Mitandao ya kijamii ni programu inayotumia
Intaneti kuwezesha watu mbalimbali kuwasiliana, kushiriki mijadala na
kuweka taarifa au kubadilishana vitu mbalimbali .
Mfano wa mitandao hii ni kama blogu, chaneli za
youtube, facebook, twitter na nyingine nyingi . Mtu anaweza kutembelea
mitandao ya kijamii kwa kutumia simu ya mkononi,, kompyuta na hata vifaa
vingine vya mawasiliano.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha watumiaji wengi wa
mitandao ya kijamii ni watu walio pweke (single), hivyo wanatumia
mitandao ya kijamii kuwasiliana, kujielezea maisha yao kwa watu na
kuendeleza mambo yao binafsi . Wanaweza kujitosheleza kwa kila kitu kwa
kutumia mitandao ya kijamii isipokuwa kwa vitu vichache kama kula,
kulala, kunywa na vinginevyo.
Kutokana na upweke huu, mtu hatumii mitandao kwa
mambo binafsi tu, lakini pia kwa makundi ambayo yeye yumo. Kwa hivyo,
mtu huyu anaweza kutumia mitandao ya kijamii kwa
maslahi ya kundi na wanachama wa kundi fulani kama vile la uhalifu.
Pia makundi pinzani yanatumia mitandao ya kijamii
kuunganisha wanachama wao na kutumia dhidi ya mahasimu wao kama ni vyama
vya kisiasa, biashara zenye ushindani mkubwa, wanamuziki, makundi ya
kigaidi. Mitandao ya kijamii imewezesha haya yote na jinsi
huduma zinavyozidi kupatikana kwa urahisi na vifaa kupungua bei, watu
wanazidi kujiunga zaidi kwenye mitandao, huku wengine wakiendelea
kupanua zaidi makundi yao.
Utafiti mwingine ulionyesha jinsi jamii inavyozidi
kupata vyombo vya mawasiliano, ndivyo jamii hiyo inavyozidi kuwa kwenye
uwezekano mkubwa zaidi wa kupata madhara ya kihalifu au mwingine
unaohusisha matumizi ya vyombo vya mawasiliano hasa mitandao ya kijamii .
Tishio la kiusalama kutokana na utumiaji wa
mitandao ya kijamii, linaanzia hapa ambapo watu wengi zaidi wanajiunga
kwenye mitandao hii kwa nia mbalimbali na hapa ndipo kila nchi hasa
Tanzania inatakiwa kuangalia maslahi yake kiusalama. Mitandao ya kijamii imekuwa ikitumika na makundi
ya kigaidi kwa shuguli mbalimbali kama kubadilisha watu mitazamo, kupata
wanachama wapya.
Kuwasiliana na kutoa mafunzo, makundi haya
yamekuwa yakitumia zaidi mitandao hii kuwasiliana na makundi mengine ya
kuhalifu kwa ajili ya kukusanya michango kutokana na shughuli haramu.
Uhusiano kati ya makundi ya kigaidi na mengine ya
kihalifu, umekuwa mkubwa katika mitandao ya kijamii. Uhusiano huu
unawezesha makundi ya kigaidi kupata mbinu na njia nyingi za kufanya
shughuli zao.
Pia wanatumia mitandao ya kijamii kusambaza propaganda na
upotoshaji mwingine mwingi kuhusu shughuli za kigaidi na kufanya jamii
ishtuke au kuwa na woga dhidi ya taasisi nyingine kama vyombo vya habari
.
Athari ya woga huu inaweza kuwa wawekezaji kuamua
kutoa mitaji yao kwenye masoko ya hisa, watu kuacha kufanya kazi na
shughuli zingine za kiuchumi na kukimbia kutoka eneo moja kwenda
jingine.
Inahofiwa pia makundi ya kihalifu hasa yale ya
kigaidi, yanaweza kutumia mitandao ya kijamii kusambaza habari za
uwongo kuhusu matukio kama ya tetemeko la ardhi, mafuriko, mlipuko wa
magonjwa ili kuchelewesha uokoaji na kusababisha madhara zaidi kwa jamii
ili hatimaye wapate ushindi.
No comments:
Post a Comment