
Mwandikishaji wa vitambulisho vya uboreshaji wa daftari la kudumu la
wapigakura, Kheri Mkali akichukua maelezo ya Rebeca Kimu katika kituo
cha Bunju A, Dar es Salaam jana.
Uandikishaji wa wapigakura kwa
kutumia mfumo mpya wa BVR unaoendelea katika kata tatu za Jiji la Dar es
Salaam umeanza kusuasua kutokana na matatizo ya watendaji na mashine
zinazotumika kwenye uandikishaji huo. Uandikishaji huo unaofanyika kwa majaribio kwenye
Kata za Bunju, Mabwepande na Mbweni ulianza Jumatatu wiki hii na
unatarajiwa kumalizika Jumatatu wiki ijayo.
Akizungumzia uandikishaji huo jana, Ofisa Mtendaji
wa Kata ya Bunju yenye vituo 13, Emmanuel Riwa alisema wamekuwa
wakikabiliwa na matatizo makubwa yanayotokana na ufanisi mdogo wa
mashine za kutoa vitambulisho, hivyo kuchukua muda mrefu tofauti na
ilivyotarajiwa. Alisema matatizo makubwa yanayojitokeza kwenye
maeneo mengi ni mashine hizo kuzimika na kushindwa kuendelea kuzitumia
kama ilivyopangwa huku idadi ya watu wanaojitokeza ikizidi kuongezeka.
“Mashine tatu unazoziona hapo nje zimezimika na
imewalazimu watendaji wetu kuzirudisha na nyingine zinazoendelea
kutumika kasi yake ya kutoa vitambulisho ni ndogo sana. Kwa hiyo watu
wanaendelea kujaa vituoni huku wakisubiri huduma bila mafanikio,”
alisema Riwa. Alieleza kwamba japokuwa wamekuwa wakiandikisha
hadi watu 800 kwa siku, itakuwa si rahisi kufikia lengo ndani ya siku
saba zilizopangwa hivyo kushauri kuongeza siku zaidi kwa ajili ya kutoa
nafasi pana zaidi kwa watu wengi kujiandikisha.
Riwa alisisitiza kamba japokuwa watu wanajitokeza
kwa wingi sasa, hali inatarajiwa kuwa ngumu zaidi katika siku za mwisho
wa wiki ambazo wengi waliopo katika kazi zisizowaruhusu kurudi nyumbani
mapema watakuwa mapumziko na kutumia nafasi hiyo kujiandikisha. “Kwa kweli, wakati tunaendelea kutafuta ufumbuzi
wa matatizo yanayojitokeza kutokana na mashine hizi, bado tunaona
changamoto zaidi katika siku hizi za mwisho wa wiki. Ndiyo maana
tunaomba ikiwezekana siku ziongezwe,” alisema.
Baadhi ya wananchi waliotokeza kujiandikisha
walieleza kwamba wapo waliojitokeza juzi wakashindwa kujiandikisha hadi
jioni kutokana na wingi wa watu na hata walipofika jana walikuwa
wakiendelea kupoteza muda mwingi kusubiri kuandikishwa. Mmoja wa wananchi hao, Peter Stephano alisema
katika kituo alichokuwa akisubiri kujiandikisha, watendaji walichelewa
na kufungua kituo saa nne badala ya saa mbili asubuhi wakati wananchi
wakiwa tayari wameshajipanga kwenye foleni tangu saa 12 asubuhi.
“Wengi tunajitokeza lakini tunapofika vituoni
matatizo yanayojitokeza yanasababisha tupoteze muda mwingi. Wengine
wanaamua kurudi nyumbani na kuendelea na shughuli zao kwa sababu
hawawezi kupoteza siku nzima hadi siku mbili kwa ajili ya kujiandikisha
tu,” alisema. Katika kituo cha Shule ya Sekondari Mbweni,
wananchi walikuwa wamefurika kujiandikisha huku wakilalamikia ubovu wa
mashine moja kati ya mbili, hivyo kutumia mashine moja na kuchelewesha
uandikishaji.
Mwandishi wetu alishuhudia watu wawili wakiandikishwa kwa nusu
saa katika kituo hicho, kutokana na mashine moja iliyobaki kuwa na kasi
ndogo ya kukusanya maelezo na kutoa kitambulisho. Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mbweni yenye vituo 15,
Sylvester Nchonja alisema wanaendelea kukabiliana matatizo madogomadogo
yanayojitokeza na uandikishaji unaendelea kama ulivyopangwa. Alipoulizwa kuhusu matatizo hayo, Mkurugenzi wa
Uchaguzi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Julius Malaba alisema bado
wanasubiri taarifa kutoka kwa msimamizi ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa
ya Kinondoni, ambaye hata hivyo, hakupatikana baada ya simu yake kuita
bila kupokewa.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment