Shirikisho la wenye Viwanda nchini (CTI),
limempongeza Rais mteule, Dk. John Magufuli, kufuatia ushindi alioupata
kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa CTI,
Leodegar Tenga, alimpongeza pia Samia Suluhu Hassan, kuwa
mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Makamu wa Rais hapa nchini.
“Kwa niaba ya CTI na mimi binafsi, napenda kuwasilisha pongezi zetu
za dhati kwa Dk. John Magufuli, kwa ushindi alioupata. Ushindi huu ni
kiashiria tosha cha imani kubwa waliyonayo Watanzania kwake,’’ alisema
Tenga.
Alibainisha kuwa pamoja na kujipanga kushirikiana kwa ukamilifu na
serikali ijayo ya Dk. Magufuli, CTI inaamini kuwa sekta ya viwanda
nchini ina uhakika wa kufanya vizuri zaidi kutokana na msimamo
aliouonyesha Dk. Magufuli wakati akiwaomba Watanzania ridhaa
aliyopatiwa.
“Tulikuwa tukifuatilia kwa ukaribu ahadi za wagombea wote
walizokuwa wanazitoa wakati wa kampeni na kinachotupa faraja zaidi ni
kwamba miongoni mwa ahadi kubwa aliyozisisitiza Dk. Magufuli ni kuigeuza
Tanzania kuwa nchi inayotegemea uchumi wa viwanda…tupo tayari
kushirikiana naye kwenye hilo,’’ aliongeza.
Akitoa maoni yake kwa serikali ijayo juu ya namna ya kufanikisha
hilo, Tenga aliyataja baadhi ya maeneo muhimu yanayohitaji kutazamwa
upya kuwa ni pamoja na uwapo wa mfumo wa kodi usiobadilika badilika.
“Kwa sasa mapato mengi ya serikali yanatoka kwenye kundi dogo la
walipa kodi na kwa maoni yetu tunaona kundi hili dogo limekuwa
likibebeshwa mzigo mkubwa wa kodi kuliko uwezo wake na matokeo yake
taifa limeshindwa kutimiza mapato yanayohitajika kuleta tija kwa
taifa,’’ alisema.
Alisema kwa sasa sekta ya viwanda na biashara inakabiliwa na
changamoto ya wingi wa kodi huku akitoa wito kwa serikali kuangalia
namna ya kupunguza idadi ya mamlaka zinazofanya majukumu yanayofanana
ili kupunguza urasimu na mzigo mkubwa wa kodi kwa wafanyabiashara
nchini.
Aidha, Tenga alitaja changamoto nyingine kuwa ni suala zima la
ukosefu wa miundombunu imara kwenye sekta ya uchukuzi huku akisisitiza
haja ya uboreshaji kwenye usafiri wa reli nchini, mfumo wa barabara na
uwapo wa nishati ya umeme wa uhakika sambamba na upatikanaji wa maji ya
kutosha.
“Kuna haja ya kuboresha zaidi reli yetu na kuiweka kwenye kiwango
cha kisasa zaidi. Pia ipo haja ya kuboresha muundo wa uingizaji na
utoaji wa mizigo kwenye bandari zetu na hili liende sambamba na
kuboreshwa kwa utendaji wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) pamoja na
Mamlaka ya Bandari nchini (TPA),’’ alisema.
Aliongeza kuwa upo umuhimu mkubwa wa serikali ijayo kuangalia upya
upatikanaji wa mikopo kwa wajasiriamali hasa wenye biashara na viwanda
vya kati na vidogo.
Tenga alisema kwa sasa suala la upatikanaji wa mikopo ni changamoto
kubwa kwa kuwa linahusisha masharti mengi sambamba na riba kubwa, jambo
linalokwamisha ukuaji wa viwanda kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Tenga, ni muhimu kwa serikali hiyo kuhakikisha
inawapa kipaumbele wawekezaji wazalendo wanaoonyesha nia ya kushiriki
kwenye uwekezaji wa rasilimali zinazogunduliwa hapa nchini
hususanimadini na gesi ili kuondoa tishio la sekta hiyo kunufaisha zaidi
raia wa kigeni.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment