Pages

Friday, December 19, 2014

SUMATRA YAIZUIA MV VICTORIA


Watumiaji wanaotegemea meli ya Mv Victoria juzi walipata adha ya usafiri baada ya kusitishwa kwa safari ya kuelekea Mwanza hatua iliyochukuliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra)kwa madai kwamba ilitoroshwa bila kukaguliwa.
Ofisa Mfawidhi wa mamlaka hiyo, mkoani Kagera, Kapteni Alex Katama alisema awali, meli hiyo ilizuiliwa Mwanza kwa ajili ya matengenezo na kwamba haikufanyiwa ukaguzi kabla ya kuruhusiwa na akisisitiza kuwa meli hiyo bado mbovu.
“Ilifika Bukoba ikitumia injini moja bila ruhusa ya mamlaka, tutaendelea kuizuia mpaka itakapofanyiwa ukaguzi na kujiridhisha, kosa lililofanyika halitakiwi kujirudia mara ya pili,’’ alisema Kapteni Katama
Hadi inazuiliwa, ilikuwa ikijiandaa kwa safari hiyo ya Mwanza na tayari mizigo ilikuwa imeshapakiwa.
Akizungumza kwa simu juzi, Meneja Masoko wa Shirika la Huduma za Meli, Obed Tirugumila alisema mv Victoria ilifanyiwa matengenezo Mwanza lakini haikufanyiwa majaribio na maofisa wa ukaguzi wa Sumatra akidai kuwa walisema hawana nafasi.
Tirugumila alisema waliamua kufanya majaribio kwa kwenda Bukoba wakiwa na abiria na kufika salama, lakini baadaye walipokea amri ya Sumatra ikiizuia meli hiyo kusubiri ukaguzi.
Kutokana na hatua hiyo, baadhi ya wafanyabiashara waliandamana hadi kwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Ziporah Pangani kulalamikia kusitishwa ghafla kwa safari hiyo wakidai kwamba itawapa hasara ya kuharibika mazao yao. Hata hivyo, Pangani aliwataka wafanyabiashara hao kurudi katika ofisi za meli hiyo akisema wanapaswa kutii agizo la Sumatra.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment