Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amepokea msaada wa
vitabu 895 vyenye thamani ya Sh. milioni 6.5/- ikiwa ni jitihada ya
wadau mbalimbali kuchangia Shule ya Msingi aliyosoma ya Kakuni iliyoko
kijiji cha Kibaoni Wilaya ya Mlele mkoani Katavi.
Pinda alipokea msaada huo juzi kwenye Shule mpya ya Msingi Kakuni
ambayo bado inaendelea kujengwa kwenye kijiji cha Kibaoni. Akizungumza
katika hafla hiyo fupi baada ya kupokea msaada huo, Waziri Mkuu
aliishukuru kampuni ya General Booksellers Ltd ya Dar es Salaam kwa
msaada huo ambao alisema utachangia kwa kiasi kikubwa kutimiza ndoto
yake aliyokuwa nayo ya kuisaidia jamii iliyomsomesha.
“Wazo la ujenzi wa Shule mpya ya Msingi Kibaoni lilitokana na
ukweli kwamba nilisoma na kumaliza kwenye shule hii ya Kakuni. Nikiwa ni
mtumishi wa serikali, Mbunge na sasa Waziri Mkuu, nilijiuliza hivi
shule hii ninaweza kuiacha hivi hivi?,” alisema na kuhoji.
Aliongeza: “Nilijiuliza sana, ni jambo gani ambalo naweza kulifanya
la kusaidia wanakijiji wenzangu na kata nzima ya Kibaoni kama shukrani
kwa kunilea na kunifikisha hapa nilipo. Ndipo wazo la kujenga shule
niliyosoma likazaliwa kama mwaka mmoja na nusu uliopita,” alisema Pinda
wakati akiwahutubia wazazi, walimu na wanafunzi.
Awali, akiwasilisha msaada huo, mwakilishi wa kampuni ya General
Booksellers Ltd, Bw. Joachim Masaburi alisema wameamua kuchangia vitabu
hivyo kwa kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto lakini pia wanatambua
juhudi za serikali za kutoa elimu bora.
Akitoa mchanganuo wa vitabu hivyo, Masaburi alisema: “Kuna vitabu
600 kwa ajili ya shule ya awali ambavyo kati yake, 300 ni vya ngazi ya
chini (nursery) na vitabu vingine 300 ni vya ngazi ya juu (pre-school).
Vyote ni vya hisabati, Kiingereza na sayansi."
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment