Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini kupitia
Chama cha NCCR-Mageuzi David Kafulila, ambaye ametangazwa kushindwa
katika jimbo hilo uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu,
ameibuka na kusema anakusudia kwenda mahakamani ili atangazwe kuwa
mshindi wa jimbo hilo.
Amedai kwa mujibu wa kura alizokusanya kupitia mawakala wake katika
vituo 182, alishinda kwa kura 34,149 dhidi ya mgombea wa Chama cha
Mapinduzi (CCM), Husna Mwilima, aliyepata kura 32,982, lakini tume
ikamtangaza kuwa mshindi.
Kafulila alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza
na waandishi wa habari kuhusiana na uchaguzi huo, akidai ameporwa
ushindi wake na nguvu ya dola imetumika kuhakikisha anakosa ushindi huo.
“Ninachofahamu mimi ni Mbunge wa Kigoma Kusini, ila nilihujumiwa na
watumishi wa tume kwa kubadili matokeo yangu na kumtangaza mgombea wa
CCM kuwa ni mshindi, hivyo nitaenda Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kudai
haki yangu na kutangazwa mshindi,” alisema Kafulila.
Alisema atakachokifuata mahakamani siyo kurudiwa kwa uchaguzi bali
kuiomba mahakama kumtangaza mshindi kwani ana vielelezo vyote.
“Wiki ijayo nitakuwa nimekamilisha mipango ya kwenda mahakamani,
nina fomu zote 382 kutoka katika kila kata, vituo 182 vilivyotumika
kupiga kura zinazoonyesha idadi ya kura zangu. Nina imani mahakama
haitatumia mlolongo mrefu kutoa hukumu kwa sababu nina vielelezo vya
kutosha,” alisema Kafulila.
Aliwataka wananchi wa jimbo hilo kutokata tamaa na taarifa za
kukosa ubunge wake na kuwataka kuwa wavumilivu wakati wakisubiri maamuzi
ya mahakama.
KASHFA YA ESCROW
Kafulila alipoulizwa sababu anayodhani kumkosesha jimbo hilo au
kuibiwa ushindi kama alivyodai, alisema kutokana na kazi kubwa
aliyoifanya Bunge lililopita ya kuibua masuala ya ufisadi ikiwamo sakata
la Tegeta Escrow.
Alidai kudhibitisha kuwa njama zilitumika, aliwekewa ulinzi mkali
wa dola wakati wa upigaji kura na kipindi cha kusubiri matokeo. “Nguvu ya dola ilitumika sana ili kuhakikisha Kafulila ninashindwa,
polisi walikuwa ni wengi sana pia matokeo yalichelewa kutangazwa isivyo
kawaida,” alisema.
Kafulila alisema alishangazwa na kitendo cha mawakala wa tume
kuahirisha kazi ya ujumuishaji wa kura mara kwa mara licha ya sheria ya
uchaguzi kutoruhusu. “Kazi ya ujumuishaji ilikuwa ikiahirishwa mara mbili na wakati
mwingine kuchukua zaidi ya saa 7 na saa 10 hali ambayo siyo ya kawaida,”
alidai Kafulila.
Akizungumzia hatma yake juu ya kupiga vita ufisadi, Kafulila alisema ataendelea na harakati hizo.
Alisema kwa sasa anaandaa vitabu vinavyozungumzia ufisadi kikiwamo
kinachoitwa ‘Escrow Unfinished Business’, ambacho kinaelezea vizuri
masuala hayo ambayo amekuwa akiyapiga vita.
Uchaguzi mkuu ulifanyika Oktoba 25, mwaka huu, katika Jimbo la
Kigoma Kusini, Mwilima wa CCM alitangazwa mshindi kwa kupata kura
34,453, dhidi ya Kafulila aliyepata kura 33,382.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment