Pages

Wednesday, December 10, 2014

KWAYA YA MAKONGORO YATIA FORA

Watoto wa halaiki wakipandisha Bendera ya Taifa juu ya ‘Mlima Kilimanjaro’. Maudhui ya wimbo uitwao ‘Chezea Pengine’ yanayokosoa viongozi wasiojali wananchi yaliamsha shangwe kutoka kwa wananchi waliohudhuria sherehe za miaka 53 ya Uhuru wa Tanganyika katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jana.

Wimbo huo wa Kwaya ya AICT Makongoro kutoka Mwanza ulionekana kuwaingia wengi ambao walitingisha vichwa vyao na wengine kupiga makofi kuashiria kukubaliana na maudhui yake.
“Cheo ni dhamana, hakuna aliyezaliwa nacho uliye madarakani yapasa kusimama kwenye haki wala usijidanganye walio chini hawajui kitu, haki ya mnyonge haipotei, bali inacheleweshwa.
“Keki inapokatwa kila mtu aipate, hivyo inapogawiwa ni vyema kila mtu aipate lakini ikiishia juujuu elewa kwamba chini manung’uniko yataanza, mwisho wake ni vurugu, chezea pengine usichezee amani,” ni miongoni mwa maneno yaliyopo kwenye wimbo huo.
Waimbaji hao waliwataka wanasiasa na waandishi wa habari kutokubali kununuliwa na kuwa chanzo cha kupotea amani.
Wananchi wazungumza
Akizungumzia maadhimisho, Mbunge wa Lindi Mjini (CUF), Salum Barwany alisema haoni kama Tanzania imefanikiwa kupambana na maadui wake watatu; ujinga, maradhi na umaskini zaidi ya kuwaongeza hao kufikia watano. Aliwataja maadui wawili wapya kuwa ni rushwa na ufisadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Elaston Mbwilo alisema: “Kwa namna watu wanavyoonekana kuyafuatilia ni dhahiri kuwa uzalendo umeongezeka miongoni mwao. Japokuwa maadhimisho haya bado hayajashika kasi, kwa ngazi za mikoa, wengi hutazama runinga au kusikiliza redio.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Zarina Madabida alisema Watanzania wanafurahishwa na maadhimisho hayo kutokana na vile yanavyoandaliwa kwa kuwa wanapata muda wa kushiriki mambo ya kitaifa.
Mwanasiasa mkongwe, Lepilal Ole Moloimet alisema kwa miaka 53, Taifa limepiga hatua, pia kuna upungufu mwingi... “Leo migogoro imekuwa mingi, hasa ya ardhi na wizi wa fedha za umma, hatukupaswa tuwe hapa.”
Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Edwin Mtei alisema: “Maadhimisho haya yaende sambamba na kasi ya Watanzania kutaka mabadiliko kwani Serikali imechoka,” alisema Mtei ambaye pia ni mwasisi wa Chadema na kuongeza kuwa upungufu mwingi unaoonekana sasa ungeweza kupatiwa ufumbuzi na Serikali kama ingekuwa na dhamira ya dhati.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo ole Nangole alisema miaka 53 ni ya kujivunia kwa kuwa na Taifa lenye amani na utulivu.
Mfanyabiashara John Minja wa Arusha alisema pamoja na umri mrefu, umaskini umeongezeka hasa vijijini, rasilimali bado zinanufaisha wachache na viongozi wamekuwa wakididimiza Taifa kwa mikataba isiyo na faida kwa wananchi,” alisema Minja.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment