Social Icons

Pages

Friday, January 09, 2015

DK. MENGI AZINDUA SHINDANO LA BIASHARA LA MILIONI 60/-

Katika kuendeleza jitihada zake za kuwahamasisha Watanzania kujiamini kwa kutumia nguvu na maarifa kwamba wanaweza kujikwamua dhidi ya umaskini kwa kubuni na kuendesha wao wenyewe miradi ya ujasiriamali, Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, amezindua tena shindano la kubuni wazo la biashara huku Sh. milioni 60 zikitarajiwa kushindaniwa.
Shindano hilo linalojulikana kama 3N likiwa na maana ya ‘Nitabuni wazo la biashara, Nitatekeleza na Nitafanikiwa’ litakuwa likifanyika kila mwezi kwa miezi sita tangu Januari Mosi hadi Juni 30, 2015  huku mshindi wa kila mwezi akijishindia ruzuku ya Sh. milioni 10 ambazo atazitumia kutekeleza kwa vitendo wazo lake la biashara.
Shindano hilo litashirikisha Watanzania pekee na kuendeshwa kwa njia ya mtandao wa kompyuta huku mshiriki akitakiwa kutuma wazo lake kwa anuani ya twita @regmengi Shindano la Wazo la Biashara.
Katika mchujo wa kwanza, jopo la wataalamu litapitia mawazo 10 bora zaidi na waliotoa mawazo hayo watakuwa wakifanyiwa usaili kwa njia ya simu. Hata hivyo, katika mawazo hayo 10, moja litachaguliwa kuwa mshindi.
Akizungumza katika uzinduzi, Dk. Mengi alisema shindano hilo linalenga kuhimiza watu kuwa na upeo mkubwa wa kuona fursa za kibiashara na kuzitumia kujikwamua kiuchumi. Alisema shindano hilo ni mchango wake binafsi wa kuunga mkono jitihada za serikali na sekta binafsi za kuwakomboa wananchi kiuchumi kwa njia ya ujasiriamali kwa kuwa sera zote za elimu ya juu na ile ya maendeleo ya viwanda vya kati na vidogo zinachochea na kuendeleza ujasiriamali wa mtu mmoja mmoja.
“Kwa muda mrefu nimekuwa nikishawishi uwapo wa moyo wa ujasiriamali miongoni mwa Watanzania hasa vijana. Ni ndoto yangu kuona uchumi wetu unakua kwa kasi kiasi cha kuzalisha zaidi ya mamilionea 100 kila mwaka wanaoendesha biashara halali. Kuwa na wazo sahihi la biashara katika muda mwafaka na eneo sahihi ni muhimu zaidi kuliko ruzuku ya fedha,” alisema.
“Nataka vijana watambue kwamba wanaweza kuanza na kitu kidogo na kukua kufikia kampuni kubwa kabisa ya kimataifa unayoweza kufikiria. Naamini siku moja mazingira ya ujasiriamali nchini yatakuwa miongoni mwa mazingira bora kabisa barani Afrika.”
Alisema shindano hilo lipo wazi kwa Watanzania wote na wanachotakiwa kukifanya ni kuhakikisha wanapeleka wazo lao la biashara kwa Dk Mengi  kupitia mtandao wa kompyuta kwa kumtag Dk Mengi kupitia mtandao wa kompyuta wa twita kwenye  @regmengi.
Aliongeza kuwa ni wale tu watakaomtag ndiyo watakaofikiriwa na jopo la wataalamu na kwamba maamuzi ya jopo la wataalamu yatakuwa ya mwisho huku washindi wa kila mwezi wakiarifiwa kwa kutumiwa ujumbe mfupi kupitia akaunti zao za twita (DM) na kupewa ruzuku yao.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: