Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, ni miongoni mwa watu wanaouelekea Uchaguzi Mkuu kwa kutambua nafasi zao katika kuchangia kumpata Rais anayefaa baada ya aliyepo sasa, Jakaya Kikwete, kutimiza muhula wake wa uongozi. Dk. Masaburi anayeaminika kuwa nguli wa mipango na mikakati ya kampeni ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), anajiweka wazi katika kutimiza wajibu wa kumpata Rais aliye bora, yule atakayeingia madarakani baada ya Rais Jakaya Kikwete. Anasema wajibu huo unajikita zaidi katika uadilifu wa mtu anayetaka kuwa Rais wa nchi, kwa vile pasipokuwapo uadilifu si rahisi kuwa na kiongozi bora wa nchi. Bila shaka Watanzania wengi wana tamanio hilo, kwamba Rais ajaye anapaswa kuwa na kiwango cha juu cha uadilifu utakaomfanya aguswe na umasikini na kadhia nyingine zinazoikabili nchi na watu wake. Haipaswi kuwa nchi inayojiwekea utitiri wa viongozi wenye kutaka kukidhi maslahi binafsi, wakiyaacha yale ya umma mpana. Sifa hiyo na pasipo shaka yoyote, haimgusi mgombea Urais kupitia CCM pekee, taasisi ambayo Dk. Masaburi ni mwanachama wake. Inamhusu kila Mtanzania anayekusudia kuwania nafasi hiyo ya utumishi wa umma. Ndiyo maana katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Dk. Masaburi, anaelezea ‘kutawaliwa’ na maslahi ya aina tatu katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015.
ANASIBU MASLAHI YAKE
Kwanza, anaelezea kuwa na maslahi yasiyokuwa na ukomo kwa taifa. Kwamba kila jambo analoshiriki katika kuitumia nchi na watu wake, maslahi mapana ya Taifa ni jambo asilofikiria kuliepuka. Pili, Dk. Masaburi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Alat, anathibitisha kuwa na maslahi ya muda mfupi na masuala ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anasema hali hiyo inatokana na kwamba masuala hayo yana ukomo wake na yanapohitimishwa, shughuli nyingine za maendeleo zinapaswa kufanyika kwa ufanisi. Pia, Dk. Masaburi anaelezea kuwa na maslahi ya muda mrefu na CCM, chama alichokitumikia kwa miongo kadhaa sasa, hata kikamfikisha kupata fursa za uwakilishi wa umma na nyinginezo. Kwa hali hiyo, Dk. Masaburi anasema kutokana na kuwa na maslahi ya kudumu na nchi huku yale ya CCM yakiwa ya muda mrefu, anawajibika kuhusisha uhusiano wa pande mbili hizo, yaani CCM na nchi. “Nina wajibu wa kuitumia nafasi yangu kuona CCM itaifanyia nini nchi hii, na kama nikigundua na kujiridhisha kwamba haipo katika kuyafikia maslahi ya kudumu kwa taifa, basi ninaachana nayo,” anasema. Dk. Masaburi anasema hatua hiyo ni pamoja na kumpata mgombea Urais bora, akiamini kwamba nafasi ya ushindi wa kiti hicho bado ipo kwa CCM.
SIFA ZA RAIS AJAYE
Anasema katika kufikia nia hiyo, yeye na wenzake katika Jumuiya ya Tawala za Mitaa (Alat), waliibua sifa anazopaswa kuwa nazo mgombea anayefaa kuwa kiongozi wa nchi baada ya Rais Kikwete. Dk. Masaburi anataja miongoni mwa sifa hizo kuwa ni kutokuwa dikteta, raia aliye mnyenyekevu kwa umma, anayefanya uamuzi kwa makini pasipo papara, mwenye kuamini na kudhamiria kutekeleza nadharia ya ukuaji uchumi wa watu katika ngazi za chini kwenye jamii. Anasema, uwekezaji katika ukuaji uchumi wa watu katika ngazi za chini ni muhimu kupewa kipaumbele katika sifa za Rais ajaye kwa vile pasipo kuwapo hali hiyo, ni vigumu kukabiliana na umasikini uliopo.
KUMPIGIA DEBE PINDA
Dk Masaburi anatajwa kuwa mpiga debe moja wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika kuteuliwa na CCM kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015. Akizungumzia hoja hiyo, Dk Masaburi anasema kwa muda mrefu amekuwa akizitaja sifa za Rais ambazo yeye binafsi anazikubali na `zinasimamiwa’ na Alat. Anasema sifa hizo zimekuwa kichocheo cha kuuaminisha umma kwamba anampigia debe Pinda. “Lakini kama Pinda anazo sifa hizo sisi wa Alat tutamuunga mkono na wakiwapo wengine zaidi tutawapima na kumpata mmoja wao. Hapa suala la muhimu ni mwenye sifa hizo,” anasema
SAKATA LA ESCROW
Dk Masaburi, anasema sakata linalohusisha akaunti ya Tegeta Escrow linagusa maisha ya watu kutokana na ukweli kwamba uchumi pasipokuwa na nishati ya umeme hauwezi kuwa wenye manufaa isipokuwa wenye kudorora. Anasema nishati ya umeme inagusa matumizi ya moja kwa moja na yasiyokuwa ya moja kwa moja, lakini kwa ujumla wake jamii inatumia bidhaa zinazotengenezwa viwandani ambapo nishati hiyo ni nyenzo muhimu. Dk. Masaburi anasema inashangaza pale sakata la Escrow na kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) lilivyopotoshwa kwa sehemu kubwa kiasi cha kuwagawa wananchi na kuibua hisa hasi kwa watawala.
Kwa mujibu wa Dk. Masaburi, yapo mambo ya msingi yanayogusia udhaifu uliopo kuhusiana na sakata hilo, wahusika wakiwa waasisi wake, lakini jamii `ikalishwa’ taarifa nyingi za upotoshaji kiasi cha kuibua chuki za wananchi kwa serikali yao. “Ninajua nitapingwa ama kufikiriwa kwamba na mimi nimemegewa fungu kutoka kwenye akaunti hiyo, lakini ukweli ni kwamba kusema fedha zote zilizokuwa kwenye akaunti ya Escrow ni za umma si sahihi, kwa maana umeme ulizalishwa na kutumika hivyo kuhitaji kulipiwa,” anasema.
Hata hivyo, Dk Masaburi anasema sakata hilo limejikita katika msingi unaomhusu mmiliki wake, ambapo umiliki wa kampuni ya Pan Africa Power (PAP) ya Harbinder Singh Sethi, unakosolewa na baadhi ya watu hasa wanasiasa. “Sasa kama huyo Singasinga (Sethi) hamiliki IPTL wangetuambia mmiliki wake halali ni nani? Wanapoliacha swali hilo bila majibu watu watazidi kujiuliza ingawa wao wananufaika wakijua wanaupotosha umma,” anasema. Dk Masaburi anasema baada ya kuisoma ripoti ya CAG, amebaini kuwa wanahisa wawili wa IPTL, Mechmar na VIP Engineering waliziuza hisa zao kwa njia na nyakati tofauti na hatimaye kumilikiwa na PAP ina Sethi. Kwa mujibu wa Dk Masaburi, upotoshwaji kuhusu sakata la Escrow na IPTL unafanywa na wasomi, wanasiasa wenye maslahi binafsi, mafisadi zikiwamo benki zinazotaka kujinufaisha kwa njia zisizokuwa halali.
KUUZWA KWA KAMPUNI YA UDA
Dk Masaburi anapozungumzia sifa za uadilifu kwa kiongozi anayefaa kuwa Rais wa nchi, anakutana na hoja inayomhusisha na sakata la uuzwaji wa kampuni ya mabasi ya usafiri jijini Dar es Salaam (UDA). Uuzwaji wa kampuni hiyo uliibua mzozo ukiwamo mjadala ulioibuliwa bungeni na wabunge wa jijini Dar es Salaam ambapo katika moja ya majibu ya serikali, Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima alielezea kuwapo kwa ukiukwaji wa taratibu katika uuzwaji wa kampuni hiyo.
Miongoni mwa mambo yaliyokuwa yakilalamikiwa na wabunge ni kuuzwa kwa kampuni hiyo kwa bei ndogo ikilinganishwa na thamani yake na utata wa kuhusu hati ya mauzo hayo. “Lakini niseme wazi kwamba mchakato wa kuuza mali ya umma, tena kwa shirika kubwa kama UDA hauwezi kufanyiwa uamuzi na mtu mmoja anayeitwa Didas Masaburi. Kulikuwa na ushiriki wa mamlaka husika na ambazo maelezo yake ya kina yanapatikana, lakini itoshe kusema kwamba sikuhusika kufanya uamuzi binafsi katika hilo,” anasema.
KUINUA UCHUMI WA RAIA
Dk. Masaburi anasema kwa hali ilivyo sasa nchini, ipo haja ya kuwekeza zaidi katika kuinua uchumi wa raia katika ngazi za mitaa. Anasema, wananchi wanaokabiliwa na hali duni ya ustawi wa maisha yao, hawataielewa serikali hata pale uboreshaji wa miundombinu unapofanyika huku wao wakizikosa huduma muhimu. “Hata serikali ikisema imejenga barabara ya mabasi yanayoenda kwa kasi ama daraja la kwenda Kigamboni jijini Dar es Salaam, kama mwananchi hapati maji safi na salama, huduma za afya na nyinginezo, kwake haitakuwa na maana sana,” anasema.
CHANZO: NIPASHE

No comments:
Post a Comment