Ukimya wa Ewura ulikosolewa na watu wengi waliotaka kujua sababu za bei
ya mafuta nchini kutoshuka kulingana na mwenendo wa soko la mafuta ghafi
ulimwenguni.
Pamoja na mamlaka husika kutoa maelezo kuhusu
kushuka kwa bei ya mafuta, mjadala kuhusu bei hizo umezidi kupamba moto
kila kona ya nchi kutokana na maelezo yaliyotolewa kutojitosheleza na
badala yake kuacha maswali mengi yanayohitaji ufafanuzi wa kina.
Moja ya sababu zinazochochea mjadala huo ni
kitendo cha Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kukaa kimya
kwa muda mrefu bila kuteremsha bei ya mafuta hayo hata baada kuwapo
taarifa za muda mrefu kuhusu kuporomoka kwa bei ya mafuta hayo katika
soko la dunia kutoka Dola 115 za Marekani kwa pipa hadi chini ya Dola 50
tangu Juni mwaka jana.
Ukimya wa Ewura ulikosolewa na watu wengi
waliotaka kujua sababu za bei ya mafuta nchini kutoshuka kulingana na
mwenendo wa soko la mafuta ghafi ulimwenguni. Hoja ya wananchi wengi ilikuwa kwamba maelezo ya
Ewura yalikuwa dhaifu, kutokana na ukweli kwamba kuanzia Julai hadi
Desemba mwaka jana, bei ya mafuta ghafi ilishuka kutoka Dola 115 hadi
Dola 56 kwa pipa, hivyo walihitaji maelezo kwa nini kushuka huko kwa bei
hakukuleta unafuu wowote hapa nchini kwa kuwa bei ya zamani ndiyo
iliyoendelea kutumika.
Tangu awali, Ewura ilionyesha bayana kwamba
haikuwa na dhamira wala mpango wowote wa kuteremsha bei ya mafuta katika
siku za karibuni. Maelezo kwamba bei ingeshuka mwezi Februari kwa
madai kwamba bei ya mafuta hushuka baada ya miezi miwili kwa sababu
waagizaji huagiza mafuta mengi ambayo huchukua muda mrefu kumalizika,
kwa maana kwamba wakati bei zinaanza kupungua katika soko la dunia, bado
waagizaji wanakuwa na shehena kubwa ambayo haijanunuliwa.
Hoja hiyo imeonekana dhaifu kwa kuwa bei ya mafuta
ilianza kushuka katika soko la dunia zaidi ya miezi sita iliyopita.
Kenya, kwa mfano ilitangaza bei mpya Desemba 15. Maelezo ya Ewura kuhusu ukokotoaji wa bei ya
mafuta ghafi yanachanganya. Kama kweli mafuta safi ya petroli kwa tani
katika soko la dunia imepungua kwa Dola 249 za Marekani, dizeli kwa Dola
189 na mafuta ya taa kwa Dola 180, inakuwaje bei mpya zilizotangazwa na
Ewura bado ziwe juu kulinganisha na Kenya? Kwa mfano, wakati Ewura
ikitangaza lita moja ya petroli itauzwa Sh1,955, nchini Kenya inauzwa
Sh1,719.
Mbali ya kuwa Tanzania na Kenya ziko karibu na
bandari zinazopunguza gharama za usafirishaji na zina mfumo wa asilimia
40 ya makato yasiyobadilika, bado bei za Kenya ni nafuu kuliko Tanzania. Tunajiuliza Ewura inashindwa nini kuweka wazi
mfumo wa kukokotoa bei za mafuta ili wananchi waelewe kinachoendelea kwa
sababu wanayo haki hiyo. Kama bei ya mafuta ilishuka katika soko la
dunia tangu Julai mwaka jana, fedha zilizookolewa ni kiasi gani na ziko wapi?
Ipo hoja kwamba bei ya mafuta ingeshuka zaidi ya asilimia 15 kwa kutilia
maanani kwamba fedha zilizookolewa ni nyingi na kwamba kiwango cha
asilimia 40 ambacho Ewura inadai ni malipo ya usafirishaji na usambazaji
wa mafuta kiko juu kupita kiasi.
Ndiyo maana tunasema Ewura ifanye kazi kwa uwazi
na kutosubiri hadi wananchi walkalamike ndipo itoe ufafanuzi. Wananchi
wanataka ufafanuzi kuhusu bei mpya za mafuta utolewe kwa wakati na uwe
unajitosheleza.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment