Vuguvugu linalopinga kusilimishwa kwa Ujerumani, Pegida, sasa limekuwa
zaidi ya jina la maandamano ya kawaida, kwani Ujerumani yenyewe
imeelemewa na watu wengi wenye hofu dhidi ya Uislamu.
Kuna hisia za kuchanganyikiwa na zisizo mashiko lakini ambazo
zinachochewa na masuala kadhaa: kutokea mashambulizi ya Septemba 11 na
khofu ya daima dhidi ya Uislamu, mijadala juu ya kofia na maburka,
upandikizaji wa siasa kali za Dola la Kiislamu (IS), ambapo Waislamu wa
Kijerumani wenye asili za kigeni wamekwenda kujiunga nalo kama
wapiganaji wa jihadi, wimbi la wakimbizi kutoka nchi ambazo zinakabiliwa
na IS, na suala lililochukuwa muda mrefu la ikiwa nchi yenye Waislamu
wengi Uturuki, iruhusike kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya ama la.
Watu wengi wameelemewa na hayo na hilo linaweza kufahamika, kwa
sababu ukiacha uchambuzi wa kisomi kwenye siasa na vyombo vya habari,
watu wengi hawana uwezo wa kuchambua tafauti kati ya taswira hiyo
inayombatanishwa na Uislamu na Uislamu halisi. Kwao wao kila Muislamu ni
kama Muislamu mwengine.
Wakati huo huo, vyombo vya habari vinazidi kuzifanya hisia
hizo kuwa kali. Mfano halisi ni tukio la hapo jana la mkahawa kutekwa
nyara mjini Australia. Hata kabla ya taarifa za ndani kujuilikana,
tayari habari nzima ilishapagazwa majina yale yale: "jihadi", "mpiganaji
wa Mungu", "Muislamu mwenye siasa kali." Hakuna maneno ya kutafautisha
ukweli mmoja kutoka mwengine. Na katika hali ya kawaida, hilo
linachanganywa na kauli ya hivi karibuni ya Rais Tayyip Erdogan wa
Uturuki, ambaye aliwashauri Waturuki wanaoishi hapa Ujerumani kutojiona
Wajerumani sana.
Ukimya katika mambo muhimu
Kwayo pia zikaja ripoti juu ya vijana kutoka Wuppertal waliokuwa
wakijiita "polisi wa Sharia" ambao wakitembea mjini na kuwataka watu
wavae mavazi sahihi ya Kiislamu. Upumbavu wa kiasi gani! Na kipi zaidi
ya "Uislamu ni uovu" ambacho raia wa kawaida anaweza kukisema katika
hali kama hiyo?
Tatizo la Ujerumani ni kwamba kuna watu wengi wanaoyahofia hayo
lakini hakuna mjadala wa wazi kwayo. Na watu wengi, kwa hivyo,
wanajihisi kwamba hisia zao hazipewi uzito. Badala yake wanabezwa hata
kwenye kiwango cha watunga sera. Mfano wa karibuni ni kauli ya Waziri wa
Sheria wa Ujerumani, Heiko Maas, ambaye ameyaita maandamano ya Dresden
kuwa ni "aibu kwa Ujerumani".
Kauli hii ni ishara mbaya kabisa ya kuwatenga watu na inaonesha kwa
kiasi gani namna uwelewa wa jambo hili ulivyopewa umuhimu mdogo, kwani
hata kwenye chama chake Maas mwenyewe, kuna sauti nyingi zinazounga
mkono mawazo ya Pegida. Asilimia 46 ya walioulizwa kwenye chama hicho cha SPD walisema
wanaakisi matakwa ya Pegida. Wanasema kuwa SPD si chama ambacho hisia za
waumini wa Ukristo zinazingatiwa. Na hilo ni jambo la kufanyiwa kazi,
maana matokeo yake ni kwamba makundi yenye siasa kali za mrengo wa kulia
yanaweza kuwavutia wengi miongoni mwa raia.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment