Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) mstaafu, Jaji Mark
Bomani, ambaye pia ni mtaalam nguli wa Katiba, ameonya kuwa iwapo
upigaji wa kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa utalazimishwa
kufanyika Aprili 30, mwaka huu, wakati dalili zote zinaonyesha kuwa
haiwezekani, unaweza kuzua mtafaruku mkubwa nchini.
Ili kuepusha hali hiyo, ameshauri kura ya maoni iahirishwe hadi
baadaye, badala yake Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) iendelee na
uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa ajili ya kutumika
katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Pia, amependekeza kuwa Katiba inayotumika sasa ya mwaka 1977
iboreshwe kwa kuingiza ndani yake mambo mbalimbali, akiwamo mgombea
binafsi. Jaji Bomani ambaye ni mtaalam nguli wa Katiba aliyewahi kuandika
katiba za nchi mbalimbali, zikiwamo za Namibia na Burundi, alisema hayo
alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Alisema nia nzuri ya Rais Jakaya Kikwete, ya kuipatia Tanzania
Katiba mpya, iliharibika baada ya kuundwa kwa Bunge Maalum la Katiba
(BMK). Jaji Bomani alisema hilo lilidhihirika baada ya baadhi ya wajumbe wa BMK kujitoa katika Bunge hilo. “Hili lilikuwa doa kubwa sana kwa mchakato wote. Ilikuwa ni mwanzo mbaya,” alisema Jaji Bomani.
Aliongeza: “Kazi yake (BMK) haikuwa nzuri, haikuridhisha, kwani iliwagawa watu.” Alisema licha ya baadhi ya wajumbe wa BMK kubaki kwenye Bunge hilo
na kuendelea na mchakato hadi kutoa Katiba inayopendekezwa, bado anaona
kuna matatizo mawili.
La kwanza, alisema ni kuwapo baadhi ya makundi na watu wanaoamini
kuwa Katiba inayopendekezwa imetupilia mbali baadhi ya mambo
yaliyopendekezwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba yaliyotokana
na maoni ya wananchi, hivyo wanaipinga na baadhi yao wanatishia
kutoipitisha. “Hili ni jambo la kusikitisha, lakini siyo jambo la kupuuza. Katiba
siyo kitu kinachotegemea kura, bali inatakiwa iwe na muafaka. Kitu
hicho Katiba za Namibia na Burundi inacho,” alisema Jaji Bomani.
Alisema katiba ya nchi ndiyo sheria mama na msingi wa kuendesha nchi na kwamba uzuri wake, sharti iungwe mkono na wengi. Alisema Katiba inayopingwa na kundi kubwa la watu, ni chanzo cha mfarakano kwenye nchi. Alisema endapo katiba ya namna hiyo inapigiwa kura nyingi za
`hapana' au inapingwa na upande mmojawapo wa Muungano iwe Zanzibar au
Tanganyika, basi hatima yake ni kuvunja Muungano na kuhoji: “Je, ni sawa
tufike huko?”
La pili, alisema ana wasiwasi mkubwa juu ya uwezekano wa kura hiyo
kupigwa Aprili 30, mwaka huu, kwani hadi kufikia jana uandikishaji wa
wapigakura katika daftari la kudumu la wapigakura ulikuwa ukisuasua. “Naambiwa eti mpaka sasa waliokwishaandikishwa hawazidi hata
milioni moja. Hapo takriban zaidi ya milioni 20 wataandikishwa katika
wiki nne zilizobaki? Nafikiri itakuwa ni muujiza kufanya hivyo,” alisema
Jaji Bomani.
Aliongeza: “Sasa tufanyeje? Tuendelee na kura ya maoni ambayo ni
idadi ndogo ya wapigakura walioandikishwa ndiyo watakaoshiriki, tena kwa
suala zito kama la Katiba? Tukifanya hivyo tutakuwa tumefanya kosa
kubwa sana ambalo litatuletea mgogoro mkubwa na manung’uniko mengi sana
nchini. Hivi kweli tufike hapo?”
“Mapendekezo yangu ni kwamba kura ya maoni juu ya Katiba mpya
iahirishwe mpaka baaadaye. Badala yake Tume ya Uchaguzi iendelee na
uboreshaji wa daftari la wapigakura tayari kwa uchaguzi mkuu Oktoba
2015. Ikiwezekana hata tuachane na mfumo wa BVR (mfumo mpya wa
kielektroniki wa Biometric Voters Registartion), ambao umewapa shida
hata wenzetu Kenya na Nigeria.”
Hata hivyo, alisema kwenye rasimu ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba na Katiba inayopendekezwa, kuna mambo mazuri, hivyo akashauri
yafanyiwe mabadiliko katika iliyopo ili yatumike kwenye uchaguzi wa
Oktoba, mwaka huu. Aliyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na uwakilishi sawa wa
jinsia, mgombea binafsi, mgombea urais kupata asilimia 50 au zaidi ili
ashinde na Tume Huru ya Uchaguzi. “Katiba iliyopo inaweza kufanyiwa mabadiliko haraka haraka, tuseme
kwenye kikao kijacho cha Bunge tayari kwa matumizi ya uchaguzi mkuu
ujao. Litakuwa ni jambo la kusikitisha kuwa hata yale mazuri yasiyo na
ubishi yasitumiwe kwenye uchaguzi huo,” alisema Jaji Bomani.
Aliongeza: “Unahitajika muda zaidi wa mazungumzo. Kwani Watanzania
tunataka nini au Mtanzania wa kawaida anataka nini? Anataka maisha yake
yaboreke, hawataki Muungano wa serikali mbili, tatu wala moja, hivyo ni
vitu vya uongozi, havitakiwi uhasama.”
Alisema kura ya maoni haiwezekani kufanyika Aprili 30, mwaka huu
kwa kuwa maandalizi hayajafanyika ya kutosha, kwani wapigakura kati ya
milioni 20 hadi 23 wanaotarajiwa wanatakiwa wote wapewe nafasi ya kupiga
kura. “Ukiangalia kwenye maandalizi, hatujafika hata nusu. Nina wasiwasi
kama hiyo tarehe 30 itafika wote watakuwa wameandikishwa. Tulipe muda.
Tusijiongeze kitu kitakachoongeza mfarakano,” alisema Jaji Bomani.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment