
Imesema kila wilaya nchini itakuwa na askari sita
wa JWTZ ambao watashirikiana na wataalamu wanne wa Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (Tehama) kutoka Nec na kampuni inayotengeneza vifaa vya
uandikishaji.
Akizungumza katika mkutano baina ya tume hiyo na
wadau wake juu ya hatua iliyofikiwa katika kuboresha daftari hilo,
Mkurugenzi wa Nec, Julius Malaba alisema timu hiyo itasimamia
uandikishaji na kufanya matengenezo madogomadogo ya vifaa wakati wa
uandikishaji iwapo yatahitajika.”
Hata hivyo, mpango huo wa kutumia JWTZ umepingwa
na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wakisema unaweza kuliingiza
Taifa kwenye machafuko.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema
kwa mpango huo, Nec inaweza kuiingiza nchi kwenye machafuko kama
yaliyotokea katika nchi nyingine.
Alisema kulitumia jeshi ni sawa na kuondoa
demokrasia ambayo imezoeleka kwa Watanzania na kusisitiza kuwa tangu
nchi imepata uhuru, hakuna siku ambayo jeshi lilitumika kwenye masuala
ya uchaguzi wala uandikishaji wa daftari la wapigakura.
“Hii mitambo ya BVR kwani ni ya kijeshi mpaka
mnasema jeshi litumike kusimamia daftari hili? Tumieni busara ili
demokrasia iendelee kuwapo nchini,” alisema Dk Slaa.
Mkurugenzi wa Uchaguzi Chama cha Sauti ya Umma
(Sau), Johnson Mwangosi alisema tangu mwaka 1995, vyama vya siasa
vilikataa jeshi kuingizwa kwenye siasa, hivyo hakuna sababu kusimamia
daftari hilo wala kujihusisha na uchaguzi.
Pia aliiomba Nec kutotumia Vitambulisho vya Taifa katika mchakato huo akisema ni Watanzania wachache wenye vitambulisho hivyo.
Mwenyekiti wa ADC, Said Miraji alisema: “Kutumia jeshi kwenye uandikishaji ni sawa na kutokomeza demokrasia iliyopo nchini.”
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Sheweji
Mketo alisema: “Ni kosa kulihusisha jeshi katika hili. Haya ni matokeo
ya Nec kutovishirikisha vyama vya siasa katika kuandaa taratibu za
maboresho haya.”
Kaimu Katibu Mkuu wa NCCR - Mageuzi, Faustine
Sungura alisema: “Kulitumia jeshi ni sawa na kuwaambia wananchi
wasijitokeze kabisa kujiandikisha. Wakiwaona watashindwa kujiandikisha,
watakaopiga kura watakuwa wachache.”
Majaribio ya uandikishaji Jumatatu
Kaimu Katibu Mkuu wa UDP, Isaack Cheyo alisema, “Kuruhusu jeshi
kushiriki siasa ni kuipeleka nchi kubaya, hakuna sababu za msingi ambazo
zimetolewa na Nec.”
Aliongeza: “Huko mbinguni tutaadhibiwa wote lakini
nyinyi ( Nec) mtaanza kupigwa viboko kwanza kwa jambo hili ambalo
mnataka kuwatendea wananchi kwa kuwanyima demokrasia yao.’’
Akijibu hoja za wadau hao, Kamishna wa Nec,
Profesa Amon Chaligha alisema: “Tumesikia malalamiko yenu. Tutayafanyia
kazi hasa kuhusu kutumia askari wa JWTZ.”
Mkuu wa kitengo cha Tehama cha Nec, Dk Sisti Karia
alisema kila mwananchi ataandikishwa katika daftari hilo na hakutakuwa
na makosa kama yaliyotokea miaka ya nyuma.
“Tunajua kuwa kuna maeneo umeme hakuna. Tunapenda
kuwaeleza kuwa mashine hizi za BVR zinatumia umeme wa jua na hivyo
kurahisisha kazi,” alisema.
Alisema hivi karibuni, walizijaribu mashine hizo
katika shule mbalimbali jijini Dar es Salaam kwa kuwaandikisha wanafunzi
na kuanzia saa nane mchana hadi saa 12 jioni waliweza kuandikisha watu
140.
Pia, aliahidi Nec kushirikiana viongozi wa vyama
vya siasa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya mashine hizo mpya
pamoja na mchakato mzima wa uandikishaji.
Majaribio ya uandikishaji Jumatatu
Awali, Makamu Mwenyekiti wa Nec, Jaji Hamid
Mahamoud Hamid alisema uandikishaji wa daftari hilo utatanguliwa na ule
wa majaribio kuanzia Desemba 15 hadi 21 mwaka huu.
Majaribio hayo yatafanyika katika majimbo matatu
ya uchaguzi ambayo ni Kawe (Dar es Salaam), Kilombero (Morogoro) na
Mlele (Katavi).
“Vyama vya siasa vitaruhusiwa kuweka mawakala wao
ili kushuhudia uandikishaji. Mpaka sasa Tume imepata vifaa 107 vya
utambuzi wa mpigakura vya kielektroniki (BVR), vingine vilivyobaki
vitapokewa wiki hii ili kufikia 250. Tukianza rasmi tutatumia BVR
8,000.”
Alisema baada ya uandikishaji kukamilika, daftari
la awali la wapigakura litawekwa wazi ili kama kuna mapingamizi yatolewe
na kushughulikiwa sambamba na kuboresha taarifa za wapigakura.
Wasomi wanena
“Tume inatarajia kuwa Daftari la Kudumu la Wapigakura litakuwa
tayari Aprili 28, 2015. Uandikishaji katika mikoa yote utafanyika kwa
awamu nne katika kila halmashauri ili kutoa fursa ya kuhamisha vifaa vya
uandikishaji kutoka eneo moja kwenda jingine,” alisema.
Alisema muda wa uandikishaji utakuwa siku saba
katika kila kituo na kufanya siku za uandikishaji kuwa 28 kwa kuwa kila
halmashauri itagawanywa mara nne.
“Mgawo huo utatokana na idadi ya vituo vya
kujiandikisha vilivyopo pia idadi ya wapiga kura wanaolengwa
kuandikishwa kwa mujibu wa takwimu za sensa zilizotolewa. Uboreshaji wa
daftari utahusisha wapigakura wote, wapya na wa zamani,” alisema.
Alisema Vitambulisho vya Taifa na vya sasa vya
kupigia kura vitatumika katika uandikishaji ili kurahisisha uchukuaji wa
taarifa za wapigakura.
Wasomi wanena
Profesa wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar
es Salaam (Duce), Kitila Mkumbo alisema ni jambo la kushangaza kwa JWTZ
kusimamia uandikishaji huo kwa kuwa lina mambo mengi ya kufanya.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam,
Dk Benson Bana alisema si mara ya kwanza kutumia jeshi nchini kwenye
masuala ya kisiasa kwani hata mwaka 1995, JWTZ lilitumika kusafirisha
masanduku ya kura.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment