Bango likionyesha bei mpya za mafuta ya petrol na dizeli katika moja ya
kituo jijini Dar es Salaam jana, baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati
na Maji (Ewura) katangaza shusha gei za mafuta, juzi.
Wakati mjadala
wa bei ya mafuta ukiendelea, imebainika kuwa bei ya nishati hiyo nchini
ni kubwa kulinganisha na Kenya, wakati Rwanda ikiongoza kwa kutonufaika
kwa kushuka kwa petroli katika soko la dunia kati ya nchi za Afrika
Mashariki. Mafuta yameporomoka bei katika soko la dunia kutoka Dola 115 za Marekani hadi chini ya Dola 50 kwa pipa tangu Juni 2014.
Takwimu ambazo Mwananchi ilizipata jana kutoka
nchi hizo tano zinaonyesha kuwa wizara zote zinazoshughulikia mafuta,
isipokuwa Uganda, zimepunguza bei kwa viwango tofauti. Wakati Rwanda, Burundi na Uganda hazina bandari,
Kenya na Tanzania zinapakana na Bahari ya Hindi na hivyo kutoathiriwa
sana na gharama za usafirishaji.
Lakini petroli nchini Kenya ilipungua bei tangu
Desemba 15 na kuuzwa kwa Sh1,719.7, wakati bei iliyoanza kutumika jana
nchini ni Sh1,955. Kwa mujibu wa taarifa hizo, Tume ya Mamlaka ya
Udhibiti wa Nishati ya Kenya (ECR) ilitangaza bei mpya elekezi za mafuta
tangu Desemba 15, 2014 na kwamba zitaendelea hadi Januari 14, 2015.
ECR ilipunguza bei ya petroli kwa Sh90.6, dizeli kwa Sh68.1 na mafuta ya taa kwa Sh93.5 kwa lita. Punguzo hilo limefanya mafuta ya dizeli Kenya yauzwe Sh 1,719.7, petroli Sh1, 931 na mafuta ya taa Sh1, 351. Mbali ya kuwa nchi hizo mbili kuwa karibu na
bandari inayopunguza gharama za usafirishaji na mfumo wa asilimia 40 ya
makato yasiyobadilika, bado bei za Kenya ni nafuu. Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Biashara na
Viwanda ya Rwanda, nchi ambayo iko zaidi ya kilomita 1,000 kutoka
bandari ya Dar es salaam, inaeleza kuwa bei ya petroli na dizeli
imeshuka kuanzia jana na kwamba hairuhusiwi kuuzwa zaidi ya Sh2,409.6
kwa lita moja. Kabla ya punguzo hilo, yalikuwa yakiuzwa kwa Sh2, 535.
Pia, takwimu zinaonyesha kuwa bei ya mafuta
Uganda, ambayo iko karibu kilomita 1,000 kutoka Mombasa, pia imebaki
kuwa juu kwa Sh2,250 na hivyo kuifanya nchi hiyo kushika nafasi ya pili
Afrika Mashariki. Petroli inauzwa kwa Sh2, 250; dizeli Sh1, 920 na
mafuta ya taa kwa Sh1, 710, bei iliyokuwapo kabla ya marekebisho ya bei
kwenye soko la dunia. Nchini Burundi, dizeli na petroli zinauzwa kwa Sh2, 237.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment