Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.
Wabunge wa Kambi ya Upinzani jana waliendeleza
mashambulizi ya kuikejeli serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba
imechoka katika kuwaletea maendeleo Watanzania.
Mashambulizi hayo yalianzishwa juzi jioni na Mbunge wa Singida
Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ambaye alitamka bungeni kuwa serikali
imechoka. Jana akichangia hotuba ya mwelekeo wa kazi za serikali, makadirio
ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge kwa mwaka 2015/16
iliyowasilishwa na Mizengo Pinda juzi,Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema),
Mchungaji Peter Msigwa, alisema adui namba moja wa usalama wa taifa ni
CCM.
Akichangia kwa maneno na hisia kali, Mchungaji Msigwa alisema:
“Serikali ya CCM siyo taifa…hapa tunazungumzia maslahi ya taifa.
Serikali hii imechoka na tunataendelea kusema hivyo hata kama inaumiza
masikioni mwenu.”
Alisisitiza kuwa serikali ya CCM ni hatari kwa usalama wa taifa na
kutoa mfano kwamba, katika kipindi cha mwaka mmoja, kumekuwa na kauli
tofauti zinazotolewa na viongozi wa juu serikalini na kusababisha
serikali hiyo kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo.
Alisema kwa mfano, serikali ya CCM imeshindwa kuratibu kura ya
maoni ya Katiba Inayopendekezwa, kuendelea na mchakato wa vitambulisho
vya taifa na pia imeboronga kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa na
sasa uandikishaji wapigakura katika daftari la kudumu la wapigakura
unasuasua.
“Hatuwezi kuwa na viongozi wenye ndimi mbili. Katika Bunge Maalum
la Katiba, hapakuwa na theluthi mbili kutoka Zanzibar, yaani kura
hazikupigwa. Ni serikali ya ajabu kabisa hii. Tukisema hamna upeo
mnakasirika. Sisi Ukawa tulitoka katika Bunge hilo na kuwaachieni
muendelee nalo, lakini mmeshindwa,” alisema Mchungaji Msigwa.
Hata hivyo, alisema ana imani na usalama wa taifa, kwani
haujapooza, isipokuwa baadhi ya viongozi waliopo madarakani, ambao ni
dhaifu wamekuwa hatari zaidi kuliko uhalifu. “Hivi mna ujasiri gani kusema hamjachoka? Tazama, katika serikali
hii mmebadilisha mawaziri wengi tu hapa. Ndugu yangu safari hii kama
hukubahatika kupata uwaziri ndiyo basi tena, hupati tena. Yaani kila
aliyewekwa uwaziri ilikuwa ni shida tu,” alisema.
Alisema serikali ya CCM imegombana na walimu, ambao awali walikuwa
marafiki zao, lakini kama hiyo haitoshi, sasa wanagombana hata na
madereva wa mabasi.
Naye Pauline Gekul (Viti Maalum-Chadema), alimshambulia Mbunge wa
Sikonge (CCM), Said Nkumba, ambaye alipopata nafasi ya kuchangia,
alianza kuwashambulia makatibu wakuu wa vyama vya CUF, Maalim Seif
Sharif Hamad; Chadema, Dk. Willibrod Slaa, dhidi ya Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana.
Nkumba alidai makatibu hao wa upinzani wamechoka na kwamba hawawezi kushindana na Kinana kwa mbio za umbali wa kilomita tano. Katika mchango wake, Gekul alisema wanaposema kuchoka kwa serikali
siyo kiafya, ila ni katika uendeshaji wake na kutekeleza miradi ya
maendeleo kwa wananchi.
“Uchovu wa serikali tunaouzungumzia hapa siyo wa afya, bali ni
kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi, kuwa na mipango
mibovu na mambo mengi. Uchovu huo unadhihirishwa kupitia wizara hii ya
Waziri Mkuu. Tamisemi ina watu na hao ndiyo Watanganyika, lakini
asilimia 28 tu ya miradi ndiyo inayopelekwa halmashauri. Huo ndiyo
uchovu. Mikoa inapewa asilimia 17 tu kutekeleza miradi ya maendeleo kwa
wananchi,” alisema Gekul.
Aliongeza: “Tukisema serikali imechoka hao (wabunge wa CCM) ndiyo wanataka kuruka kwenye viti kutetea.” Alihoji sababu za kutopeleka fedha halmashauri kwa sababu miradi mingi inakwama kwa kukosa fedha.
Katika hatua nyingine, aliwataka wabunge wa CCM kutobeza Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa sababu vyama vilivyounda umoja huo ndiyo
kimbilio la wananchi na kuonya kuwa Watanzania hawataridhika kuona
uchaguzi mkuu unasogezwa mbele.
Kuhusu uchaguzi mkuu, alisema serikali kwa muda mrefu imekuwa ikicheza na wanafunzi wa vyuo vikuu. Alisema mara nyingi serikali imekuwa ikiwaandikisha wanafunzi wa
vyuo vikuu wakiwa vyuoni, lakini wakati wa uchaguzi vyuo vinafungwa hali
ambayo inawafanya washindwe kurudi maeneo walikojiandikisha kupiga
kura.
Aliitaka serikali kutoa majibu iwapo itafunga vyuo wakati wa
uchaguzi mkuu au la ili wanafunzi hao wapate haki yao ya kikatiba ya
kupiga kura. Akizungumzia mambo ambayo wananchi wataikumbuka serikali ya
CCM, Gekul alitaja ni kushindwa kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi,
kushindwa kuwawezesha wananchi hadi kuamua kujiundia vicoba, kushindwa
kutekeleza miradi ya maendeleo na watakumbukwa kwa bajeti hewa.
Mbunge mwingine, Conjesta Rwamlaza, alisema kama wapo wabunge ambao
wamekasirika kwa kuambiwa serikali imechoka, basi waifanyie ‘masaji’. “Ukiambiwa serikali imechoka, usikasirike. Nenda kaifanyie masaji,” alisema.
Mapema katika mchango wake, Nkumba alisema: “Ukiona watu wanaungana kwenye vita hao ndiyo dhaifu, wamechoka. “Wameamua kuunganisha nguvu ili kupambana na CCM. Lakini huwezi kwenda Ikulu bila kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa.
Huwezi kukabidhiwa nchi kama hujui maendeleo yaliyopo tangu tupate
uhuru hadi leo. Tumefanya vizuri katika ujenzi wa barabara, katika elimu
na mambo mengi,” alisema Nkumba akimuunga mkono Mbunge wa Moshi
Vijijini (CCM), Dk. Cyril Chami.
Dk. Chami katika mchango wake alionyesha kukerwa na kauli kwamba
serikali imechoka na kusema serikali imeleta maendeleo katika sekta
nyingi nchini. Alitaja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni barabara, ujenzi wa shule na maabara.
Mbunge wa Mafia, Abdulkarim Shah, alisema Serikali ya CCM imefanya mambo mengi kuwaletea maendeleo wananchi. “Tumefanya mengi. Sitaki kuingia sana kwa undani. Kwa hao wanaosema tumechoka, hayo ni maneno tu,” alisema Shah.
Jumatatu wiki hii, Lissu aliibua kauli ya serikali imechoka katika mchango wake bungeni. Aliionya serikali kuhusu mpango wa kuahirisha uchaguzi akisema
haitawezakana kwa vile ni vita pekee ndiyo inayokubalika kikatiba
kuahirisha uchaguzi. Alisema serikali chovu imeshindwa kukamilisha kura ya maoni,
kadhalika hadi sasa imebakia miezi mitano imeshindwa kuandikisha
wapigakura.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment