Social Icons

Pages

Thursday, December 18, 2014

LHRC YALAANI VURUGU CHAGUZI ZA MITAA

Hellen Kijo Bisimba, Mkurugenzi Mtendaji LHRC.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani vikali vurugu zilizotokea na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali  katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Ezekiel Masanja, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari na kufafanua kuwa taarifa zao zinaonyesha kuwa vurugu nyingi zilitokea kutokana na udhaifu wa usimamizi, kuwapo kwa maandalizi hafifu na ya kubabaisha  ambayo ndiyo yaliyoibua hasira kwa wananchi na kusababisha vurugu hizo.
Aidha, alisema ni dhahiri kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imeshindwa kuandaa na kusimamia vyema uchaguzi  huo na kusababisha usumbufu mkubwa na ukiukwaji haki ya kikatiba ya wananchi kupiga kura.  “Kama vituo vingefunguliwa kwa wakati, majina ya wapiga kura yangekuwapo tayari na pia uratibu wa zoezi zima ungefanyika kama inavyotakiwa kisheria kwa kiasi kikubwa tungepunguza vurugu nyingi zilizojitokeza,” alisema Masanja.
Aliongeza kuwa LHRC kinatoa wito kwa kwa Waziri mwenye dhamana kuwajibika mara moja na wote waliohusika kuzembea na kuharibu uchaguzi huu wawajibishwe. Aliyataja maeneo yaliyokumbwa na vurugu na uvunjifu wa amani mara baada ya matokeo kutangazwa  kuwa ni Kimara na  Kawe kwa mkoa wa Dar es Salaam, Ilemela kwa mkoa wa Mwanza na Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa.
Pia waangalizi walishuhudia tukio la ukiukwaji wa haki ya kuishi kwa kijana mmoja huko Nzega aliyeripotiwa kuwa alipigwa risasi kwa bahati mbaya katika harakati za kusubiri matokeo baada ya kuzuka kwa vurugu na polisi kuingilia kati kwa kuwatawanya wananchi kwa kutumia risasi za moto.
Alizitaja dosari nyingine kuwa ni ushiriki mdogo wa wananchi katika kampeni uliosababishwa na mkanganyiko wa tarehe ya kampeni, uelewa mdogo wa umhimu wa kushiriki katika uchaguzi, kampeni nyingi kumalizika baada ya saa 11 jioni na wanachama kupita mitaani wakiimba na kupiga tarumbeta kuhamasisha wananchi kuwapigia kura wagombea wao.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: