
Rais Jakaya Kikwete.
Mawaziri walioteuliwa Jumamosi iliyopita na Rais Jakaya Kikwete, kuongoza wizara kadhaa, jana waliripoti ofisini huku wakitisha.
Mawaziri hao walipokelewa jana jijini Dar es Salaam, kwa nyakati
tofauti kwa shangwe na nderemo katika wizara zao na kukabidhiwa ofisi na
watangulizi wao, huku katika Wizara ya Nishati na Madini, Naibu Waziri
mpya, Charles Mwijage, akimpokea bosi wake, Waziri George Simbachawene.
LUKUVI: NIMEINGIA WIZARA YA FITNA
Akizungumza baada ya kupokelewa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema anatambua Wizara
aliyopelekwa ni ngumu yenye watu wafitini na majungu, huku wakihusudu
wenye fedha katika kutenda kazi.
Alisema wanaodhani watafanya kazi kwa fitna badala ya kutekeleza
sera ya utendaji bora, ni bora waachie ngazi mapema kabla fagio lake
halijaanza. Alisema anatambua Wizara aliyopelekwa ni kaa la moto na ina
watendaji wanaodhani kuwa wao ni bora kuliko wengine na kazi yao ni
kukwamisha utendaji kazi wa Wizara. “Natambua kabisa wengi wenu hapa ni miongoni mwa wanaokwamisha
utendaji kazi, siwatishi, lakini nataka mtambue sijaja hapa sijui kitu
kabisa, kinachoendelea hapa najua na ninaahidi kuyashughulikia hayo,”
alisema Lukuvi.
Akimkabidhi wizara hiyo, Waziri wa Nishati na Madini wa sasa,
aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George
Simbachawene, alisema anasikitika kuacha Wizara aliyokuwa ameizoea kwa
muda mrefu kidogo. “Katika Wizara hii kuna mambo ambayo ni lazima yafanyiwe ufumbuzi
likiwamo suala la migogoro ya ardhi isiyoisha na usimamiaji upimaji
ardhi katika maeneo mbalimbali,” alisema Simbachawene. Aidha, alisema ni lazima kujua Wizara hiyo ndiyo iliyobeba Watanzania wengi wenye vipato tofauti tofauti. Aliwaeleza kuwa wakati umefika Wizara kupeleka ramani za maendeleo
na makazi katika ofisi za serikali za mitaa na vijiji, ili kusaidia
wananchi kujua maeneo yao yalivyo na wajenge vipi kuepuka adha ya
bomoabomoa.
Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Angella Kairuki,
aliwataka watendaji wenye sifa ya kutumia nafasi zao kuwaonea Watanzania
wachache wafuatilie historia yake katika Wizara aliyotoka na kuwa
hatakuwa tayari kumuangusha kiutendaji Waziri wake. Alisema atahakikisha anashirikiana na Waziri wake kwa muda uliobaki kusimamia wizara hiyo yenye changamoto nyingi.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Alphons Kidata, alimtaka Waziri
Lukuvi, kutokuwa na wasiwasi na suala la fedha za kufuatilia migogoro.
SIMBACHAWENE: RASILIMALI ZIWANUFAISHE WATANZANIA
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, amesema siku
tatu zinamtosha kufuatilia usiri uliopo kwenye mikataba ya gesi na
mafuta na kutoa taarifa kwa Watanzania. Akijibu maswali ya waandishi wa habari mara baada ya kupokelewa,
alisema anachofahamu hakuna usiri wowote katika mikataba hiyo kwa kuwa
wanachostahili kupata Watanzania na mwekezaji kinajulikana, na kwamba
wabunge wanaifahamu mikataba hiyo.
“Mkisema kuna usiri nashindwa kuwaelewa mnataka mikataba ibandikwe
Kariakoo au wapi, nami nimekuwa nikisikia haya maneno ya usiri usiri,
nimepata nafasi kubwa kwenye Wizara nipeni siku tatu niingine ofisini
nitatoa taarifa kamili,” alisema na kuongeza: “Tutaweka wazi kila kitu ili ajenda hii ifugwe na Watanzania
wajadili mambo mengine, Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC), wameshaiona hii mikataba na wabunge wengine nawashangaa
wanavyosema kuna usiri.”
Kauli ya Waziri huyo imekuja miezi miwili baada ya PAC kutaka
kupewa mikataba 26 ya uchimbaji na utafutaji wa gesi kutoka Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), lakini haikuwasilishwa kwenye
kikao cha kamati cha Oktoba 28, mwaka jana. Kutokana na hali hiyo, Kamati hiyo iliagiza kukamatwa kwa
Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi wa Shirika hilo kwa kosa la kuidharau
kamati, hata hivyo walikamatwa Novemba 13, mwaka huu, na kuachiwa.
Simbachawene alisema rasilimali zilizopo ni mali ya Watanzania,
hivyo wanapaswa kunufaika nazo na kwamba wawekezaji wa nje wanakuja na
mitaji ya fedha, lakini wanapaswa kushirikiana na Watanzania. “Sekta ya madini na nishati ni kubwa sana duniani, ni jicho la
wafanyabiashara wakubwa wa nje na waliopo nchini, tunafanya kila
jitihada kuhakikisha sekta binafsi inanufaika hapa nchini,” alisema.
Waziri huyo alisema ni lazima kuwa na mpango mkakati wa kujenga
uwezo wa Watanzania kutumia fursa zilizopo na kuhakikisha
kinachopatikana kinawafikia Watanzania wote na kwa wakati. Alisema baada ya kuanza kazi jambo jingine atakalolifanyia kazi
kwa haraka ni bei ya mafuta isiyoeleweka, ambayo katika soko la dunia
imeshuka, lakini mabadiliko hayo hayaonekani hadi kwa Mtanzania wa
kawaida. “Nitakutana na Mamlaka Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), kujua
tatizo kwa nini bei ya mafuta haishuki ili hali katika soko la dunia bei
ni ndogo, tutafanyia kazi na kutoa tamko kwa haraka,” alisema.
Simbachawene aliwataka wachimbaji wadogo kutojiona wanyonge mbele
ya wachimbaji wakubwa na wakati, na kwamba wajiweke tayari kukabiliana
na ushindani. Alisema aliwataka Watanzania kuwa na matumaini makubwa ya
kushuka kwa bei ya umeme mara tatu hadi nne ya bei ya sasa, baada ya
kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha umeme cha Kinyerezi one cha gesi,
ambacho kitapunguza kutegemea umeme wa mafuta na gesi.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mwijage, alisema amefanyakazi
katika bomba la gesi akiwa kama mlinzi wa kufungua na kufunga mafuta,
hivyo ana uzoefu wa kutosha katika sekta hiyo na kwamba iwapo bomba la
gesi litalipuka atakuwa wa kwanza kuwajibika.
SITTA APIGA MKWARA WATAKAONDANGANYA
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harson Mwakyembe, na
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, jana walikabidhiana ofisi huku
wakitoa mikwara kwa watendaji waliopo chini ya wizara hizo.
Makabidhiano hayo ambayo yalifanyia katika ofisi za Wizara ya
Uchukuzi, Sitta aliwatahadharisha watendaji wa Wizara yake mpya ya
Uchukuzi kwamba hatakuwa tayari kuwavumilia watendaji waongo wakati wa
utendaji kazi. “Nitafanya kazi chini ya timu hii ambayo ilikuwa chini ya utendaji
wa Dk. Mwakyembe. Jambo ambalo silipendi ni uongo, bora ukanieleza
ukweli hata kama ni makosa, halafu mtu mzima kama mimi ukanidanganya
wakati kuna data za kweli sitakuelewa kwa kweli,” alisema.
Alisema yeye ni mtu msikivu sana, lakini atakuwa mbabe zaidi ya Dk. Mwakyembe kwa watendaji wabovu. Sitta alimfagilia Dk. Mwakyembe kuwa ni mtendaji mzuri ambaye
amefanya mabadiliko makubwa katika wizara hiyo, tena kwa kipindi kifupi
na kwamba hata vitabu vya hstoria vitaandika kazi zake.
“Katika wizara ambazo zimefanya vizuri katika serikali moja ni
Uchukuzi chini ya Mwakyembe, hata vitabu vya historia vitaandika kazi
zake, aliongeza. Alimtaka Dk. Mwakyembe kuendelea na utendaji wake mzuri wa kazi na
kwamba watashirikiana naye kuendeleza wizara zao ili kuleta ufanisi
zaidi.
MWAKYEMBE AMKABIDHI SITTA RELI, BANDARI,
Awali, Dk. Mwakyembe akimkabidhi Sitta ofisi alisema Wizara ya
Uchukuzi inakabiliwa na vipaumbele vinne ambavyo kama waziri anatakiwa
kuanza navyo. Dk. Mwakyembe, alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni Reli ya Kati,
ujenzi wa viwanja vya ndege, Bandari na Uwekezaji katika bandari ya
Mtwara na Kigoma.
“Nafurahi kuwa wizara niliyohamishiwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa
ni anayotoka Sitta, ambaye licha ya kuwa ni kiongozi wa siku nyingi, pia
ni kaka yangu, ambaye naamini kupitia yeye ninaweza kumudu wizara hii
ambayo ina mambo mengi zaidi ukilinganisha na miaka ya nyuma,” alisema
Dk. Mwakyembe.
Alisema anaamini kwa kushirikiana na Sitta wanaweza kuendeleza na kufanya kazi kubwa ambazo wameanziasha katika wizara zao. Kadhalika,, alisema yuko tayari kuendelea kutoa ushauri pale
watakapokwama katika wizara hiyo kwa lengo la kukamilisha yale ambayo
aliyaanzisha.
Dk. Mwakyembe alimtaka Sitta kuwa tayari kumsaidia na kushirikiana naye pale atakapohitaji msaada kutoka kwake.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment