Mama akikamua maziwa kwa ng'ombe
Biashara ya maziwa ni muhimu kwa kukuza uchumi
na kuimarisha afya. Licha ya ukweli huu hapa nchini bado biashara ya
maziwa na lishe haijapewa umuhimu ukilinganisha na nchi nyingine.
Tanzania inashika nafasi ya pili katika bara la
Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya ng’ombe ambayo ni zaidi ya milioni
21.3. Nchi ya kwanza kwa idadi ya ng’ombe barani Afrika ni Sudan. Pamoja
na ukweli huo Tanzania haijapata mafanikio makubwa kiuchumi kutokana na
kutowekeza kikamilifu katika biashara ya maziwa. Takwimu kutoka Bodi ya Maziwa zinaonyesha kuwa
wastani wa unywaji wa maziwa kwa mtu mmoja hadi sasa umefikia lita 43
kwa mwaka ingawa Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza wastani wa
lita 200 kila mwaka kwa kila mtu. Utafiti uliofanywa katika mikoa ya Mbeya, Rukwa,
Ruvuma na Iringa unaonyesha kuwa sehemu kubwa ya wakazi wa mikoa hiyo ni
wafugaji, lakini mifugo haiwanufaishi kiuchumi. Kwa mfano mkoani Ruvuma
mtu anakunywa lita 11.6 tu za maziwa kwa mwaka ukilinganisha na viwango
vya kitaifa na kimataifa vya unywaji maziwa kwa mwaka.
Kwa sasa uzalishaji wa maziwa nchini ni lita
bilioni mbili kwa mwaka, lakini kiasi hicho siyo cha kujivunia kwa
sababu sehemu kubwa ya uzalishaji upo katika mfumo wa kienyeji hivyo
maziwa yanayozalishwa hayakidhi viwango vya kimataifa ukilinganisha na
nchi jirani ya Kenya ambayo soko lake ni la nje. Takwimu kutoka Bodi ya maziwa nchini Kenya
zinaonyesha kuwa uzalishaji wa maziwa kwa mwaka katika nchi hiyo ambayo
haina idadi kubwa ya mifugo ukilinganisha na Tanzania, ni lita bilioni
2.4 na unywaji wa maziwa kwa mtu kwa mwaka ni wastani wa lita 57.
Kwenye maziwa kunapatikana bidhaa nyingi kama vile
maziwa freshi, mtindi, samli, siagi na jibini za aina mbalimbali kama
mozzarella, gouda, cheeda. Utafiti unaonyesha kuwa Watanzania hawana
utamaduni wa kunywa maziwa, wakati Kenya inaongoza kwa nchi za Afrika
mashariki Kenya ndio wanaoongoza kwa wananchi wake kunywa maziwa kwa
wingi ikifuatiwa na Uganda na Rwanda. Moja ya kampuni ambazo zinafanya vizuri katika
biashara ya maziwa nchini Kenya ni Brookside Dairy Ltd ambayo inauza
maziwa katika nchi mbalimbali, zikiwemo Tanzania, Uganda, Sudan kusini,
Rwanda, Burundi, Kongo DRC, Ethiopia, Mauritius, Seychelles na Syria.
Meneja masoko wa kampuni hiyo, Peter Wasonga
anasema kila mwaka Brookside inakuza uchumi na kuongeza soko kupitia
biashara ya maziwa na mwaka huu imetumia Sh540 milioni kudhamini michezo
ya shule za sekondari kwa nchi za Afrika mashariki na kati iliyofanyika
Tanzania, ikishirikisha wanamichezo zaidi ya 7,000 ambao walikuwa
wanauziwa bidhaa mbalimbali zinazotokana na maziwa. “Tunazalisha maziwa yenye ubora wa kimataifa.
Uzalishaji kwa siku ni zaidi ya lita milioni moja. Tumefungua depot ya
maziwa Kampala Uganda, Dar es salaam, Arusha, Dodoma na Mwanza nchini
Tanzania kwa lengo la kusambaza maziwa ulimwenguni kote,’’ anasisitiza
Wasonga.
Anabainisha kuwa kampuni ya Brookside imekuwa
inatoa mafunzo ya ufugaji bora kwa wakulima wa Afrika Mashariki ili
kuhakikisha kuwa maziwa yanayozalishwa yanakuwa na ubora wa kimataifa. “Nawashauri watu wa Afrika Mashariki na Kati, hasa
wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 50 ambao kutokana na umri wao
wameanza kupoteza virutubisho muhimu vinavyosababisha magonjwa ya
mifupa, kujenga utamaduni wa kunywa maziwa kwa kuwa maziwa yana
virutubisho vyote muhimu kwa afya,’’ alisisitiza.
Moja ya sababu ambazo zinatajwa kusababisha Watanzania
kutokunywa maziwa, ni hali ngumu ya kiuchumi katika ngazi za kifamilia.
Hali hii inasababisha afya za wananchi kuwa hatarini kutokana na kukosa
virutubisho muhimu vilivyopo katika maziwa. Inadaiwa Watanzania hawanywi maziwa kwa kiwango
kinachotakiwa kimataifa sio kwa sababu hawana elimu ya umuhimu wa lishe
hiyo bali ni umaskini ndiyo unasababisha kuishi chini ya Dola moja kwa
siku, kuona kuwa kwamba wanaostahili kunywa maziwa ni watu wenye uwezo
wa kipato tu .
Utafiti unaonyesha kuwa kiwango cha uzalishaji
maziwa nchini ni kidogo ukilinganisha na mahitaji ya soko la bidhaa
hiyo. Kutofikiwa kiwango cha uzalishaji ni matokeo ya uhaba wa
wataalamu, tathimini inaonyesha kuwa idadi ndogo ya viwanda vya maziwa ,
upungufu wa watumishi na uhaba wa bidhaa za maziwa sokoni unachochewa
na tatizo hilo. Takwimu za mwaka 2013 zinaonyesha kuwa Tanzania
ina zaidi ya ng’ombe milioni 24.3, kati yao asilimia 90 ndiyo wanaotoa
maziwa kwa kiwango kidogo sana. Licha ya kuwa na ng’ombe wengi, Tanzania
inazalisha kiasi cha tani 100,000 za maziwa kwa siku ukilinganisha na
Kenya inayozalisha tani 1,000,000 za maziwa kwa siku.
Takwimu zinaonyesha kiwango cha Tanzania cha
ukuaji wa sekta ya maziwa ni asilimia 3.4 ambacho kinachangia asilimia
3.8 tu katika pato la ndani (GDP) hali hiyo ni matokeo ya uwekezaji
mdogo katika sekta ya mifugo.Kwa sasa inakadiriwa kuwa kiasi
kinachowekezwa na serikali katika sekta ya maziwa ni 30%. Waziri mkuu Mizengo Pinda katika hotuba yake hivi
karibuni alipokuwa akizungumzia uboresha upatikanaji wa maziwa nchini,
alisema Serikali imeongeza uzalishaji mitamba katika mashamba yake
kutoka mitamba 943 kwa mwaka 2012/2013 hadi mitamba 1,046 mwaka
2013/2014 na kusambaza Mbuzi wa maziwa 9,530.
Kwa mujibu wa Pinda, mpango wa Kopa Mbuzi Lipa
Mbuzi umesaidia wafugaji kuongeza tija na hivyo kuchangia ongezeko la
uzalishaji wa maziwa kutoka lita bilioni 1.9 mwaka 2012/2013 hadi lita
bilioni 2 mwaka 2013/2014. Utafiti unaonyesha kuwa Tanzania na nchi
nyingine zinazoendelea zinakabiliwa na tatizo la utapiamlo kwa sababu
mataifa hayo hayana mazoea ya ulaji wa vyakula vyenye protini kama vile
unywaji wa maziwa. Upungufu wa vyakula vya protini unachangia taifa
kupoteza nguvu kazi kwa sababu wananchi wengi wanakuwa na afya duni.
Ripoti wa mwaka 2003 iliyotolewa na Shirika la
Afya Ulimwenguni (WHO) unaonyesha kuwa asilimia tatu ya watoto chini ya
miaka mitano hapa nchini wana utapiamlo mkali.Kutokana na hali hiyo WHO
inashauri uwekezaji katika maendeleo ya sekta ya maziwa utiliwe mkazo
ili kuwawezesha wafugaji kuboresha uzalishaji maziwa nchini.
Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) imeundwa na kupewa
uwezo wa kufanya kazi na Sheria ya Maziwa Sura ya 262 ya Mwaka 2004.
Kazi kuu za Bodi ya Maziwa Tanzania ni kuendeleza sekta ya maziwa,
pamoja na uhamasishaji na ushawishi wa wadau wa sekta ya Maziwa. Kwa mujibu wa wataalamu wa lishe, umuhimu wa
maziwa mwilini unatokana na utafiti kubaini kuwa kati ya vyakula vyote,
ni maziwa na asali pekee ambavyo vinaweza kujitegemea kama mlo kamili. Kulingana na wataalamu maziwa ni mchanganyiko wa
protini, sukari na madini kama kalisiamu na fosiforasi. Maziwa ni muhimu
katika milo ya watoto na watu wazima.Kihalisi kazi ya maziwa ni kujenga
mwili na kutoa kinga dhidi ya maradhi hasa kwa watoto na watu wa rika
zote.
Maziwa ni chanzo cha uhakika cha madini ya
kalisiamu ambayo husaidia kuimarisha mifupa na meno ya mtoto au mtu
mzima na Kwenye maziwa kuna vitamini ambazo husaidia kuimarisha kinga ya
mwili na kusaidia katika matumizi ya virutubisho. Ni changamoto kwa Bodi ya Maziwa nchini kuhamasisha uzalishaji,
ukusanyaji wa maziwa, usindikaji na kuboresha masoko na unywaji wa
maziwa na bidhaa zake kwa kuwawezesha wadau katika shughuli zao kama
ilivyo katika nchi jirani ya Kenya. Bodi ya maziwa nchini inatakiwa kuhamasisha
wananchi kuongeza ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ili kukidhi mahitaji ya
vituo vya ukusanyaji na usindikaji wa maziwa na hatimaye kuondoa
umasikini kwa kuboresha kipato na kuongeza lishe.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment