Mwenyekiti wa IPP, Dk. Reginald Mengi, ametoa wito
kwa matajiri nchini kutumia sehemu ya utajiri wao kuwasaidia watu wenye
ulemavu. Alitoa wito huo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya chakula cha
mchana alichowaandalia watu wenye ulemavu ikiwa ni sehemu yake ya
kuwasadia watu wa kundi hilo kila mwaka.
Dk. Mengi, aliwasihi Watanzania matajiri kukumbuka kwamba utajiri
walionao unatoka nchini, hivyo watumnie sehemu ya utajiri wao kuwasaidia
watu wenye ulemavu. “Wafanyabiashara wajitahidi kupeleka sehemu ya faida zao kwa wenye
uhitaji. Kuna vitu vichache ambavyo nataka kuwakumbusha wenzangu.
Kwa mfano, mimi ni mfanyabiashara wa soda…..sehemu ya faida ya
mauzo ya soda inatokana na huyo mtu mwenye ulemavu….ifike mahali
mfanyabiashara aseme ‘nitafute njia ya kumrudishia mtu mwenye ulemavu,”
alisema. Katika jitihada zake za kuendelea kuwawezesha watu wenye ulemavu,
Dk. Mengi alitangaza shindano la kubuni wazo la biashara huku kila mmoja
miongoni mwa washindi kumi watakuwa wakizawadiwa Sh. milioni 10 kwa
ajili ya kuwasaidia kuinua hali zao kiuchumi.
Pia, aliwataka Watanzania kuendelea kuombea amani kwani vitendo vya
uvunjifu wa amani vinapotokea, wanaoathirika wakubwa ni kundi la watu
wenye ulemavu. Naye mjumbe wa bodi ya Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu
Tanzania (Shivyawata), Abdallah Omari, alisema watu wenye ulemavu
wanakabiliwa na changamoto kubwa ikiwamo ya kuendelea kuongozeka idadi
ambayo hadi sasa inafikia takribani milioni 7.5.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni mauaji dhidi ya watu wenye
ulemavu wa ngozi likiwamo tukio la hivi karibuni la kutoweka katika
mazingira ya kutatanisha kwa msichana mkazi wa Wilaya ya Kwimba, Mwanza.
Changamoto nyingine ni pamoja na kukosa uwezo wa kujiendeleza kielimu kutokana na kukosekana kwa mtaji. Alimpongeza Dk. Mengi kwa kuyasaidia makundi ya watu wenye ulemavu
ikiwamo kuanzishwa kwa vikundi vya Vicoba na kwamba vikundi saba tayari
vimewezeshwa.
“Dk. Mengi ni mmoja wetu katika harakati zetu. Katika nyakati
tofauti, amekuwa akifikiria jinsi ya kuwakomboa watu wenye ulemavu. Kwa
mfano ameanzisha vitu mbalimbali kusaidia walemavu….Tumeanzisha vikundi
48 vya Vicoba,” alisema.
Alipongeza moyo wa Dk. Mengi akisema wapo wengi ambao wana utajiri
mwingi, lakini hawajawahi kujitokeza kufanya hivyo kwani hadi sasa
takribani ni miaka 20 amekuwa akiwasaidia. Kwa upande wake, kampuni ya Kamal Group, iliahidi miguu ya bandia
200 wiki hii kwa ajili ya kuwasaisaidia watu walioko kwenye kundi hilo.
Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, Sameer Gupta, alisema wataendelea
kutoa msaada huo kila mwaka ikiwa ni sehemu ya kuwasaidia watu wenye
ulemavu nchini. Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu Tanzania (Chawata) John
Mlabu, alishukuru kwa msaada huo huku akiwataka watu wenye ulamavu ambao
watapewa miguu hiyo ya bandia, kuitumia kama ilivyokusudiwa.
CHANZO:
NIPASHE


No comments:
Post a Comment