Watoto wa halaiki wakipandisha Bendera ya Taifa juu ya ‘Mlima Kilimanjaro’. Maudhui ya wimbo
uitwao ‘Chezea Pengine’ yanayokosoa viongozi wasiojali wananchi
yaliamsha shangwe kutoka kwa wananchi waliohudhuria sherehe za miaka 53
ya Uhuru wa Tanganyika katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jana.
Wimbo huo wa Kwaya ya AICT Makongoro kutoka Mwanza
ulionekana kuwaingia wengi ambao walitingisha vichwa vyao na wengine
kupiga makofi kuashiria kukubaliana na maudhui yake.
“Cheo ni dhamana, hakuna aliyezaliwa nacho uliye
madarakani yapasa kusimama kwenye haki wala usijidanganye walio chini
hawajui kitu, haki ya mnyonge haipotei, bali inacheleweshwa.
“Keki inapokatwa kila mtu aipate, hivyo
inapogawiwa ni vyema kila mtu aipate lakini ikiishia juujuu elewa kwamba
chini manung’uniko yataanza, mwisho wake ni vurugu, chezea pengine
usichezee amani,” ni miongoni mwa maneno yaliyopo kwenye wimbo huo.
Waimbaji hao waliwataka wanasiasa na waandishi wa habari kutokubali kununuliwa na kuwa chanzo cha kupotea amani.
Wananchi wazungumza
Akizungumzia maadhimisho, Mbunge wa Lindi Mjini
(CUF), Salum Barwany alisema haoni kama Tanzania imefanikiwa kupambana
na maadui wake watatu; ujinga, maradhi na umaskini zaidi ya kuwaongeza
hao kufikia watano. Aliwataja maadui wawili wapya kuwa ni rushwa na
ufisadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Elaston Mbwilo alisema:
“Kwa namna watu wanavyoonekana kuyafuatilia ni dhahiri kuwa uzalendo
umeongezeka miongoni mwao. Japokuwa maadhimisho haya bado hayajashika
kasi, kwa ngazi za mikoa, wengi hutazama runinga au kusikiliza redio.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Zarina Madabida
alisema Watanzania wanafurahishwa na maadhimisho hayo kutokana na vile
yanavyoandaliwa kwa kuwa wanapata muda wa kushiriki mambo ya kitaifa.
Mwanasiasa mkongwe, Lepilal Ole Moloimet alisema
kwa miaka 53, Taifa limepiga hatua, pia kuna upungufu mwingi... “Leo
migogoro imekuwa mingi, hasa ya ardhi na wizi wa fedha za umma,
hatukupaswa tuwe hapa.”
Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
Edwin Mtei alisema: “Maadhimisho haya yaende sambamba na kasi ya
Watanzania kutaka mabadiliko kwani Serikali imechoka,” alisema Mtei
ambaye pia ni mwasisi wa Chadema na kuongeza kuwa upungufu mwingi
unaoonekana sasa ungeweza kupatiwa ufumbuzi na Serikali kama ingekuwa na
dhamira ya dhati.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo ole Nangole alisema miaka 53 ni ya kujivunia kwa kuwa na Taifa lenye amani na utulivu.
CHANZO: MWANANCHI
Mfanyabiashara John Minja wa Arusha alisema pamoja na umri
mrefu, umaskini umeongezeka hasa vijijini, rasilimali bado zinanufaisha
wachache na viongozi wamekuwa wakididimiza Taifa kwa mikataba isiyo na
faida kwa wananchi,” alisema Minja.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment