Pages

Tuesday, November 18, 2014

MAJIBU YA MAWAZIRI YACHEFUA WABUNGE

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai
Bunge limeingilia kati kushughulikia tatizo la mawaziri, ambalo kwa muda mrefu limekuwa likilalamikiwa na wabunge la kutoa majibu yenye utata na yasiyotosheleza kiasi cha kuacha maswali kuhusiana na masuala ya maendeleo na ya kitaifa.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliliambia Bunge jana kuwa kutokana na tatizo hilo kulalamikiwa na wabunge kwa muda mrefu, Kamati ya Uongozi wa Bunge ilikaa na Serikali na kuzungumzia kuhusu kuboresha majibu ya serikali.
“Kuhusu uboreshaji wa majibu ya serikali tulikaa Kamati ya Uongozi na serikali, tukazungumza nao na tukakubaliana kwamba, katika siku zinazokuja, majibu yatakuwa bora zaidi,” alisema Ndugai.
Aliongeza: “Nilipenda tu nilifahamishe Bunge katika eneo hilo, ambalo mmekuwa mkililalamikia sana la majibu kwamba, hayana uzito mkubwa zaidi.”
Alisema hayo baada ya Mbunge wa Chonga (CUF), Haroub Muhammed Shamis, kuonyesha kutoridhishwa na majibu yaliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani, kuhusiana na kesi iliyokuwa ikiwakabili baadhi ya watuhumiwa wa ugaidi kuondolewa mahakamani.
Pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, aliungana na mbunge huyo akisema majibu yaliyotolewa na Waziri Kombani yaliacha maswali.
Haroub alionyesha kutoridhishwa na majibu ya Waziri Kombani kupitia mwongozo alioumba bungeni chini ya kanuni ya Bunge ya 68 (7) na 46 (1), ambayo inasema: “Waziri anayeulizwa swali atakuwa na wajibu wa kujibu swali hilo kwa ukamilifu kama lilivyoulizwa.”
Kutokana na kanuni hiyo, alisema swali la nyongeza alilouliza katika kipindi cha maswali na majibu bungeni jana, lilikuwa linaitaka serikali iwataje wafadhili wa watuhumiwa wa ugaidi waliokamatwa.
Alisema yeye aliwataja kuwa walikuwa ni wageni, lakini la kushangaza, waziri katika jibu lake naye pia akasema kuwa watu hao waliokamatwa ni wageni.
 “...Ndiyo majibu ya serikali haya? Mheshimiwa naibu spika, naomba mwongozo wako juu ya jibu hili (la waziri),” alisema Haroub.
Baada kuomba mwongozo huo, Jaji Werema alisimama pamoja na mambo mengine, alisema: "Lakini nakubaliana kwamba, pengine majibu (ya waziri) yalikuwa hayatoshelezi."
Baadaye, Waziri Kombani alisimama na kusisistiza kuwa ana uhakika na jibu alilolitoa.

LUGOLA
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), amesema kuwa hatua ya wananchi wa jimbo lake kukosa mbegu za pamba huku Wizara ya Kilimo ikiwa kimya na hata kumfanya apate hasira na kwenda kuwahamasisha wananchi ili waingie bungeni  na kwenda kumng’oa kwa nguvu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Chistopher Chiza na naibu wake, Godfrey Zambi.
Alisema katu siyo nia yake kufanya kama yaliyotokea nchini Burkinafaso baada ya wananchi kuvamia Bunge na kwenda kuing’oa serikali kwa nguvu.Alitoa kauli hiyo jana ijana alipokuwa akiomba mwongozo wa Spika kuhusu hatua ya wizara hiyo kushindwa kupeleka mbegu za pamba, huku msimu wa
kupanda mbegu hizo ukiwa umebakisha siku nane.
Alisema hatua hiyo inamfanya atumie nguvu yake ya kumwondoa waziri huyo mzigo, “Mimi binafsi sina chuki binafsi na Waziri wa Kilimo wala Naibu wake Zambi ila ni kutokana na utendaji wao, hadi sasa wana Mwibara hawajapata hata kijiko kimoja cha mbegu ya Pamba.
“Ingawa Mheshimiwa Werema anatuambia tutumie lugha stahaha lakini hatuna  namna kutokana na hali namna ilivyo.Sasa zimebaki siku nane za msimu wa kupanda mbegu za pamba lakini hatuna namna ya kufanya au ninashawishika kutumia kama yale yaliyotokea Burkinafaso ya kwenda kuwahamasisha wananchi ili waje kuwavamia hapa
na kuundoa mzigo huu.
“Sitaki kufikia huko lakini Waziri ni mzigo, sasa zimebaki siku nane sina la kufanya ninaomba Mheshimiwa Naibu Spika nisaidie kwa hili,” alisema
 Lugola.
Hivi karibuni, Mbunge wa Ludewa, Deo  Filikunjombe (CCM), aliliomba Bunge kubadilisha kanuni ili mawaziri wanaoshindwa kujibu maswali ya wabunge wachapwe viboko.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment