Uhaba wa mabasi
yanayokwenda mikoa ya Kilimanjaro na Arusha umeendelea kuwatesa abiria
wa mikoa hiyo hali iliyowalizimu wagombee mabasi ya usafiri wa jijini
hapa maarufu kama ‘daladala’ ambayo yameruhusiwa kufanya safari katika
mikoa hiyo. Picha|Maktaba
Mapema juzi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Usafirishaji wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), Gilliard Ngewe
alinukuliwa na gazeti hili kuwa jana wangeongeza mabasi makubwa matano
ili kukidhi mahitaji ya abiria lakini jitihada hizo ziligonga mwamba
baada ya mabasi hayo kudai kuwa yamejaa.
Akikagua na kutoa vibali kwa daladala hizo katika
Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani kilichopo Ubungo, Ofisa Mfawidhi wa
Sumatra, Conrad Shio alisema jana kuwa kila jitihada za kuyapata mabasi
mengine makubwa lakini ilishindikana na kuamua kuendelea kutumia usafiri
wa daladala hizo aina ya Eicher kusafirisha abiria.
“Leo (jana) kuanzia saa moja asubuhi hali ilianza
kuwa mbaya tofauti na siku zingine ndiyo maana tunazikagua hizi daladala
ili ziwasafirishe hawa abiria, tukishatoa kibali abiria wanaanza
kugombania.
“Hatuna jinsi tutaendelea kuzitumia hizi daladala
maana mabasi ya njia nyingine tuliyokuwa tukiyatagemea kurahisisha kazi
hii nao wana kilio chao cha abiria kuwa wengi wanaelekea katika mikoa
wanayokwenda,” alisema.
Shio alisema daladala hizo zenye uwezo wa kubeba
abiria 41 zilianza kuruhusiwa juzi na zaidi ya Eicher 25 zimepewa vibali
na kutoza nauli ya Sh25,000 iliyopangwa na Sumatra.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa
Kipolisi Kinondoni, Awath Haji alisema polisi wamejipanga kuhakisha
abiria hao wanalindwa kwa kipindi chote watakachokuwa wakisubiri usafiri
kituoni hapo.
“Tangu asubuhi nipo hapa nikikagua magari
zikiwamo hizi daladala na sijapokea malalamiko yoyote kutoka kwa
abiria,” alisema Haji.
Albert Kitale ni miongoni mwa abiria waliokuwa
wakisubiri mabasi kuelekea Same mkoani Kilimanjaro, alisema hali ya
usafiri ni mbaya, kwani mabasi yote yamejaa hadi Desemba 27.
“Huu umati wa abiria unaonekana upo toka saa 11
alfariji mabasi ya kuunganisha hakuna na sidhani kama hizi daladala
zilizopo zitatosha. Jana (juzi) nilisikia kulikuwa na utaratibu wa
kupanga foleni ya kupanda katika daladala lakini leo suala hilo hakuna
gari likishakaguliwa na kupewa kibali abiria tunagombania,” alisema
Kitale.
No comments:
Post a Comment