
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Cosmas Mwaifwani.
Bohari Kuu ya Dawa (MSD), imesema imepanga kuanzisha
mradi wa uzalishaji dawa na vifaa tiba na kwa kushirikiana na sekta
binafsi utakaoisaidia kuzalisha dawa nyingi nchini badala ya kuendelea
kuagiza nje.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Cosmas Mwaifwani, alisema lengo la kuanzisha
mradi huo ni kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wingi
nchini.
Kadhalika, alisema ni kuifanya MSD kuwa kituo bora cha ufanisi katika mnyororo wa usambazaji dawa barani afrika.Mwaifwani alisema ili kufanikisha mradi huo, wamelenga kuingia ubia na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF). Alisema mpaka sasa asilimia 85 ya dawa za MSD zinazotumika kuhudumia nchini, zimekuwa zikinunuliwa nje, jambo ambalo linasababisha kuongezeka kwa matumizi makubwa ya fedha za kigeni kwa wastani wa Dola za Marekani 100 kila mwaka.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, wanalazimika kutegemea kampuni ya nje katika kudhibiti ubora wa dawa na vifaa tiba vinavyoagizwa, kiwango cha upatikanaji wa dawa kuwa chini pamoja na kutumia gharama kubwa kutunza dawa kwa muda mrefu kwa tahadhari ya kuepuka kuishiwa dawa kabla ya kukamilisha manunuzi.
“Baada ya kuzingatia hali halisi inayotukabili na kutafakari njia mbalimbali mbadala ambazo zinaweza kusaidia kutimiza lengo letu la kuimarisha upatikanaji wa dawa nchini, Bohari ya Dawa imeona kuwa kuongeza uzalishaji wa dawa wa ndani ndio litakuwa suluhisho la kudumu la upatikanaji wa dawa wa uhakika nchini,” alisema na kuongeza: “Tunaamini kwamba kama hili litafanikiwa changamoto hiyo na nyingine zitakuwa zimetatuliwa kwa kiasi kikubwa na pia tutachangia katika ongezeko la ajira nchini.”
NUKUU
“Baada ya kuzingatia hali halisi inayotukabili na kutafakari njia mbalimbali mbadala ambazo zinaweza kusaidia kutimiza lengo letu la kuimarisha upatikanaji wa dawa nchini, Bohari ya Dawa imeona kuwa kuongeza uzalishaji wa dawa wa ndani ndio litakuwa suluhisho la kudumu la upatikanaji wa dawa wa uhakika nchini,”
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment