Pages

Tuesday, November 18, 2014

DK. MENGI ATWAA TUZO YA MAFANIKIO AFRIKA

Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, akionyesha Tuzo ya Mafanikio ya Kutukuka katika Maisha barani Afrika mara baada ya kutuzwa katika fainali ya tuzo hizo zilizoandaliwa na CNBC kwa Wafanyabiashara wa Afrika jijini Johannesburg, Afrika Kusini mwishoni mwa wiki.
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, ameshinda Tuzo ya Mafanikio ya Kutukuka katika Maisha kwa mwaka 2014 katika fainali za tuzo hizo barani Afrika.
Alitangazwa kushinda tuzo hiyo jijini Johannesburg, Afrika Kusini wiki iliyopita katika fainali za CNBC All Africa Business Leadership Awards (AABLA), zilizohudhuriwa na wafanyabiashara mashuhuri barani Afrika na maeneo mengine duniani.
Katika hotuba yake ya kukubali tuzo hiyo Dk. Mengi alisema kwamba anaitoa kwa vijana wa Afrika ili iwe chachu ya kuwafanya waamini kuwa wanaweza kubadili hali zao na kujikomboa dhidi ya minyororo ya umasikini.
Pia aliwataka wajasiriamali vijana kuwa macho yanapoona fursa za kibiashara na wawe tayari kufanya kazi kwa bidii bila kukata tamaa.
“Vijana msisubiri kuisaidia jamii, isaidieni... mafanikio ya kibiashara yanakwenda na wajibu wa kurejesha sehemu ya mafanikio hayo kwa jamii.”
Pia alisema kuna njia nyingi za kuwa tajiri bila kujiingiza kwenye mambo ya rushwa. Alisema wakati umefika kwa Waafrika kuamka kutoka kwenye lindi la uongo uliosukwa kwao kwa miaka mingi kwamba bara la Afrika ni maskini.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa kundi la Kampuni za ABN, Roberta Naicker, alisema mchakato wa tuzo za mwaka huu ambazo ni za nne tangu zianze kutolewa, ulikwenda vyema hasa kutokana na kuwa na washiriki wa kiwango cha juu.
Alisema ABN inayojihusisha na masuala ya mawasiliano, inawapongeza wote walioshiriki na kuonyesha umahiri wao katika maeneo yao kiasi cha kutimiza ndoto za wafanyabiashara wa Afrika.
”Tupo hapa kusherehekea ufanisi wa uongozi katika taasisi za Afrika. Wakati tunasubiri matokeo kutoka kwa majaji napenda kuwapongeza wale wote waliofikia fainali katika tuzo hizi …” alisema mwanzilishi mwenza wa ABN na Makamu Mwenyekiti, Rakesh Wahi.
Msemaji mkuu katika hafla hiyo mjumbe wa Baraza la Utendaji la Maendeleo ya Uchumi, Gauteng (MEC), Lebogang Maile, alisema kuwa AABLA ni taasisi muhimu katika kufanikisha uhuru wa kiuchumi kwa bara la Afrika.
Tuzo ya Mafanikio ya Kutukuka Maishani hutolewa kwa mtu ambaye amefanya vyema katika kutekeleza maono ya kibiashara katika bara la Afrika na kuonyesha uthubutu na ujasiri katika kufikia mafanikio.
Tuzo ya mfanyabiashara wa mwaka ilitwaliwa na Ofisa Mtendaji wa EOH ya Afrika Kusini, Asher Bohbot ; wakati tuzo ya mfanyabiashara mwanamke imekwenda kwa Ofisa Mtendaji wa Keroche Breweries  ya Kenya, Tabitha Karanja.
Gil Oved na Ran Neu-Ner ambao ni maofisa watendaji wa kampuni ya ushauri wa masoko ya Afrika Kusini, Creative Counsel walinyakua tuzo ya wafanyabiashara vijana, wakati mwanzilishi wa kampuni ya uwekezaji Brimstone Investment Corporation, Fred Robertson, alipata Tuzo ya Mjasiriamali wa mwaka.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment