Pages

Tuesday, November 18, 2014

BOT YAAGIZA BENKI KUHAKIKI MIFUMO YA FEDHA

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema taasisi za fedha nchini  zinapaswa kuhakikisha mifumo yao ya  fedha inakuwa imara na salama kwa wateja wake ili kupunguza wizi wa fedha kwa njia ya mitandao.
Aidha, BoT imesema zoezi la kuhakiki taarifa za kibenki kwa wateja haliwezi kusitishwa bali litakuwa endelevu.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Benki, Agapit Kobello, alisema BoT inahimiza benki kuhakikisha wakati wote zinakuwa na kanuni, taratibu na teknolojia imara za mawasiliano na mifumo ambayo ni ya usalama ili kuepusha wateja wake kutoka kwenye majanga.
Alisema zoezi la kuhakiki taarifa za kibenki litaendelea kufanyika  ili kuhakikisha benki zinakuwa na taarifa sahihi za wateja kwa kuwa taarifa za wateja zinabadilika mara kwa mara.
Kobello alisema katika utekelezaji wa majukumu yake ya usimamizi wa mabenki, BoT  imekuwa ikiwasiliana na benki zote  kufuatilia mambo mbalimbali likiwamo la usalama wa mifumo ya malipo.
“Ni wajibu wa kila benki kuhakikisha kwamba mifumo yake ya fedha ni imara na salama kwa wateja wake wote. Benki Kuu ya Tanzania inasimamia na kutoa sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zinazowezesha benki kuendesha shughuli zake kwa ufasaha na ufanisi, ili kuleta maendeleo kwa nchi na wananchi kwa ujumla ,” alisema  Kobello.
Baadhi ya hatua zilizochukuliwa ni benki  kufunga mitambo ya kuzuia na kubaini wezi, kutunza kumbukumbu za matukio yote ya wizi, kuweka vioo vizuia risasi katika madirisha ya kuchukulia fedha, matawi yote ya benki kulindwa na walinzi wenye silaha za moto, watoa huduma ndani ya matawi ya benki kuwa na vifaa vya kutoa taarifa kwa siri wakati tukio la wizi linaendelea.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment