Social Icons

Pages

Friday, January 09, 2015

MAHANGA: WALIONIZOMEA NI WAHUNI

Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga, amezungumzia kitendo cha kuzomewa alichofanyiwa juzi akisema kilikuwa ni cha kihuni, ambacho kimegubikwa na chuki za kisiasa.
Dk. Mahanga, ambaye pia ni Mbunge wa Segerea (CCM), alikumbwa na masaibu hayo alipokwenda kushuhudia zoezi la kuapishwa kwa wenyeviti na wajumbe wa serikali za mitaa, lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, wa Anatoglou, jijini Dar es Salaam. 
Akizungumza na NIPASHE jana, Dk. Mahanga alisema kitendo hicho hakijamuumiza, kwani aibu ya kuzomewa inawarudia waliomzomea. Alisema hilo ni kwa sababu yeye kama mbunge, alikuwa na haki ya kwenda kushuhudia zoezi hilo kwa kuwa waliokuwa wakiapishwa ni viongozi wa serikali wanaotoka katika mitaa iliyoko jimboni kwake.
Alisema mbali na yeye kuwa ni kiongozi wa serikali, pia ni mkazi wa jimbo hilo, hivyo alikuwa na haki nyingine ya kushiriki kama mwananchi wa kawaida kama ambavyo wengine walishiriki kushuhudia kwa kuwa zoezi hilo lilikuwa linashirikisha umma. “Mimi kama mwananchi wa kawaida na kama Mbunge wa Jimbo la Segerea, nilikwenda kushiriki na kushuhudia viongozi wangu wa mitaa 60 wakiapishwa. Na ni haki yangu kufanya hivyo,” alisisitiza Dk. Mahanga.
Aliongeza: “Mbali na kwamba ni mbunge wa jimbo hilo, tukio hilo lilikuwa  linashirikisha umma, hivyo na mimi nilikuwa na haki ya kushiriki kama mwananchi wa kawaida, mkazi wa Segerea. Hivyo, hawa waliniozomea ni aibu yao wenyewe ya kutokuwa na uelewa kwamba hiyo ilikuwa ni haki yangu. Na hata kama ni upinzani, siyo hivyo.”
Aidha, alikana madai ya kuhusika kupeleka wenyeviti au wajumbe waliodaiwa kwenda katika hafla hiyo ya kuapishwa wakati hawakushinda katika uchaguzi. “Suala la kutangaza au kufahamu washindi, halinihusu. Ni la wakurugenzi. Hivyo sihusiki kwa lolote na hao unaowasema walipelekwa kuapishwa wakati hawakushinda katika uchaguzi,” alisema Dk. Mahanga.
Alikuwa akijibu swali la NIPASHE kwamba kama kuzomewa kwake kulitokana na kuhusishwa kupeleka baadhi ya viongozi waliodaiwa kwenda kuapishwa wakati hawakushinda uchaguzi. Tukio la kuzomewa Dk. Mahanga lilitokea juzi wakati wa zoezi la kuwaapisha wenyeviti wa serikali za mitaa iliyoko katika Wilaya ya Ilala. Mitaa iko katika majimbo ya Ukonga, Segerea na Ilala wilayani humo.
Kabla ya kukumbwa na masaibu hayo, Dk. Mahanga alifika katika ukumbi huo na kuketi. Hata hivyo, dakika chache baadaye, umati wa watu waliokuwa nje ya ukumbi, walianza kulalamika wakitaka atoke nje kwa madai kwamba, zoezi hilo halikuwa likimhusu. Hata hivyo, Dk. Mahanga awali, hakufanya hivyo, lakini alivyoona hali imekuwa mbaya aliondoka.
Katika eneo hilo, kulikuwako na mchanganyiko wa watu, wakiwamo wapambe waliokuwa wakishuhudia zoezi hilo. Zomea zomea hiyo iliyomkuta Dk. Mahanga, ilifanywa na wananchi waliokuwa wamesimama mlangoni katika ukumbi huo. Kutokana na mchanganyiko huo wa watu, haikuwa rahisi kufahamu waliomzomea wanatoka chama gani cha siasa.
Tukio hilo lilianza muda mfupi baada ya kuingia zamu ya kuapishwa wenyeviti na wajumbe wa serikali za mitaa zilizoko katika jimbo analowakilisha baada ya kumalizika kwa viongozi wa majimbo ya Ukonga na Ilala. Wakati akitoka nje kwa ajili ya kuondoka, umati wa watu waliokuwa wamesimama nje ya ukumbi walianza kumzomea, huku wakimuita `mwizi' bila kufafanua alichoiba. Walifanya hivyo hadi Dk. Mahanga alipoondoka katika eneo hilo huku akisindikizwa na askari polisi kupanda kwenye gari lake.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: