Social Icons

Pages

Monday, December 29, 2014

ASKOFU: SERIKALI ITUMIE FEDHA ZAKE KUSAIDIA WATOTO JAMII

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi.
Serikali imetakiwa kutunza fedha zake na kutumia kwa manufaa ya jamii ikiwamo kuwasaidia watoto waishio katika mazingira magumu na  yatima badala ya kuziacha zikiliwa na vigogo wachache kama ilivyotokea kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Akizungumza na waumini pamoja na watoto waishio katika mazingira magumu katika ibada maalum ya Boxing Day na kutoa zawadi kwa watoto waishio katika mazingira magumu mkoani Njombe, Askofu wa Dayosisi ya Kusini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Njombe, Isaya Mengele, alisema kuwa serikali iweke udhibiti mzuri wa fedha zake na kuhakikisha haziibiwi na kutumiwa na watu wachache. Alisema kukiwapo na udhibiti mzuri wa mali za serikali hakutakuwapo na wezi kama wa akaunti ya Tegeta Escrow na fedha hizo zitatumika vizuri na kubaki kwa ajili ya watoto waishio katika mazingira magumu na wa mitaani. Alisema  kuwa fedha zilizoibiwa ni nyingi sana na nchi haikupaswa kuwa na watoto wanaolala katika majalala na kula matunda yaliyo tupwa katika mapipa ambayo hayafai kwa kuliwa, hivyo fedha hizo zingempendeza Mungu kama zingetumiwa na watoto hao ikiwamo kuwapatia elimu na chakula.
Askofu Mengele aliwageukia wala rushwa na mafisadi wakiwamo wa Escrow na kuwataka kuachana na tabia hizo badala yake kuwaangalia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na yatima kwa kuwasaidia.
Kanisa hilo lilifungua zawadi za Boxing Day na kuwagawia watoto 123 waishio katika mazingira magunu na yatima. Zawadi hizo ni sweta na vyakula zikiwa na thamani ya zaidi ya Sh. milioni 3.6.
Mgeni rasmi katika ibada hiyo alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi na kuhudhuriwa na watoto wa mitaani 14 na watoto 105. Dk. Nchimbi alisema kuwa watoto hao wanahitaji msaada mkubwa kutoka kwa jamii ili kuondokana na maisha magumu wanayo ishi. Alisema katika makanisa na misikiti kuna waumini wenye fedha nyingi, lakini wanazitumia katika anasa na wengine kuzilalia wakati kuna watu wanaishi katika mazingira magumu na wanashindwa kupata hata mlo mmoja.
Dk. Nchimbi alipongeza juhudi za kanisa hilo kuangalia watoto hao waishio katika mazingira magumu na kula nao chakula pamoja na msaada huo ambao alisema unasaidia kuonyesha watoto hao kuwa kuna watu wanaowajali na kuwapa furaha na kuwasaidia kulala usinguzi mzuri. “Kanisa mmefanya kitu kikubwa kuliko kawaida kwani hawa ni watoto ambao ni taifa la kesho na msaada huu mtawawezesha kuishi na kulala usingizi mzuri,” alisema.
Katika risala yao, watoto hao walisema kuwa wamekuwa wakilala katika mabanda na kuwa wamekuwa wakinyanyaswa na walinzi kwa kufukuzwa wakiwa wamelala na wakati mwingine kufanyishwa mazoezi usiku kucha, muda ambao walipashwa kuwa wamelala.
Msoma risala hiyo, Danford Mrigo, alisema wamekuwa wakilalia maboksi, kuvaa nguo za kuokota na kula matunda yaliyo tupwa majalalani huku wakijishugulisha na shuguli za kubeba mizigo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: