Mwanajeshi wa kikosi cha anga cha Indonesia akiwa kwenye helikopta kutafuta miili na mabaki ya ndege ya AirAsia. Timu zenye kutafuta mabaki ya ndege ya abiria ya shirika la AirAsia
ilioanguka ikiwa na watu 162 zimegunduwa vipande vinne vikubwa vya ndege
hiyo chini ya habari.
Mkuu wa shirika la msako na uokozi la Indonesia Fransiskus Bambang
Soelistyo amewaambia waandishi wa habari mjini Jakarta Jumamosi
(03.01.2014) kwamba wamegunduwa vipande vinne vikubwa vya mabaki ya
ndege hiyo ambayo wamekuwa wakiitafuta.
Ugunduzi huo umekuja wakati serikali ikisema kwamba shirika la ndege la
AirAsia limekiuka masharti ya leseni yake ya kutumia njia ya Surabaya
kwenda Singapore hapo Jumapili siku ambayo ndege yake hiyo aina ya
Airbus A320-200 ilipoanguka kwenye bahari ya Java na kutangaza kwamba
watachunguza ratiba nyengine za safari ya ndege za shirika hilo. Kipande kimoja kikubwa kiligunduliwa na meli iliokuwa ikifanya msako
wakati wa usiku na vipande vyengine vitatu zaidi ambacho kikukwa kabisa
kikiwa na urefu wa mita 18 vimegunduliwa Jumamosi kwa mujibu wa
Solelistyo.
Hali mbaya ya hewa yatatiza
Afisa mwengine wa timu hiyo ya uokozi Supriyadi ambaye
anaratibu operesheni za uokozi kutoka bandari ya Pangkalan Bun ilioko
Borneo amesema hapo awali kwamba hali ya kutoweza kuona vizuri
imekwamisha juhudi za kunasa taswira za vipande hivyo kwa kutumia vyombo
vya kuzamia chini ya bahari.
Amesema uwezo wa kuona unakuwa wa umbali wa mita mbili tu na kwamba kuna
mawingu jambo linalofanya iwe vigumu kwa kamera kugunduwa kitu. Wapiga mbizi ikiwemo timu ya wataalamu ya Urusi ambao ndio kwanza
wamewasili huko Pankalan Bun wanaweza kuanza kuchunguza mabaki hayo hapo
Jumapili iwapo hali ya hewa itakuwa nzuri.
Hakuna manusura
Hakuna manusura waliogundulika kutokana na ajali hiyo ambayo
imetokea kama dakika 40 baada ya ndege hiyo kuruka kutoka Surabaya mji
wa pili kwa ukubwa nchini Indonesia katika eneo ambalo linafahamika kwa
kuwa na vimbunga vikali hususan wakati huu wa msimu wa mvua.
Repoti kutoka katika ofisi ya utabiri wa hali ya hewa nchini Indonesia
imesema yumkini ndege hiyo imeruka kwenye hali mbaya ya hewa jambo
ambalo ingelikuwa vigumu kuliepuka na kwamba inawezekana hali hiyo
imesababisha kuganda kwa barafu kwenye engine za ndege hiyo. Ofisi hiyo imesema kwa kuzingatia data zilizopatikana mara ya mwisho juu
ya mahala iliokuweko ndege hiyo hali ya hewa imesababisha ajali hiyo.
Leseni ya AirAsia yumkini kufutwa
Maafisa wa serikali ya Indonesia hapo Ijumaa walihoji iwapo
rubani wa ndege hiyo alifuata taratibu sahihi za hali ya hewa na baadae
ikazisitisha safari za shirika hilo la AirAsia za kutoka Surabaya kwenda
Singapore kwa kusema kwamba leseni ya safari zake hizo inaziruhusu tu
kusafairi siku za Jumatatu,Jumanne, Alhamisi na Jumamosi. Djoko Murdjatmondo kaimu mkurugenzi mkuu wa Usafiri wa Anga nchini
Indonesia amesema hapo Jumamosi kwamba Wizara ya Uchukuzi itachunguza
njia nyengine za safari zinazotumiwa na ndege za shirika hilo ambayo
husafiri katika vituo 15 nchini Indonesia.
Amesema watachunguza ratiba za safari zote za ndege za shirika hilo la
AirAsia na kwamba wanataraji kuanza kufanya hivyo hapo Jumatatu.
Ameongeza kusema inawezekana leseni ya shirika hilo la AirAsia nchini
Indonesia ikafutwa.
CHANZO: DW KISWAHILI
No comments:
Post a Comment