Pages

Tuesday, December 16, 2014

TAMBWE ASAINI YANGE, MAXIMO NJE


Yanga imefanya usajili wa kushtukiza kwa kumsajili Amissi Tambwe aliyeachwa na Simba huku kibarua cha Mbrazili Marcio Maximo kikiwa dakika za mwisho Jangwani.
Habari za ndani kutoka Yanga zinasema kuwa Tambwe alisaini mkataba wa mwaka mmoja jijini Dar es Salaam jana. Kutokana na kusajiliwa kwa Tambwe, Yanga imemkata Mbrazili mwingine, Emerson Roque, ambaye alikuwa akibebwa na Maximo licha ya uongozi kutomfurahia. Tambwe, ambaye alifunga mabao 19 msimu uliopita akiwa na Simba alitemwa na Simba na nafasi yake kuchukuliwa na Simon Sserunkuma aliyeng’ara katika mchezo wa Nani Mtani Jembe, Jumamosi. Asaini Yanga, Maximo nje katika hatua nyingine, kocha wa Yanga, Marcio Maximo amegomea mpango wa uongozi wa klabu hiyo wa kutaka kumrejesha aliyekuwa kocha msaidizi Charles Boniface Mkwasa katika benchi la ufundi.
Uongozi wa Yanga kwa muda mrefu unataka kumpa jukumu Mkwasa la kumsaidia Maximo ili kuimarisha benchi hilo kutokana na ukweli kuwa enzi ya Mkwasa na aliyekuwa mkuu wake, Hans Van Pluijm, klabu hiyo ilikuwa moto wa kuotea mbali pamoja na kushindwa kutwaa ubingwa.
Uamuzi huo umetokana na mwenendo wa klabu hiyo kwa sasa ambapo pamoja na kushika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, imani ya mashabiki na wanachama ya kufanya vizuri msimu huu imetoweka kutokana na timu inavyocheza iwe katika mechi za kirafiki na za kimashindano.
Habari za uhakika kutoka klabuni hapo zimesema kuwa Maximo ametoa sharti la kuvunja mkataba wake na klabu hiyo endapo uongozi utamrejesha Mkwasa katika timu hiyo kwani yeye tayari ana mfumo wake na kocha wa sasa, Leonaldo Neiva.
Mmoja wa viongozi wa Yanga alisema kuwa Maximo ameshtukia ‘janja’ hiyo kwani anajua fika baada ya Mkwasa, itafuata zamu ya Pluijm kuingia katika timu hiyo na yeye ’kurushiwa’ virago vyake. “Juzi (Jumapili) kulikuwa na tetesi hizo na baadhi ya viongozi wa Yanga kukutana na kocha kujadili masuala hayo lakini kikao hakikumalizika kwa maridhiano na hii imetokana na msimamo wa Maximo ambaye amesimama katika falsafa yake,” alisema. Akizungumzia taarifa hizo, Mkwasa alisema kuwa hajui lolote kuhusiana na yeye kujiunga na Yanga na kama ipo nafasi hiyo, basi yeye hajaambiwa.
“Sijui lolote, ila kwa methali zetu, lisemwalo lipo na kama halipo linakuja, ila kiukweli kabisa, sijui lolote na hata huyo Hans Van Pluijm ambaye anatajwa kuwa yupo hapa nchini, hayupo, kama angekuwepo, lazima angewasiliana na mimi,” alisema Mkwasa. Kwa upande wake, Maximo hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo na kusema anaheshimu utaratibu wa klabu. “Kuna taratibu za klabu, nafasi yangu ya kuzungumza ni baada ya mechi au kwenye mkutano na waandishi wa habari, naheshimu utaratibu huo,” alisema Maximo.
Naye kocha wa Simba, Patrick Phiri ameshangazwa na kitendo cha Yanga kutaka kumfungashia virago Maximo kwa kusema klabu hiyo inafanya uamuzi wa haraka. Phiri alisema kumfukuza Maximo si sababu ya Yanga kupata ushindi na kusisitiza kuwa kufungwa mechi ya Mtani Jembe pia si kipimo cha kumwona Maximo hafai na kupuuza mchango wake. “Huo ni uamuzi wa haraka wanaotaka kufanya Yanga. Maximo ni kocha mzuri na mwenye kiwango kikubwa, viongozi wanapaswa kutambua mechi ya Simba na Yanga ni kubwa, leo Simba imeshinda kesho Yanga itashinda, Simba kumfunga Yanga au Yanga kumfunga Simba ni matokeo ya mpira.”

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment