Antonio Gutteres akiwa na Valerie Amos
Umoja wa Mataifa umeomba kiasi cha Dola Bilioni 8.4 kwa ajili ya kutoa
msaada wa dharura wa kibinaadamu kwa takribani watu Milioni 18 wa Syria
na kuzunguka ukanda huo unaokumbwa na mzozo.
Ombi hilo limetolewa jana na maafisa wa Umoja wa Mataifa mjini
Berlin, Ujerumani kwenye mkutano wa wafadhili na wamesema msaada huo
unahitajika haraka nchini Syria, na katika nchi na jamii zinazopambana
kuwahifadhi wakimbizi wa Syria. Kwa mara ya kwanza ombi hilo la Umoja wa Mataifa, linahusisha msaada
wa chakula cha kuwapa nguvu na kurudisha afya, malazi, msaada mwingine
wa kibinaadamu pamoja na msaada wa maendeleo. Maafisa wa umoja huo wamesema Dola bilioni 2.9 zinahitajika ili
kuwasaidia watu milioni 12.2 walioko ndani ya Syria kwa mwaka 2015, na
Dola bilioni 5.5 zinahitajika kwa ajili ya Wasyria walioomba hifadhi ya
ukimbizi kwenye nchi jirani na zaidi ya watu milioni moja katika jamii
zinazowahudumia. Kiasi hicho cha fedha kilichoombwa mjini Berlin, ni kikubwa zaidi ya
kile kilichoombwa mjini Geneva, mwanzoni mwa mwezi huu, msaada ambao
haukujumuisha fedha kwa ajili ya nchi jirani. Hata hivyo, umoja huo
umeshapata nusu tu ya kiwango kilichoombwa mwaka huu 2014.
Mahitaji ya kibinaadamu yanaongezeka
Kamishna Mkuu wa Shirika linalowahudumia Wakimbizi la Umoja wa
Mataifa-UNHCR, Antonio Gutteres ameonya kuwa wakimbizi na watu wasio na
makaazi ndani ya Syria hawana akiba na nchi zinazowahifadhi ziko katika
wakati mgumu, hivyo utaratibu mpya wa misaada unahitajika. ''Mahitaji ya kibinaadamu duniani yanaongezeka, na yanaongezeka kwa
kasi. Na ni wazi kwamba fedha zilizopo kwa ajili ya kutimiza mahitaji
hayo, haziongezeki kulingana na kukua kwa kasi ya mahitaji,'' alisema
Gutteres. Naye Mkuu wa shughuli za kibinadamu na misaada ya dharura ya Umoja wa
Mataifa, Valerie Amos amesema Syria imetoka katika taifa la watu wenye
kipato cha kati na kutumbukia kwenye nchi inayopambana na umaskini
mkubwa. Amesema watu walioathirika na mzozo wanahitaji chakula, malazi,
maji, dawa na ulinzi, lakini pia wanahitaji msaada wa kujenga upya
maisha yao, kupata elimu na huduma za afya. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier
amesema mzozo wa kibinaadamu nchini Syria na kwenye nchi jirani unatoa
kitisho kwa utulivu wa ukanda wote. Amesema huo ni mwito wa mshikamano
kwa mataifa yote na nchi yake iko tayari kutoa sehemu yake. Mwezi Oktoba, Ujerumani ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa
kuhusu Syria, ambapo wajumbe waliahidi kuongeza msaada wa kifedha wa
muda mrefu katika nchi kama vile Lebanon na Jordan, ambazo zinakabiliana
na mamilioni ya wakimbizi wa Syria wanaoingia kwa kasi kwenye nchi
hizo. Kiasi watu 200,000 wamekufa na karibu nusu ya idadi ya wakaazi wa
Syria hawana makaazi kutokana na mgogoro ulioanza kwa maandamano ya
kuipinga serikali ya Rais Bashar al-Assad mwaka 2011 na kugeuka vita vya
wenyewe kwa wenyewe.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment