Rais Jakaya Kikwete, amefanya uteuzi wa Mwenyekiti,
Makamu Mwenyekiti na Makamishna wanne wa Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Rais
Kikwete amemteua Bahame Tom Mukirya Nyanduga kuwa Mwenyekiti.
Nyanduga ana Shahada ya kwanza ya Sheria aliyoipata mwaka 1977 kutoka
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Shahada ya Uzamili ya Sheria mwaka 1987
kutoka London, Uingereza.
Alifanya kazi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa wa Kimataifa kwa
miaka 17 na aliwahi kuwa Rais wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea wa
Tanganyika 2001-2009. Kadhalika alikuwa Kamishna wa Umoja wa Afrika wa
Kamisheni ya Haki za Binadamu kuanzia mwaka 2003 hadi 2009.Taarifa hiyo ilieleza kuwa Rais Kikwete pia amemteua Iddi Ramadhani Mapuri kuwa Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo. Ana Shahada ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyoipata mwaka 1984, Diploma ya Uzamili ya Maendeleo Vijijini ya mwaka 1987 na Diploma ya Uzamili ya Menejimenti (India). Alikuwa Kamishna wa Kazi kuanzia mwaka 1989 hadi 2010 na Mkurugenzi wa Utawala na Maendeleo ya Rasilimali Watu katika Wizara ya Vijana, Wanawake na Uwezeshaji tangu mwaka 2011.
Walioteuliwa kuwa makamishna ni Mohamed Khamis Hamadi ambaye ni Wakili wa Serikali Mwandamizi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka. Aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Rufani za Kodi. Pia aliwahi kuwa Mkuu wa Kitengo cha Utafiti, Tume ya Kurekebisha Sheria.
Kamishna mwingine ni Dk. Kevin Mandopi , ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Msaada wa Sheria, Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto na wakili wa kujitegemea tangu 2005. Vile vile, Rais Kikwete amemteua Rehema Msabila Ntimizi kuwa kamishna. Alikuwa Wakili Mkuu wa Serikali 2005-2007; Kaimu Msaidizi Mwandamizi wa Msajili wa Hati, Wizara ya Ardhi 1994-2005. Ni Meneja wa Ulinzi wa Mali Vijijini, Mkurabita tangu tangu 2008.
Yumo pia Salma Ali Hassanmwenye ambaye alikuwa Wakili wa Serikali, 2002-2009, Afisa wa Haki za Binadamu, Wizara ya Katiba na Utawala Bora. Ni Wakili wa Kujitegemea tangu 2011.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment