Pages

Wednesday, November 19, 2014

BARABARA YA JUU KUJENGWA SALENDER MWAKANI

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Mgufuli akiangalia ramani ya barabara za juu katika daraja la Salender litakalo kuwa na urefu wa kilomita 1.03. Tatizo la msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam, linaendelea kupatiwa ufumbuzi baada ya Serikali ya Tanzania na Korea Kusini kukubalina kujenga barabara za juu katika daraja la Salender litakalo kuwa na urefu wa kilomita 1.03
Ujenzi huo utaghalimu kiasi cha Sh. bilioni 110, utachukua muda wa miaka miwili kumalizika na unatarajia kuanza muda wowote mwakani.
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Mgufuli, alitangaza mpango huo jijini Dar es Salaam jana aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akieleza mikakati ya serikali kupunguza msongamano.
Alisema Korea Kusini itachangia asilimia 80 ya ujenzi na asilimia 20 itachangiwa na serikali ya Tanzania.
“Lile daraja la Salender lililopo kwa sasa halitavunjwa, tutaliacha ila litajengwa lingine la kisasa pembeni, hakutakuwa na foleni tena katika eneo lile,” alisema.
Pia, alisema itajengwa barabara yenye urefu wa kilomita 7.2 itakayoanzia Coco Beach kupitia baharini hadi Aghakan na kuungana na barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
Dk. Magufuli alisema flyover hiyo itakuwa na uwezo wa kupitisha magari zaidi ya 61,000 kwa siku na itakuwa na njia  nne za magari, sehemu ya waenda kwa miguu na baiskeli.
Alisema daraja lililopo sasa linapitisha zaidi ya magari 51,000 kwa siku, na kueleza kuwa kujengwa kwa barabara hiyo ya juu kutasaidia kupitisha zaidi ya magari 112,000 kwa siku.
“Novemba 15 mwaka huu  wataalamu kutoka Korea Kusini walikamilisha utafiti wa flyover hiyo, kilichobakia sasa ni kutolewa kwa fedha tu na ujenzi uanze mara moja,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema katika miaka ijayo Jiji la Dar es Salaam litakuwa na flyover nyingi na za kisasa ambazo hazijawahi kujengwa Afrika Mashariki na Kati.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale, alisema daraja hilo litakuwa na upana wa mita 27.
Alisema hatua iliyobaki kwa sasa ni kuandikishiana mikataba kwa kuwa michoro na utafiti umeshafanyika.
Hadi sasa Serikali imeshatoa ahadi ya ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara kadhaa  jijini  Dar es Salaam ikiwamo eneo la Ubungo itakayoghalimu kati ya  Sh. bilioni 46 na 50.
Sehemu nyingine ni makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere (Tazara) zaidi ya Sh. bilioni 100 zitatumika.
Eneo lingine ni ujenzi wa daraja la Kigamboni ambako Sh. bilioni 214 kinatarajiwa kutumika kujenga daraja hilo lenye urefu wa meta 680.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment