisa wengi wenu hapa ni miongoni mwa wanaokwamisha utendaji kazi, siwatishi, lakini nataka mtambue sijaja hapa sijui kitu kabisa, kinachoendelea hapa najua na ninaahidi kuyashughulikia hayo,” alisema Lukuvi.
Akimkabidhi wizara hiyo, Waziri wa Nishati na Madini wa sasa, aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene, alisema anasikitika kuacha Wizara aliyokuwa ameizoea kwa muda mrefu kidogo. “Katika Wizara hii kuna mambo ambayo ni lazima yafanyiwe ufumbuzi likiwamo suala la migogoro ya ardhi isiyoisha na usimamiaji upimaji ardhi katika maeneo mbalimbali,” alisema Simbachawene. Aidha, alisema ni lazima kujua Wizara hiyo ndiyo iliyobeba Watanzania wengi wenye vipato tofauti tofauti. Aliwaeleza kuwa wakati umefika Wizara kupeleka ramani za maendeleo na makazi katika ofisi za serikali za mitaa na vijiji, ili kusaidia wananchi kujua maeneo yao yalivyo na wajenge vipi kuepuka adha ya bomoabomoa. 
Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Angella Kairuki, aliwataka watendaji wenye sifa ya kutumia nafasi zao kuwaonea Watanzania wachache wafuatilie historia yake katika Wizara aliyotoka na kuwa hatakuwa tayari kumuangusha kiutendaji Waziri wake. Alisema atahakikisha anashirikiana na Waziri wake kwa muda uliobaki kusimamia wizara hiyo yenye changamoto nyingi.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Alphons Kidata, alimtaka Waziri Lukuvi, kutokuwa na wasiwasi na suala la fedha za kufuatilia migogoro.
 
SIMBACHAWENE: RASILIMALI ZIWANUFAISHE WATANZANIA 
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, amesema siku tatu zinamtosha kufuatilia usiri uliopo kwenye mikataba ya gesi na mafuta na kutoa taarifa kwa Watanzania. Akijibu maswali ya waandishi wa habari mara baada ya kupokelewa, alisema anachofahamu hakuna usiri wowote katika mikataba hiyo kwa kuwa wanachostahili kupata Watanzania na mwekezaji kinajulikana, na kwamba wabunge wanaifahamu mikataba hiyo. 
“Mkisema kuna usiri nashindwa kuwaelewa mnataka mikataba ibandikwe Kariakoo au wapi, nami nimekuwa nikisikia haya maneno ya usiri usiri, nimepata nafasi kubwa kwenye Wizara nipeni siku tatu niingine ofisini nitatoa taarifa kamili,” alisema na kuongeza: “Tutaweka wazi kila kitu ili ajenda hii ifugwe na Watanzania wajadili mambo mengine, Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), wameshaiona hii mikataba na wabunge wengine nawashangaa wanavyosema kuna usiri.”
Kauli ya Waziri huyo imekuja miezi miwili baada ya PAC kutaka kupewa mikataba 26 ya uchimbaji na utafutaji wa gesi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), lakini haikuwasilishwa kwenye kikao cha kamati cha Oktoba 28, mwaka jana. Kutokana na hali hiyo, Kamati hiyo iliagiza kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi wa Shirika hilo kwa kosa la kuidharau kamati, hata hivyo walikamatwa Novemba 13, mwaka huu, na kuachiwa.
Simbachawene alisema rasilimali zilizopo ni mali ya Watanzania, hivyo wanapaswa kunufaika nazo na kwamba wawekezaji wa nje wanakuja na mitaji ya fedha, lakini wanapaswa kushirikiana na Watanzania. “Sekta ya madini na nishati ni kubwa sana duniani, ni jicho la wafanyabiashara wakubwa wa nje na waliopo nchini, tunafanya kila jitihada kuhakikisha sekta binafsi inanufaika hapa nchini,” alisema.
Waziri huyo alisema ni lazima kuwa na mpango mkakati wa kujenga uwezo wa Watanzania kutumia fursa zilizopo na kuhakikisha kinachopatikana kinawafikia Watanzania wote na kwa wakati. Alisema baada ya kuanza kazi jambo jingine atakalolifanyia kazi kwa haraka ni bei ya mafuta isiyoeleweka, ambayo katika soko la dunia imeshuka, lakini mabadiliko hayo hayaonekani hadi kwa Mtanzania wa kawaida. “Nitakutana na Mamlaka Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), kujua tatizo kwa nini bei ya mafuta haishuki ili hali katika soko la dunia bei ni ndogo, tutafanyia kazi na kutoa tamko kwa haraka,” alisema. 
Simbachawene aliwataka wachimbaji wadogo kutojiona wanyonge mbele ya wachimbaji wakubwa na wakati, na kwamba wajiweke tayari kukabiliana na ushindani.  Alisema aliwataka Watanzania kuwa na matumaini makubwa ya kushuka kwa bei ya umeme mara tatu hadi nne ya bei ya sasa, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha umeme cha Kinyerezi one cha gesi, ambacho kitapunguza kutegemea umeme wa mafuta na gesi. 
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mwijage, alisema amefanyakazi katika bomba la gesi akiwa kama mlinzi wa kufungua na kufunga mafuta, hivyo ana uzoefu wa kutosha katika sekta hiyo na kwamba iwapo bomba la gesi litalipuka atakuwa wa kwanza kuwajibika.
 
SITTA APIGA MKWARA WATAKAONDANGANYA
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harson Mwakyembe, na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, jana walikabidhiana ofisi huku wakitoa mikwara kwa watendaji waliopo chini ya wizara hizo.
Makabidhiano hayo ambayo yalifanyia katika ofisi za Wizara ya Uchukuzi, Sitta  aliwatahadharisha watendaji wa Wizara yake mpya ya Uchukuzi kwamba hatakuwa tayari kuwavumilia watendaji waongo wakati wa utendaji kazi. “Nitafanya kazi chini ya timu hii ambayo ilikuwa chini ya utendaji wa Dk. Mwakyembe. Jambo ambalo silipendi ni uongo, bora ukanieleza ukweli hata kama ni makosa, halafu mtu mzima kama mimi ukanidanganya wakati kuna data za kweli sitakuelewa kwa kweli,” alisema.
Alisema yeye ni mtu msikivu sana, lakini atakuwa mbabe zaidi ya Dk. Mwakyembe kwa watendaji wabovu. Sitta alimfagilia Dk. Mwakyembe kuwa ni mtendaji mzuri ambaye amefanya mabadiliko makubwa katika wizara hiyo, tena kwa kipindi kifupi na kwamba hata vitabu vya hstoria vitaandika kazi zake.
“Katika wizara ambazo zimefanya vizuri katika serikali moja ni Uchukuzi chini ya Mwakyembe, hata vitabu vya historia vitaandika kazi zake, aliongeza. Alimtaka Dk. Mwakyembe kuendelea na utendaji wake mzuri wa kazi na kwamba watashirikiana naye kuendeleza wizara zao ili kuleta ufanisi zaidi.
 
MWAKYEMBE AMKABIDHI SITTA RELI, BANDARI,
Awali, Dk. Mwakyembe akimkabidhi Sitta ofisi alisema Wizara ya Uchukuzi inakabiliwa na vipaumbele vinne ambavyo kama waziri anatakiwa kuanza navyo. Dk. Mwakyembe, alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni Reli ya Kati, ujenzi wa viwanja vya ndege, Bandari na Uwekezaji katika bandari ya Mtwara na Kigoma.
“Nafurahi kuwa wizara niliyohamishiwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa ni anayotoka Sitta, ambaye licha ya kuwa ni kiongozi wa siku nyingi, pia ni kaka yangu, ambaye naamini kupitia yeye ninaweza kumudu wizara hii ambayo ina mambo mengi zaidi ukilinganisha na miaka ya nyuma,” alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema anaamini kwa kushirikiana na Sitta wanaweza kuendeleza na kufanya kazi kubwa ambazo wameanziasha katika wizara zao. Kadhalika,, alisema yuko tayari kuendelea kutoa ushauri pale watakapokwama katika wizara hiyo kwa lengo la kukamilisha yale ambayo aliyaanzisha. 
Dk. Mwakyembe alimtaka Sitta kuwa tayari kumsaidia na kushirikiana naye pale atakapohitaji msaada kutoka kwake.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment