Dk. Benson Bana.
Wakati mzozo mkubwa umeibuka hivi karibuni juu ya
kile kinachoelezwa kuwa serikali imekuwa ikipuuza maamuzi ya Bunge hasa
kutokana na kinachoendelea nchini kwa sasa juu ya sakata za Escrow,
Tokomeza na Richmond, mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Dk. Benson Bana, amesema kimsingi kinachotokea ni kutokueleweka
kwa dhana ya mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili mitatu ya dola.
Katika mahojiano maalum na NIPASHE wiki hii, Dk. Bana ambaye ni
mtaalamu wa utawala na sayansi ya siasa, alisema kuwa kwa bahati mbaya
kumekuwa na msuguano mkubwa baina ya mihimili miwili, utawala
(Executive) na Bunge (Legislature) kwa kiwango kikubwa nchini kila
muhimili ukitaka kuuthibiti mwingine.
“Kwa bahati nzuri muhimili ambao umesurvive (umebaki salama) ni
mahakama. Ukitazama kwa undani utaona bado muhimili huu hauingiliwi sana
na mingine kama ilivyo kwa msuguano baina ya bunge na utawala,” alisema
Dk. Bana.
Alisema kuwa wakati dhana ya mgawanyo wa madaraka ya dola baina ya
mihimili mitatu ni mkamilishano, kinachoonekana katiba kuendesha mambo
nchini kwa sasa ni: “Kuviziana na kutegeana.” Dk. Bana alisema kuwa hakuna ubishi kwamba Bunge kwa muda sasa
limekuwa likifanya kazi nzuri katika kutimiza wajibu wake, lakini kuna
tatizo moja kubwa juu ya namna mambo mengi yanavyoendeshwa na
kuhitimishwa.
“Kwa nini kwa mfano uchunguzi haufanywi na kuwawajibisha mawaziri
tu ndani ya Bunge ambao wana nafasi ya kujitetea ndani ya Bunge? Kwa
nini mbunge anasimama na kumshughulikia mtendaji ambaye hawezi kujitetea
ndani ya Bunge?” alihoji na kuongeza kuwa: “Dhana ya kudhibiti serikali inaweza kwenda mbali zaidi, hapa
kinachojitokeza ni supremacy (kuwa na nguvu juu ya muhimili mwingine) na
siyo mkamilishano. Kama Bunge linataka kuwa supreme, je, lenyewe
linawajibishwa na nani? Mbona kwenye katiba inayopendekezwa wanakataa
kuwajibishwa na wananchi?” alihoji.
Alisema katika sakata zilizotikisa nchi kama Tokomeza, ni kweli
Kamati ya Bunge iliyochunguza madhila waliyofanyiwa wananchi iliibua
mambo mengi na inasikitisha kwamba wananchi waliuawa, lakini cha
kujiuliza ni kwamba, ni kwa kiwango gani kamati za Bunge zimekuwa na
utaalam wa kuchunguza kila kitu.
Dk. Bana alisema kuwa ili Bunge liweze kutekeleza majukumu yake
sawasawa na kuepuka kuingia katika mtego wa kutetea maslahi binafsi, ni
vema kukawa na vitengo vya kudumu vya utafiti vyenye watalaamu wa
kuendesha uchunguzi ili likitokea jambo, utaalamu wao uwaongoze wabunge
kufikia hitimisho la kina la kile wanachofanya.
Alisema mara kadhaa kumekuwa na dalili za dhahiri za maslahi
binafsi kuteka mijadala katika sakata kadhaa zilizotokea ndani ya Bunge. “Kwa mfano ukifuatilia na kusoma jinsi Mwakyembe (Dk. Harrison) alivyokuwa anawasilisha ripoti ya Richmond mbwembwe zote zile unaona wazi kwamba kulikuwa na mtu anawindwa.
Ukisema mtu ajipime, ajitafakari unaona wazi kwamba hapa ni mtu
anatafutwa katika mazingira haya tunaondoka kwenye hoja tunajadili
personalities (watu),” alisema.
Alisema habari ya kumalizana na kuviziana inawaondoa watu kwenye
hoja na matokeo yake kila anayepata fursa anamshughulikia mwingine na
gharama yake ni kubwa kwa taifa. Dk. Bana alisema hadi sasa suala la Escrow limezidi kuwa zito na kwa maoni yake, bado ni tatizo kubwa.
“Serikali imeshindwa kuliweka sawa jambo hili, kuna wanaoamini
kwamba fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Escrow zote ni za umma. Rais
Kikwete alijaribu kulizungumzia hili, lakini halikupata wa kuli-amplify
(kulipigia debe). Kuna tatizo la mawasiliano ndani ya serikali. Hakuna
communication strategy (mkakati wa mawasiliano),” alisema na kuongeza:
“Umma unataka kujua ni kitu gani hasa kilisababisha ile fast
tracking (kuharakisha) ya kuchukua zile fedha. Suala hili limeanzia
mbali. Ni mkataba mbaya wa IPTL ambao ulianza mwaka 1994 chini ya Mwinyi
(Ali Hassan), akaja Mkapa (Benjamin) na sasa chini ya Kikwete. Kuna
nini hasa ndani ya kitu hiki?” alihoji na kusisitiza kuwa suala hili
bado halijafanyiwa uchunguzi wa kutosha.
“Sitaki kuamini kwamba Takukuru wako makini kwenye suala hili.
Yaani haijulikani nani alikuwa anagawa fedha? Escrow haijaisha bado,”
alisisitiza. Alisema kuwa ni vigumu kina Profesa Muhongo na Eliackim Maswi na
wote walioguswa na sakata la Escrow kurejea katika hali zao za kawaida
mbele ya jamii hata kama kuna juhudi za kuwasafisha. “Maswi
angestaafishwa mapema tu au sijui apelekwe wapi, hata kama ikifanyika
nini, madhara kwa jamii dhidi yake yapo pale pale,” aliongeza.
Wakati Dk. Bana akionyesha madhara ya msuguano wa Bunge na utawala
ambayo kwa kiwango kikubwa yamekuzwa na maslahi binafsi katika kufikia
maamuzi mengi ambayo madhara yake yangeliweza kuepukwa, mchambuzi wa
masuala ya siasa nchini, Alphonce Temba, alisema taarifa kwamba taifa
sasa linadaiwa Sh. bilioni 120 baada ya serikali kushindwa kesi ya
kuvunja mkataba wa Dowans huko Ufaransa katika mahakama ya usuluhishi,
ni janga lingine linaloonyesha jinsi serikali ilivyozingirwa na makundi
kiasi cha kujikuta ikifanya maamuzi bila kuwa makini.
“Kuna matabaka ndani ya CCM. Kila kundi linaweka mitego dhidi ya
lingine. Ni mitego mitego, serikali siyo makini kwa sababu imegubikwa na
mapambano ya makundi, kila moja likitaka kupata. Matokeo yake ni
kutolewa kwa maamuzi ambayo siyo makini na yanayowagharimu wananchi,”
alisema Temba.
“Yaani ndani ya CCM wenyewe kwa wenyewe wanashughulikiana kwa
sababu tu kundi hili linapambana na mwekezaji, huyu afukuzwe kwa sababu
tu wanaamini hakuletwa na kundi lao. Hali hii ni kielelezo cha serikali legelege. Siyo makini. Mwalimu
alisema nchi imejaa nyufa, hii ni kansa inayoangamiza taifa,” alisema.
Temba alisema kuwa kwa kawaida makundi yanye maslahi binafsi hayana
uzalendo ndani yake, hayana wito wa uongozi na katika maamuzi yake
hayajali kwamba mwisho wake ni kuleta hasara kubwa kwa taifa kama ilivyo
sasa kuhusu mkataba wa Dowans ambao nchi inadaiwa Sh. bilioni 120 baada
ya kushindwa kesi.
Mei 12 mwaka huu, Kiongozi wa Kambi ya Upizani Bungeni (KUB),
Freeman Mbowe, akiwasilisha msimamo wa kambi hiyo kuhusu makadirio ya
matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2015/16, pamoja
na mambo mengine alitaka kujua sababu za serikali kuchukizwa sana Bunge
linapotekeleza wajibu wake na kutoa mifano ya juhudi za kuwasafisha
watuhumiwa wa sakata za Tokomeza na Escrow, ambao ambao Bunge
lilichunguza kashfa zao na kuwatia hatiani.
Katika hotuba hiyo iliyojaa makombora mazito dhidi ya udhaifu wa
serikali hasa katika masuala ya uandikishaji wa wapigakura kwa mfumo wa
BVR, Mbowe alisema makundi ndani ya CCM yamekuwa na madhara makubwa kwa
taifa na kutoa mfano wa maamuzi yaliyokuwa yanasukumwa na makundi ya
kugombea madaraka ndani ya chama hicho kiasi cha kukosekana kwa ukweli,
uwazi na haki katika mchakato mzima wa kushughulikia kashfa ya Richmond.
Mbowe alisema wakati umefika kwa Serikali kusimama na kulielezea
Taifa ni nani anasema kweli, ni nani alilidanganya Bunge na ni nani
analindwa na serikali katika kashfa ya Richmond.
Katika hotuba hiyo ambayo Spika wa Bunge, Anne Makinda, alijitahidi
kumzuia Mbowe asisome sehemu hiyo iliyokuwa inaivua nguo serikali na
CCM kwa kisingizio cha muda na kwamba hatambui makubaliano ya kambi ya
upinzani ya kuachiana muda ili hotuba nzima ya KUB isomwe yote na
wananchi waisikie kwa kuwa ilikuwa ikirushwa moja kwa moja na TBC1,
alisema katika mlolongo wa kushindwa kusimamia nchi, kuendekeza makundi
na vita vya kisiasa ndani ya CCM na serikali yake, Taifa sasa linadaiwa
Sh. bilioni 120 baada ya kushindwa kwenye kesi ya Dowans/Richmond katika
Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC) huko Paris, Ufaransa.
“Serikali haijataka kuliweka jambo hili wazi na ni dhahiri kuna
siri kubwa inayosababisha jambo hili kuwa la usiri mkubwa. Huko mbele ya
safari jambo hili litaligharimu Taifa mabilioni haya ya fedha ambayo
yangeweza kuepukika kama ukweli, uwazi na haki vingetawala mchakato
mzima wa kashfa ya Richmond. Serikali isimame sasa na ilieleze Taifa ni
nani anasema kweli, ni nani alilidanganya Bunge na ni nani analindwa na
serikali katika kashfa hii?” alisisitiza.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment