Mbunge wa Ubungo, John Mnyika akionyesha baadhi ya vipengele
alivyoviongeza wakati wa kupitisha vifungu vya Muswada wa Sheria ya
Bajeti wa Mwaka 2014 bungeni mjini, Dodoma jana.
Wabunge watano
wamelitikisa Bunge tangu mkutano wa 19 wa Bunge ulipoanza kutokana na
michango yao binafsi katika mijadala ya miswada ya sheria mbalimbali
iliyowasilishwa bungeni. Tathmini iliyofanywa na gazeti hili tangu kuanza
kwa vikao hivyo, imeonyesha wabunge hao ndio waliokuwa wakisimama mara
kwamara kuchangia hoja.
Hoja zilizozungumzwa na wabunge hao kwa nyakati
tofauti ziliitikisa Serikali na kusababisha aliyekuwa akikaimu nafasi ya
Waziri Mkuu bungeni, Profesa Mark Mwandosya, kiti cha Spika na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju kusimama kutoa
ufafanuzi.
Waliotikisa
Wabunge waliotikisa Serikali katika michango yao
ni Kangi Lugola (Mwibara - CCM), Tundu Lissu (Singida Mashariki -
Chadema), John Mnyika (Ubungo-Chadema), Chrisowaja Mtinda (Viti
Maalumu-Chadema) na Habib Mnyaa (Mkanyageni-CUF).
Lissu
Machi 20 mwaka huu wakati akichangia muswada wa
Sheria ya Usimamizi wa Maafa, aliibana Serikali huku akitumia dakika 125
kupinga muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa wakati Bunge lilipokaa
kama kamati kupitisha vipengele.
Mara kadhaa Masaju, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), Jenister Mwenyekiti wa Bunge, Mussa
Azzan Zungu walisimama kumwelewesha mbunge huyo, lakini alishikilia
msimamo wake, huku akisema muswada huo una mgongano wa kisheria kuhusu
mamlaka ya kuweka utaratibu wa kutangaza maafa na kutangaza hali ya
hatari, akisema kuwa sheria hiyo imempora Rais madaraka ya kutangaza
maafa na kuyapeleka kwa waziri.
Mnyika
Aliibuka Machi 26 wakati Bunge lilipokaa kama
kamati kupitisha Muswada wa Takwimu wa mwaka 2013, kuibuka na hoja
ambayo lilikuwa halifahamiki kwamba katika muswada huo kuna kipengele
kinachotoa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela na faini isiyopungua
Sh10 milioni kwa mtu au chombo cha habari kitakachofanya makosa ya kutoa
takwimu zisizokuwa sahihi.
Mbunge huyo akihoji sababu za kutobadilishwa kwa
vipengele vya muswada huo vyenye utata kama ambavyo Serikali iliahidi
Novemba mwaka jana baada ya muswada huo kukwama kupitishwa kutokana na
wabunge wengi kupinga vipengele vyenye utata, kikiwamo kipengele hicho.
Mnyaa
Mbunge huyo wa Mkanyageni aliibuka Machi 20 na kutoa hoja ya
kutaka muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Uhamiaji namba 54
wa mwaka 2014, kutojadiliwa bungeni kwa sababu unagusa mambo ya
muungano, ambapo katika hoja yake alisema kama uhamiaji ni eneo la
muungano, iweje muswada huo upitishwe na Bunge hilo bila theluthi mbili
ya wabunge kutoka Zanzibar kama Katiba inavyotamka. Mvutano huo ulisababisha Masaju kufafanua kuwa
kati ya masuala yanayogusa muungano, ambayo yakifanyiwa marekebisho
yanahitaji kupitishwa na theluthi mbili za wabunge wote wa Tanzania Bara
na visiwani, uhamiaji na masuala ya silaha hayamo.
Licha ya ufafanuzi huo, Spika wa Bunge Anne
Makinda aliahirisha kujadiliwa kwa muswada huo pamoja na mingine miwili
ya takwimu na usimamizi wa kodi ili kupata nafasi nzuri ya kupitia
vifungu vya sheria kuona kama jambo hilo ni sahihi ama la.
Lugola
Machi 24 wakati akichangia muswada wa Sheria ya
Udhibiti na Usimamizi wa Dawa za Kulevya, alizua taharuki baada ya
kueleza kuwa amekwama kuwataja vigogo wanaojihusisha na uuzaji wa dawa
hizo kwa kuhofia usalama wake.
Mtinda
Mbunge huyo aliliteka Bunge Machi 23 wakati
akichangia mjadala wa muswada wa Sheria ya Mifumo ya Malipo baada ya
kuzilipua kampuni za simu na benki kuwa zinawaibia Watanzania na hakuna
sheria ya kuzishitaki. Hata hivyo, hoja zake zilijibiwa na Waziri wa
Fedha, Saada Mkuya.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment