Wakati homa ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na
madiwani utakaofanyika mwakani ikianza kupanda nchini, idadi ya makada
wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanaowania nafasi ya kuteuliwa na chama
hicho kugombea urais inazidi kupanda, baada ya Waziri wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu, kutangaza kuwa atachukua fomu ya kuwania nafasi
hiyo.
Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, walitangaza nia hiyo wakiwa ziarani nchini Uingereza na kwa upande wa Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalah jijini Dar es Salaam. Nyalandu alitangaza nia hiyo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika jimboni kwake katika uwanja wa Ilongero.
Mkutano huo uliitishwa na Nyalandu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM) kwa lengo la kuwashukuru wapiga kura wake kumchagua kushika wadhifa huo kwa vipindi vitatu mfululizo tangu mwaka 2000. Nyalandu alisema chama chake kitakaporuhusu wanachama wake kuchukua fomu za kusimamishwa na CCM kugombea urais, atajitokeza kwani wakati sasa umefika wa yeye kuwania nafasi hiyo nchini ili aweze kuwatumikia wananchi. “Katika safari yetu ya miaka 15, Mungu ametusaidia na sasa tunasonga mbele, safari moja huanzisha nyingine. Mwaka 2015, sisi vijana ndani ya CCM tunaamini utakuwa ni mwaka wa kuchukua wajibu wa kuisimamia nchi yetu”.
“CCM mwakani tutaanza kura za maoni kwa ngazi za urais, ubunge na udiwani. Chama chetu kina taratibu na kanuni. Tunajiandaa kuwashangaza Chadema, CUF na Ukawa kwa ujumla. Kwamba tutashindanishwa miongoni mwetu ili apatikane wa kumrithi Rais Kikwete. “Kipenga kikipigwa wakati huo ukifika…Lazaro Nyalandu, mbunge wenu wa miaka 15, nitaelekea Dodoma nikiwa na wananchi makumi kwa maelfu kutoka mikoa yote ili kuchukua fomu ya kugombea urais wa Tanzania,” alisema Nyalandu na kushangiliwa na wananchi wake.
Katika mkutano huo Nyalandu aliongozana na familia yake, mkewe Faraja Kota na watoto wake wake wawili, Christopher na Sera, wazazi, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Queen Mlonzi na viongozi wengine wa CCM. Alisema anaitazama siku hiyo kama ya kuwashangaza watu na Dunia kwamba vijiji vidogo kama Ilongero vinaweza kuwa sehemu ya historia ya Tanzania. Aliwataka wanasiasa wenzake ndani ya CCM wenye nia ya kuwania urais kwenda kwa wananchi ili wapimwe kwa kazi zao na kushindanishwa kisha baadaye apatikane mgombea mmoja wa kupeperusha bendera ya chama.
Nyalandu alitamba kuwa kwa kipindi chote cha miaka 15, wakazi wa Singida Kaskazini wamekuwa wakimchagua kwa kura nyingi kuliko wabunge wote, na kuitaja Ilongero kama kituo cha ushindi wake kisiasa. “Kutokana na utendaji wangu hapa nimekuwa nikiitwa kwa Kinyatulu “Mwanyengu senasena Mwanyengu” na kwamba mafanikio ya kimapinduzi waliyoyapata ni ishara ya umoja wetu ambao naamini utakuwa umoja wa kitaifa,”alisema.
Alimshukuru Rais Kikwete kwa kupewa macho ya kuona mbali na hivyo kumwona mwaka 2010 kwa kumteua kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara kisha Maliasili na Utalii na baadaye mwanzoni mwa mwaka huu, kufanya waziri kamili wa wizara hiyo. Chini ya kauli mbiu yake ya “Pamoja Daima Tutashinda, Nyalandu aliwasihi wapiga kura wake kuwa na utaratibu wa kuwa na Bunge la familia ili wajadiliane mambo kwa pamoja, huku akisisitiza kwamba wananwake wana mchango mkubwa sana hivyo hawapaswi kuachwa mbali.
Mapema kabla ya mkutano huo, Nyalandu aliungana na waumini wa makanisa ya KKKT Dayosisi ya Kati, Usharika wa Ilongero na la Kipentekoste la K.P.C.F katika misa na kuchangia Sh. milioni 10 kwa kila kanisa kwa ajili ya ujenzi na baadaye alitembelea Msikiti wa Ijumaa Ilongero na kuchangia kiasi kama hicho kwa ajili ya ujenzi wa madarasa. Akisoma taarifa ya utekelezaji wa jimbo, Katibu wa CCM Wilaya ya Singida Vijijini, Mwamvua Quilo, alisema tangu mwaka 2000 hadi sasa, Nyalandu ametumia Sh. bilioni 2.3 katika miradi ya maendeleo ya maji, elimu, afya na mambo mengine.
Alisema katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliomalizika karibuni, CCM ilipata ushindi wa asilimia 91.9 katika jimbo hilo na kupoteza vijiji vinane baada ya Chadema na CUF kubuika na ushindi. Hata hivyo alisisitiza kuwa ni uongo kwamba Nyalandu ndiye alichangia wanyang’anywe viti hivyo na vyama hivyo vya upinzani.
“Kampeni tumefanya viongozi wote wa CCM wilaya tulishiriki na kupata ushindi huo mkubwa, hivyo hao wapinzani wa Nyalandu kisiasa wanaozunguka kupotosha alisababisha tukapoteza vijiji vinane siyo wakweli…mbona kwenye majimbo mengine tumepoteza viti vingi sana lakini hawasemi,” alisema Quilo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment