Shinikozo la kutaka Rais Jakaya Kikwete kumwajibisha
Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, limeendelea
kushika kasi baada ya viongozi wa vyama vya siasa kueleza kuwa kuendelea
kumuweka kiporo waziri huyo ni sawa na kupuuza azimio la Bunge.
Wakizungumza na kituo cha televisheni cha ITV juzi walisema baada ya
Rais Kikwete kuzungumza na Taifa kupitia wazee wa mkoa wa Dar es Salaam
walitegemea kuwa uamuzi wa kumwajibisha Prof.Muhongo hautachukua muda
mrefu kama ilivyotokea.
“Sasa kiporo hiki kimekuwa kinaenda siku nyingi, kimechacha na
kitachacha zaidi na kitakuwa hakiliki kwa sababu mambo ya msingi ni
Tanesco ambalo ni shirika la umma ambalo kutokana na suala la Escrow
limeibebesha Tanesco mzigo,” alisema Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi
(CUF), Prof. Ibrahimu Lipumba.Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mpinduzi (CCM), Najimu Msenga alisema imani ya CCM ni kwamba Rais Kikwete atafanya maamuzi ya sakata ya uchotwaji fedha katika kaunti ya Tegeta Escrow kwa maslahi ya Taifa kwani suala hilo haliwezi kuathiri uhai wa CCM kwa sababu bado kipo imara.
“Mheshimiwa Rais na yeye kama binadamu lazima na yeye aangalie ukweli upo wapi katika jambo hili, lakini maamuzi yatatoka yaliyokuwa na busara ya ama Muhongo aendelee au asiendelee,” alisema. Msenga alisema Rais Kikwete hana nia ya kupingana na maamuzi ya bunge, ni lazima atatoa maamuzi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willbrod Slaa, alisema viongozi waliojiuzulu na kuenguliwa uteuzi wao kutokana na kashfa ya Tegeta Escrow watuhumiwa wote walipaswa wawe wamefikishwa mahakamani. “Katika suala la watu waliotafuna rasilimali za Taifa na watu wanaosema uongo ndani ya Bunge kama Muhongo na wale wanaoshindwa kusimamia rasilimali za Taifa hatuwezi kubembelezana nao,” alisema.
Naye Katibu Mkuu wa Chama Cha ACT, Samson Mwigamba, alisema Katika mihimili mitatu ulio juu ni Bunge, hivyo Rais alistahili kutekeleza maazimio yaliyotolewa na bunge bila kuwa na kigugumizi. Katika hatua nyingine Prof. Lipumba akizungumza juzi jioni kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Bururuni, jijini Dar es Salaam, alisema Rais Kikwete anapaswa kufanya maamuzi ya haraka ya kumwajibisha Prof. Muhongo ili kuinusuru nchi na sio kuwadanganya Watanzania kuwa amemweka kiporo.
Aliongeza kuwa kukaa kimya kwa Rias Kikwete ni wazi kuwa anashindwa kutoa maamuzi juu ya waziri huyo, huku ikionekana wazi hataweza kuchukua maamuzi yoyote kutokana na kumwonea aibu Prof. Muhongo. Bado mhusika mkuu anaachwa bila kuwajibishwa kwa kisingizio cha kuwekwa kiporo,” alisema.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment