Mjumbe wa Kamati ya
Uongozi ya Wabunge wa CCM, Anna Abdallah amesema wanachama wote
wanaoendelea kukiuka kanuni na taratibu za chama hicho, lazima
wachukuliwe hatua kali za kinidhamu.
Alisema chama kitapunguza heshima yake endapo
wanachama hao hawataadhibiwa kwa sababu walishapewa adhabu lakini
hawataki kujirekebisha. Ingawa hakuwataja, waliopewa adhabu ni; Waziri
Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa,
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wasira,
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja. Adhabu zao zinamalizika Februari
18, mwaka huu. Kauli hiyo imekuja wakati Kamati ndogo ya maadili
ya chama hicho inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wake (Bara), Philip
Mangula, ikimaliza kazi ya kutathmini adhabu hizo juzi huku Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akisema inashangaza kuona baadhi
yao wakiendelea kufanya kampeni licha ya kamati Kuu ya CCM kupiga
marufuku.
Msimamo wa Anna Abdallah
Akizungumza jana, Abdallah ambaye ni Mwenyekiti wa
Umoja wa Wanawake Wanasiasa Tanzania (Ulingo), alisema chama hakitakiwi
kuogopa lolote juu ya kuwaadhibu wanachama hao. “Mwanachama asipokuwa mtii wa kanuni za chama,
huyo hatakiwi tena kuwa mwanachama, lazima ashughulikiwe na kama hataki
kutii agizo la chama basi ajiondoe kwenye chama ili aende huko
anakodhani kuna uhuru wa aina hiyo,” alisema na kuongeza: “Chama kisiogope lolote kwani nidhamu inajengwa na
utii wa kutekeleza maagizo ya chama, kisipowachukulia hatua nadhani
inaweza kuleta athari kwa wengine kutotii maagizo.”
Kauli ya Nape
Akizungumza jana CCM Kisiwandui, Zanzibar baada ya
Kamati Ndogo ya Maadili kumaliza kazi ya kuwajadili viongozi wa
waliokumbwa na kashfa ya ufisadi wa fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow,
Nape alisema: “Chama hakitasita kuwanyima nafasi ya kuwania urais
wagombea watakaobainika na kudhibitika kuendelea kufanya kampeni kabla
ya wakati kinyume na mwongozo uliotolewa mwaka jana.” Aliwataka wagombea na wapambe wao kuheshimu
utaratibu na uamuzi wa chama na wakati ukifika, kila mgombea atapewa
haki ya kufanya kampeni. Alisema licha ya wagombea hao kutahadharishwa, lakini bado wapo na wapambe wao wanaondelea kufanya kampeni. Nape pia alisema kumewa na uzushi mwingi kuhusu baadhi ya
wagombea kujadiliwa na vikao vya chama na kuelezwa kuwa wapo katika
hatari ya kupoteza hata uanachama wao mambo ambayo hayana ukweli.
Aliwataka wananchi kutosikiliza taarifa za uvumi kuhusu wagombea au
shughuli za chama hicho. Katibu huyo aliwataka wagombea wa nafasi ya urais
waliojitokeza kusimamia miiko ya chama na kuwakanya wapambe wao na watu
wanaosambaza taarifa za uongo dhidi ya chama na kujiepusha na kampeni
mapema kabla ya kuwavurugia. “Wengi wanaosambaza taarifa hizi ni wagombea au
wapambe wao wasiojiamini kutokana na matendo yao, ambayo hata wao wana
shaka na uadilifu wao. Hatuoni sababu ya mgombea anayefuata sheria,
kanuni na taratibu za chama kuhofia kuchuliwa hatua kila vikao vya chama
vinapofanyika,” alisema Nape.
Kashfa ya escrow
Alisema pia kwamba kamati hiyo imemaliza
kuwajadili viongozi waliokumbwa na kashfa ya escrow na kwamba uamuzi na
mapendekezo yake yatawasilishwa katika kikao cha Kamati Kuu. “Tumemaliza na Kamati itawasilisha mapendekezo yake kwa Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete baadaye Februari.” Waliokumbwa na kashfa ya miamala ya Akaunti ya
Tegeta Escrow ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge na Mbunge wa
Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Mwenyekiti wa Kamati ya
Katiba na Sheria na Mbunge wa Segerema, William Ngeleja.
Kinana na mabango
Katika hatua nyingine, Kinana ambaye yuko katika
ziara ya siku 10 Visiwani Zanzibar, amepokewa kwa mabango na wananchi wa
Kijiji cha Miwani, Mkoa wa Kusini Unguja, waliokuwa wakilalamikia kero
ya muda mrefu ya uchakavu wa barabara, ukosefu wa huduma za maji, afya
na mgogoro wa masilahi ya kisiasa uliyoibuka baina ya Mbunge wa Uzini,
Mohamed Seif Khatib na Mwakilishi, Mohamed Raza. Wananchi hao walinyanyua mabango yao muda mfupi baada ya kiongozi huyo kuwasili katika mkoa huo kukagua uhai wa chama. Wakizungumza muda mfupi baada ya kuwasilisha
ujumbe wao kwa amani, wananchi hao walisema kwa muda mrefu wamekuwa
wakikabiliwa na matatizo hayo bila dalili za suluhu. Mkazi wa Miwani, Juma Mussa Ussi alisema mgogoro
wa masilahi ya kisiasa baina ya Khatib na Raza unadumaza maendeleo ya
jimbo na kwamba wameamua kuwasilisha ujumbe huo kwa kiongozi wa juu
baada ya viongozi wa chama na Serikali Zanzibar kushindwa kuutatua. Kinana aliwataka viongozi wa chama hicho Mkoa wa Kusini Unguja,
pamoja na viongozi wa CCM Zanzibar kuchukua hatua za haraka kusuluhisha
mgogoro huo. Khatib alisema anaunga mkono hatua ya wananchi
kulalamika juu ya kero zinazowakabili kwa kuwa yamekuwa ya muda mrefu
yakiwamo ya uchakavu wa barabara, ukosefu wa daktari na dawa katika
Kituo cha Afya Miwani na uhaba wa Majisafi. Alisema tatizo la maji limesababishwa na kuungua
kwa mashine ya kuyasukuma kutoka katika Manzese lakini licha ya
kuwasilisha taarifa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), hakuna hatua
zilizochukuliwa. Kuhusu mgogoro wake na Raza alisema hakumbuki kuwa na mgogoro na mwakilishi huyo.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment