Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya
Dodoma Mjini, Roda Ngimilanga, imemrudishia dhamana Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini, Johnson Minja. Hatua ya kumfutia dhamana mfanyabiashara huyo ilizua mjadala mkali
bungeni juzi, baada ya wabunge wengi kuilalamikia na kuituhumu serikali
kwamba inahusika kuishawishi mahakama kuchukua hatua hiyo. Wabunge hao walitaka Minja arudishiwe dhamana yake ili kuwezesha
kufanyika kwa majadiliano kati ya serikali na wafanyabiashara ambao
walikuwa wamegoma na kufunga maduka katika sehemu mbalimbali za nchi
kushinikiza kiongozi wao arejeshewe dhamana yake. Mahakama hiyo
ilimfutia dhamana kiongozi huyo wa wafanyabiashara na kuamuru awekwe
rumande kwa muda wa wiki moja kwa tuhuma za kuvunja kanuni za dhamana
aliyopewa na mahakama hiyo Januari 28, mwaka huu.
Jana baada ya kusikiliza hoja zilizowasilishwa mahakamani hapo na
pande za utetezi na Jamhuri, Hakimu Ngimilanga alieleza kuwa Mahakama
haioni sababu yoyote ya kuendelea kumshikilia Minja gerezani, kwani
madai yaliyowasilishwa na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Rose Shio,
hayana mashiko ya kisheria ya kumuondolea dhamana Minja.
Aidha, alisema kuwa kwa mujibu wa jalada la kesi hiyo, hakuna
kifungu chochote cha dhamana ambacho mtuhumiwa amekivunja na kwamba kwa
mujibu wa masharti ya dhamana husika, hakuna kifungu chochote
kinachomkataza Minja kufanya mkutano na wanachama wake. “Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kupitia jalada la
kesi, ninatamka kuwa Minja ataendelea kuwa huru kwa masharti ya dhamana
yake ya Shilingi milioni nne na wadhamini wawili,” alisisitiza Hakimu
Ngimilanga.
Kadhalika, alisema kuwa masharti mengi yanayodaiwa kuwa chanzo cha
kufutwa kwa dhamana ya mtuhumiwa katika kesi iliyosomwa mahakamani hapo
wiki moja iliyopita, hayakuandikwa katika jalada la kesi hiyo. Shio aliitaka Mahakama kuendelea kumshikilia mshtakiwa kwa tuhuma
kwamba hali ya amani nchini bado siyo shwari kutokana na migomo ya
wafanyabiashara inayoendelea maeneo mengi nchini.
Pia Shio alidai kuwa wafanyabiashara wengi bado wanaigomea Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) kutumia mashine maalum ya kufanyia malipo
(EFD). Kwa upande wake, Wakili wa Minja, Godfrey Wasonga, aliieleza
Mahakama kuwa kwa mujibu wa ibara (13 (6) b na 15 (1) za Katiba ya nchi,
mteja wake hakustahili kufutiwa dhamana na kuwa jukumu la kuhakikisha
kwamba wafanyabiashara wanafungua maduka siyo la mteja wake, bali la
Jeshi la Polisi.
Hata hivyo, mwanasheria huyo aliiambia Mahakama kuwa kama kweli
mteja wake alikuwa na makosa ambayo yalisababisha kufutiwa dhamana,
Polisi walitakiwa kumkamata wakati ule ule walipobaini akiwa katika
mwendelezo wa kufanya makosa hayo. Hakimu huyo aliahirisha kesi hiyo kwa ajili ya kutajwa hadi Aprili 9, mwaka huu huku Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi.
HALI ILIVYOKUWA
Kabla ya kuanza kwa kesi, idadi kubwa ya wafanyabiashara kutoka
maeneo mbalimbali nchini walikusanyika kwenye eneo la Mahakama,
wakisubiri kuletwa kwa Mwenyekiti wao huku polisi waliovaa sare na
makachero wakiwa wamelizunguka eneo hilo kuimarisha ulinzi. Kabla
mahakama hiyo haijamrejeshea dhamana mshtakiwa huyo, maduka katika
maeneo kadhaa nchini yalikuwa yamefungwa.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, aliwataka wafanyabiashara kufungua
maduka yao wakati serikali ikiendelea kushughulikia tatizo hilo. Alisema tayari kamati imeshaundwa kushughulikia malalamiko yao na kwamba wanapaswa wasubiri badala ya kufunga maduka.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment