Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sezibela.
Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),
wameishauri serikali ya Burundi kusogeza mbele mwezi mmoja na nusu
uchaguzi mkuu nchini humo.
Uchaguzi wa wabunge ulitarajiwa kufanyika Ijumaa wiki hii na wa urais ukipangwa kufanyika mwezi huu. Hatua hiyo imetokana na kutoimarika kwa hali ya amani na utulivu
kufuatia baadhi ya vyama vya upinzani na mashirika yasiyo ya kiserikali
kuendelea na maandamano kupinga hatua ya Rais wa nchi hiyo, Pierre
Nkurunziza, kutangaza kuwania urais kwa muhula wa tatu.
Taarifa ya kuomba kusogezwa mbele kwa uchaguzi huo ilitolewa jana
na wakuu wa nchi hizo katika mkutano wao uliofanyika jana jijini Dar es
Salaam. Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sezibela, alisema wakuu hao
waliishauri serikali ya Burundi kusogeza uchaguzi huo kutokana na nchi
hiyo kutotengemaa kisiasa.
Alisema wakuu hao pia walitoa wito kwa makundi yenye silaha kuziweka chini. Pia, waliishauri serikali ya Burundi kuwarejesha raia wake wote waliokimbilia nchi jirani.
Kadhalika, walitoa wito kwa serikali ya nchi hiyo kukutana na makundi hayo ili kurejesha amani na utulivu. Dk. Sezibera alisema wakuu wa EAC pia walitoa wito kwa wadau wa
amani ukiwamo Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU), kuingilia
kati mgogoro huo.
Waliohudhuria mkutano huo ni Mwenyekiti wa AEC, Rais Jakaya Kikwete
(Tanzania); Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta; Rais wa Uganda, Yoweri
Museveni huku Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, akihudhuria kama mlezi
wa Burundi.
Rwanda iliwakilishwa na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Valentine
Rugwaiza huku Burundi ikiwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Allen
Nyamizwe.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment