Social Icons

Pages

Friday, January 09, 2015

RC: DAWA KUKOMESHA 'PANYA ROAD' INAANDALIWA

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick.
Katika kukabiliana na kikundi cha uhalifu unaofanywa na vijana wanaojiita ‘Panya road’, serikali imetangaza kuanzisha daftari maalumu kwa ajili ya kuorodhesha watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, alisema hayo wakati akizindua awamu ya tatu ya utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (Tasaf) katika Wilaya ya Temeke. Alisema daftari hilo, ambalo litasambazwa katika ngazi zote za mitaa, kata, wilaya hadi mkoa na litakuwa maalumu kwa ajili ya kuwatambua na kuwadhibiti watu wote wanaojihusisha na vitendi vya uhalifu.
Sadiki alisema kwa kutumia mfumo huo itakuwa rahisi kwa vyombo vya dola kubaini majina na mahali wanapoishi na kuwafuatilia kwa karibu kabla hawajafanya jambo baya. Wiki iliyopita kikundi cha vijana kinachojiita ‘Panya Road’ kilizua taharuki kubwa na kusababisha watu kuporwa mali katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo na shughuli mbalimbali kusimama kwa muda.
“Hatutakubali kuvumilia chokochoko zozote zinazoharibu utulivu na amani yetu. Sisi kama serikali tumeamua kuanzia sasa tutaanzisha daftari maalumu, ambalo tutaorodhesha watu wote wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu,” alisema Sadiki.
Aliongeza: “Kwa kutumia daftari, tutamtafuta kila mtu atakayehusika na tukio lolote la kihalifu. Hawatakuwa na mahali pa kujificha kwa kuwa tutakuwa tunajua hadi nyumbani kwake. Kitu muhimu naomba ushirikiano wa wananchi, madiwani na viongozi wa mitaa kuwaorodhesha wale wote wanaotuhumiwa kwenye daftari hili.”
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: