Nassari akiwa amebebwa na wafuasi wa Chadema
Mamia ya wakazi wa Jimbo
la Arumeru Mashariki, jana walifurika katika Mahakama ya Mwanzo ya Maji
ya Chai kusikiliza kesi inayomkabili Mbunge wa jimbo hilo, Joshua
Nassari ya kuchoma bendera ya CCM yenye thamani ya Sh250,000.
Nassari alifikishwa katika mahakama hiyo saa tano
asubuhi akitokea rumande ya Kituo cha Polisi Usa River ambako alilala
baada ya kukamatwa juzi jioni. Mbunge huyo alipandishwa kizimbani na kusomewa
mashtaka mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, David Mwita kuwa alichana na
kuichoma bendera hiyo juzi saa 11 jioni katika eneo la Maji ya Chai. Ilielezwa kuwa mbunge huyo akijua anavunja sheria,
kifungu cha 326 cha makosa ya jinai, alichoma bendera hiyo mali ya
Raphael Moses. Mbunge huyo kwa tiketi ya Chadema alikana mashtaka hayo na aliachiwa kwa dhamana hadi Desemba 24. Wakati kesi hiyo ikiendelea, mawakili watatu
walifika kumtetea lakini hawakupewa nafasi ya kuzungumza kutokana na
mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kutumia mawakili.
Nje ya Mahakama
Baada ya Nassari kutoka nje akiwa ameambata na
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alibebwa juujuu na
wafuasi wa chama hicho huku wakiimba Mandela! Mandela! Mandela!
Akizungumza na wafuasi hao, alisema kesi hiyo ni
ya kisiasa na inatokana na hasira za Serikali ya CCM kushindwa vibaya
katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika jimbo hilo.
Wafuasi CUF mbaroni
Wafuasi wanne wa CUF katika Mamlaka ya mji mdogo
wa Utete, Rufiji, wamekamatwa na polisi kwa tuhuma za kuvunja vioo
katika jengo la ofisi ya CCM Wilaya ya Rufiji na ofisi mbalimbali za
Serikali wakidai wamehujumiwa katika uchaguzi huo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei
aliwataja wanaoshikiliwa na polisi kuwa ni Issa Ngosho, Jumanne Ngosho
na mtu mmoja aliyetajwa kwa jina moja la Rwambo na mkewe ambao
walikamatwa juzi jioni majumbani mwao.
Nyumba ya mgombea yateketezwa
Watu wasiojulikana wameteketeza nyumba ya mgombea
uenyekiti wa Kitongoji cha Lemkuna, Kata ya Ngorika, wilayani Simanjiro,
Hamis Mwanakoga (CCM) wakati wa upigaji wa kura za marudio juzi. Uchaguzi huo ulishindwa kufanyika Desemba 14 baada
ya baadhi ya vijana kuwapiga wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi huo,
kisha kupora masanduku matatu ya kupitia kura na kutoweka nayo. Katika uchaguzi huo wa marudio, Mwanakoga, alishinda kura 27 dhidi ya 19 za mgombea wa Chadema, Stephano Magay. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Deusdedit Nsimeki alisema watu wawili wanashikiliwa kwa tuhuma hizo.
Vurugu Songea
Wafuasi wa Chadema wilayani Songea wanadaiwa
kufanya fujo na kuchoma ofisi ya Kijiji cha Nakawale baada ya msimamizi
wa uchaguzi kubatilisha ushindi wa mgombea wao na kumtangaza wa CCM. Wafuasi hao walifika hatua hiyo baada ya msimamizi
kumtangaza mgombea wa Chadema, Juma Chanduko kuwa ndiye mshindi na siku
iliyofuata akamtangaza mgombea wa CCM, Thabiti Mussa kuwa mshindi. Hali hiyo iliamsha hasira kwa wafuasi hao ambao
waliamua kuchoma moto ofisi hizo za Serikali na kumjeruhi Ofisa Mtendaji
wa Kijiji hicho, Rajabu Issa kwa jiwe kwenye mguu wa kushoto. Katika tukio hilo askari wa kikosi cha kutuliza
ghasia (FFU) G 9771 PC Abdallah alijeruhiwa vibaya kwa kupigwa na kitu
kizito kwenye paji la uso na amelazwa katika hospitali ya mkoa. Kamanda wa Molisi wa Mkoa wa Ruvuma, Mihayo
Msikhela alisema polisi wanaendelea kuchunguza ili kubaini ukweli wa
tukio hilo la Desemba 15.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment