Social Icons

Pages

Thursday, December 18, 2014

WABUNGE AFRIKA MASHARIKI WAMNG'OA SPIKA

Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) jana walifanikiwa kung’oa Spika wa Bunge hilo, Dk. Margret Zziwa kwa kile kilichoelezwa kwamba kiongozi huyo amepoteza sifa za kuendelea kushikilia wadhifa huo.
Hatua hiyo ilikuja baada ya wabunge hao kukubaliana na mapendekezo ya kamati ya Sheria, kanuni na madaraka ya bunge ambayo yalionyesha kwamba Dk. Zziwa hana tena sifa za kuendelea kushikiria wadhifa huo. Katika kikao chao kilichofanyika kwenye Makao Makuu ya  Jumuiya ya Afrika Mashariki, wabunge 39 kutoka nchi tano wanachama waliohudhuria kikao hicho ambapo kura 36 zilimkataa Zziwa kuwa Spika , Mbili zikimkataa na moja ikiharibika.
Mapema mwaka huu, Mbunge Peter Mathuki  kutoka Kenya, aliibua hoja ya kung’oa  Spika Zziwa hatua ambayo iliibua mvutano miongoni mwa wabunge waliokuwa wakimtetea Spika Zziwa na waliotaka ang’oke. Mwenyekiti wa kamati uchunguzi dhidi ya Spika Zziwa, Frederic Ngenzebuhoro kutoka Burundi alisema madai yote dhidi ya kiongozi huyo yamethibitika kuwa kweli na kuomba bunge lipitishe azimio la kumng’oa madarakani.
“Baada ya kuchunguza, kufanya mahojiano na kukusanya nyaraka mbalimbali zikiwemo barua za Spika Zziwa mwenyewe, picha za mgando na video, kamati inapendekeza aondolewe madarakani mara moja kwa kushindwa kutimiza wajibu na matumizi mabaya ya madaraka,” alisema Ngenzebuhoro. Pamoja na madai mengine, Spika Zziwa anadaiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kuwaingiza baadhi ya ndugu zake akiwemo mumewe kwenye shughuli za Eala wakati siyo wabunge wala watumishi wa bunge hilo.
Nafasi ya Zziwa inatarajiwa kupiganiwa tena na wabunge kutoka Uganda kutokana na ukweli kwamba nafasi hiyo bado inashikiliwa na nchi hiyo kwa muujibu wa taratibu za uendeshaji wa bunge hilo. Katibu wa bunge hilo anawajibu wa kuitisha uchaguzi huo mapema iwezekanavyo kuziba nafasi hiyo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: