Social Icons

Pages

Wednesday, December 17, 2014

TULITARAJIA NINI BILA TUME HURU YA UCHAGUZI?


Kwa muda mrefu sasa, tumekuwa tukionya kuhusu udanganyifu katika chaguzi mbalimbali zinazofanyika katika nchi yetu na kusema hiyo hasa ndiyo sababu inayowakwaza wananchi wengi kiasi cha kutojitokeza kupiga kura.

Tumekuwa tukisisitiza kuwa, pamoja na takwimu kuonyesha bayana kwamba idadi ya watu wanaojitokeza kupiga kura inapungua mwaka hadi mwaka, Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NecC) zimekaa kimya bila kuona umuhimu wa kutafuta kiini cha tatizo hilo na kulitafutia ufumbuzi. Hofu yetu muda wote imekuwa kwamba madhara yanayoweza kusababishwa na udanganyifu katika uchaguzi ni makubwa.
Hakuna asiyejua kwamba wizi wa kura na udanganyifu mwingine katika uchaguzi umesababisha maafa makubwa katika nchi nyingi barani Afrika, ikiwa ni pamoja na vita ya wenyewe kwa wenyewe. Ikumbukwe kwamba baadhi ya nchi zilizokumbwa na maafa hayo zilikuwa zikisifika kwa umoja na utulivu kama ilivyo kwa Tanzania. Hivyo, somo tunalopaswa kujifunza kama Taifa ni kuwa, amani iliyopo katika taifa lolote ikichezewa, kwa maana ya watawala kufanya hila na udanganyifu katika chaguzi ili waendelee kubaki madarakani, husababisha Taifa husika kusambaratika.
Tusisahau kwamba Tanzania siyo kisiwa, hivyo tusijidanganye kudhani kwamba amani na utulivu tulionao utadumu hata kama wananchi wataendelea kunyimwa haki zao za kikatiba, ikiwa ni pamoja na kuchagua viongozi wanaowataka.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Jumapili iliyopita umewafadhaisha wananchi wengi. Uligubikwa na vimbwanga na kasoro nyingi ikiwa ni pamoja na vitendo vya udanganyifu, hila na hujuma.
Waziri Hawa Ghasia, ambaye wizara yake ya Tamisemi ndiyo husimamia uchaguzi huo, anasema wizara yake haiwezi kutolea ufafanuzi malalamiko kuhusu kasoro lukuki zilizojitokeza katika uchaguzi wa Jumapili hadi itakapopata ripoti kutoka mikoani. Lakini waziri huyo anasahau kwamba kabla ya uchaguzi huo, alikutana na vyama vya siasa mjini Morogoro, ambako vyama hivyo viliainisha na kujadili kasoro za uchaguzi hata kabla hazijatokea katika uchaguzi wenyewe. Pamoja na mambo mengine, vyama hivyo viliunga mkono kauli ya awali ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu umuhimu wa kusogeza mbele tarehe ya uchaguzi huo ili kukamilisha maandalizi.
Tunaambiwa kwamba kikao hicho pia kiliona kasoro katika maeneo mbalimbali ya mapendekezo ya Serikali kuhusu kanuni za uchaguzi, ambazo hata katika uchaguzi wa Jumapili, zilileta matatizo makubwa. Hata hivyo, Waziri Ghasia alishikilia msimamo wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwamba uchaguzi ufanyike Jumapili iliyopita, hivyo viongozi hao wawili hawawezi kukwepa lawama na kuwajibika kwa kasoro zote zilizojitokeza katika uchaguzi huo.
Ndiyo maana tunasema visingizio vinavyotolewa na Waziri Ghasia na Tamisemi kwa jumla haviwezi hata kidogo kuhalalisha udhaifu, hujuma, uzembe na udanganyifu uliojitokeza katika uchaguzi wa juzi.
Baada ya kukataa kwa muda mrefu mapendekezo ya wadau kwamba chaguzi za Serikali za Mitaa pia zisimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Serikali sasa imesema utaratibu huo utaanza wakati wa uchaguzi wa mwaka 2019.
Hata hivyo, hatudhani kama kutakuwa na mabadiliko yoyote katika chaguzi zetu kama Nec haitaundwa upya na kuwa tume huru ya taifa ya uchaguzi (NIEC).

CHANZO: MWANANCHI

No comments: