Askari wakiwataka wananchi kutawanyika baada ya kuahirishwa uchaguzi wa
Serikali za mitaa katika kituo cha Mabibo Mpakani Mtaa wa Jitegemee, Dar
es Salaam jana.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika juzi
nchi nzima ulikumbwa na kasoro nyingi ambazo wananchi wengi wanasema
zilitokana na uzembe au hujuma kwa upande wa maofisa walioteuliwa
kuuratibu na kuusimamia. Ni dhahiri sasa kwamba kasoro nyingi
zilizougubika uchaguzi huo hazikutokea kwa bahati mbaya, kutokana na
kutokea katika mazingira yanayoonyesha kwamba aidha zilitokea kwa uzembe
au kwa makusudi kwa lengo la kutimiza malengo fulani ya kisiasa.
Haijawahi kutokea uchaguzi huo, ambao husimamiwa
na Ofisi ya Waziri Mkuu inayohusika na Serikali za Mitaa (Tamisemi),
kugubikwa na kasoro nyingi kama ilivyotokea katika uchaguzi huo. Pamoja
na vyombo vya habari na asasi nyingi zisizo za kiserikali kuonya mapema
kwamba uchaguzi huo ungekabiliwa na matatizo mengi kutokana na
kutofanyika matayarisho ya kutosha, viongozi serikalini wakiwamo wa
Tamisemi walikaa kimya, hivyo kusababisha hofu kwamba uchaguzi huo
ungevurugika.
Kama tulivyosema hapo juu, kasoro zilizojitokeza
hazikuwa za kawaida. Vituo vingi vya kupigia kura viligeuka kuwa viwanja
vya mapambano, kutokana na kuwapo sintofahamu iliyosababishwa na
kutokuwapo kwa uhakika wa kupiga kura. Katika sehemu nyingi, uchaguzi
uliahirishwa kutokana na kutokuwapo kwa karatasi za kupigia kura, huku
katika baadhi ya sehemu uchaguzi ukiahirishwa kutokana na karatasi hizo
kuibwa. Baadhi ya maeneo yalikumbwa na tatizo la majina ya
baadhi ya wagombea kubadilishwa vyama wakati sehemu nyingine
zilishuhudia wapigakura wakishindwa kuona majina yao kwenye orodha ya
wapigakura, huku wengine wakikuta majina yao yamewekwa alama za
kuonyesha kwamba walikuwa tayari wamepiga kura.
Katika maeneo mengi, wananchi walicheleweshwa
kupiga kura kutokana na kuchelewa kwa vifaa vya kupigia kura, wakati
wengine walipiga kura pasipo kujiandikisha au kutumia wino unaotumiwa
kubaini watu ambao tayari wamepiga kura. Kero kubwa ilikuwa pale baadhi
ya wasimamizi walipopima umri wa wapigakura kwa macho na kuwakataa
baadhi ya wapigakura waliokuwa wamejiandikisha. Katika mazingira
yaliyoonyesha kwamba hapakuwapo ulinzi wa kutosha, ulitokea wizi wa
maboksi ya kura katika baadhi ya maeneo, huku katika maeneo mengine
wapigakura wakipelekwa vituoni kwa mabasi yaliyokodiwa kinyume na kanuni
za uchaguzi huo.
Matokeo ya hali hiyo ni vurugu zilizosababisha,
kwa mfano, kuchomwa moto Ofisi ya Mtendaji wa Serikali za Mitaa,
Sumbawanga mkoani Rukwa na kusababisha uchaguzi kuahirishwa katika kata
tisa kati ya 19 mjini humo. Katika maeneo mengi nchini polisi walitumia
mabomu ya machozi kutuliza vurugu za aina hiyo zilizotokana na wananchi
kupinga kuvurugwa kwa uchaguzi huo kwa kutokuwapo maandalizi ya kutosha
na matatizo mengine ambayo yangeweza kuepukwa kama mamlaka zilizoandaa
uchaguzi huo zingekuwa na dhamira ya kuufanikisha.
Ni katika mazingira hayo tunasema uchaguzi huo
haukuwa huru na wa haki katika sehemu nyingi nchini. Jambo la kushangaza
ni pale wagombea wengi wa upinzani walipowekewa pingamizi zisizo za
msingi na wenzao wa CCM, huku rufaa zao zikitupwa ama kutosikilizwa na
kamati za rufaa. Matokeo yake ni wale wa CCM kupita bila kupingwa. Ndiyo
maana tunasema viongozi wote katika ngazi zote za mchakato huo kuanzia
wizarani hadi vijiji, vitongoji na mitaa waliosababisha hali hiyo,
wawajibishwe. Uvurugaji wa chaguzi mbalimbali nchini utaendelea kuwa
utamaduni wa kudumu, kama mamlaka husika zitaendelea kushindwa
kuwawajibisha viongozi ‘nyangumi’ na kuwaonea maofisa ‘dagaa’.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment