Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta akitoka katika Mahakama ya Wilaya ya
Hai, Mkoa wa Kilimanjaro baada ya kupanda kizimbani na kutoa ushahidi
mahakamani hapo katika kesi ya jaribio la kutapeli viongozi wa Chadema.
Kushoto ni shahidi namba mbili wa kesi hiyo, Profesa Abdalah Safari.
Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta jana
alipanda kizimbani kutoa ushahidi katika Mahakama ya Wilaya ya Hai tukio
lililovuta hisia za wananchi wengi kwani ni la kwanza na la aina yake
kwa kiongozi wa juu wa mhimili huo wa dola. Jaji Samatta aliingia eneo la Mahakama saa 2.40
asubuhi akifuatana na Profesa Abdallah Safari na baadaye kwenda moja kwa
moja chumba cha mapumziko kabla ya kuingia mahakamani.
Baada ya kula kiapo kutoka kwa karani wa Mahakama
hiyo, Baltazar Buretta, Jaji Samatta alianza kutoa ushahidi katika kesi
inayomkabili Adam Abeid (25) ya kujifanya jaji huyo na kutaka kuwatapeli
viongozi wa Chadema, akisema alishtuka alipoelezwa na Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa kuwa kuna mtu ambaye amempigia simu
akijitambusha kuwa ni Jaji Samatta.
Abeid pia anakabiliwa na shtaka kutaka kumtapeli Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi
wa Wilaya ya Hai, Denis Mpelembwa ilisikilizwa chemba huku Jaji Samatta
akiongozwa kutoa ushahidi wake na Mwanasheria wa Takukuru, Susan Kimario
anayesaidiana na Furahini Kibanga akikana kumfahamu wala kuwa na
uhusiano na mshtakiwa huyo.
Jaji Samatta ambaye sasa ni Mkuu wa Chuo Kikuu
Mzumbe na mjumbe wa Bodi ya Kuchuja Mahakimu na Majaji Kenya, alisema
kati ya Aprili na Mei 2012, Dk Slaa alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi
(sms) akiambatanisha na ujumbe unaodaiwa kutumwa na mshtakiwa, akimtaka
athibitishe kama ndiye aliyeutuma kwake. Ujumbe huo ulisomeka: “Hali yako Dk Slaa, kesho
nataka nikamuone Jaji Mkuu Chande, naomba nichangie nauli (ili)
nikashughulikie yale masuala yetu.”
Jaji Samatta alisema alishtuka na kuamua kumpigia
simu Dk Slaa na kumweleza kuwa ujumbe huo haukuwa umetoka kwake na
kumtaka alifikishe suala hilo kwenye vyombo vya dola. “Nilimpigia pia Wakili Profesa Safari (Abdallah)
nikamuomba ahakikishe suala hilo haliishi kisiasa, bali upelelezi
ufanyike kwa sababu hadhi yangu na heshima yangu ilikuwa at stake
(shakani),” alisema.
Maswali kati ya mshtakiwa na Jaji Samatta yalikuwa kama ifuatavyo;
Mshtakiwa: Je, katika zile meseji alizokutumia Dk Slaa unazo kwenye simu yako?
Jaji Samatta: Zile meseji ziko katika simu yangu ya zamani ambayo niliacha kuitumia baada ya kuzeeka.
Mshtakiwa: Wakati Dk Slaa anakupa taarifa hizo, nani alikuwa wa kwanza kulifikisha suala hilo Takukuru?
Jaji Samatta: Sijui kwa sababu niliwaambia Dk Slaa
na Profesa Safari walipeleke hilo suala kwenye vyombo vya dola na mimi
ningeitwa kuandika maelezo.
Profesa Safari ambaye ni shahidi wa pili,
aliiambia Mahakama kuwa kati ya Aprili na Mei, 2012, alipokea simu
kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni Jaji Samatta akiomba simu ya
Lema. “Aliniambia anataka azungumze na Lema ili
kumsaidia kwenye kesi yake ya Arusha (ya kupinga ubunge wake). Nilimpa
na nikampigia pia Lema kuwa kuna mtu anamtafuta,” alisema.
Profesa Safari alisema hata hivyo, alishuku kuwa
mtu huyo hakuwa Jaji Samatta kutokana na kwamba alikuwa akiifahamu sauti
yake na ni mtu ambaye wamefanya naye kazi kwa muda mrefu. Baadaye Profesa Safari alisema aliamua kumjulisha
Dk Slaa kuhusiana na jambo hilo kwa vile lilikuwa linaonekana kuwa na
sura ya utapeli na rushwa na Chadema hakijihusishi na mambo hayo. Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka unadai kuwa
mshtakiwa alijifanya ni Jaji Samatta akitaka kumsaidia Lema katika rufaa
yake namba 47/2012 ya kupinga hukumu iliyokuwa imemvua ubunge wa Arusha
Mjini.
Pia, upande wa mashtaka unadai pia katika kipindi
hicho, mshtakiwa huyo ambaye alikana mashtaka hayo, alijifanya kuwa ni
mkuu wa Takukuru Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, Abel Kibaso.Kesi hiyo
imeahirishwa mpaka Januari 14.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment