Social Icons

Pages

Monday, November 02, 2015

MAALIM SEIF: UFUMBUZI WA UCHAGUZI KUPATIKANA KARIBUNI

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha.
Chama cha Wananchi CUF kimesitisha ajenda ya kurejesha kwa wananchi mpango wa kupinga uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi, baada ya juhudi za kidiplomasia kuonyesha mwelekeo wa kupata ufumbuzi hivi karibuni.
Msimamo wa kusitisha mpango huo kwa muda umetangazwa na mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana. Alisema juhudi zinazochukuliwa na Jumuiya za kimataifa katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo ikiwamo Umoja wa Mataifa (UN), zinaonesha mwelekeo mzuri na kuwataka wananchi kuwa watulivu wakati kazi ya kutafuta ufumbuzi ikiendelea kufanyika.
“Sisi tumepata moyo na imani kwamba ufumbuzi wa haki wa suala hili hauko mbali na Wazanzibari wataona mafanikio ya demokrasia yetu tunayoijenga katika nchi yetu,” alisema Maalim Seif akiwa ameambatana na Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakar na Makamu Mwenyekiti wake wa kampeni, Mansour Yussuf Himid.
Alisema miongoni mwa wanaofanya jitihada ya kumaliza mgogoro huo na kuonyesha mwelekeo mzuri ni UN, Jumuiya ya kimataifa pamoja na walioleta waangalizi katika uchaguzi huo.
Wengine ni viongozi wakuu wastaafu nchini, viongozi wa dini na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.
Hata hivyo, Maalim Seif alisema kuna kikundi cha watu wachache ambacho kimekuwa kikwazo kutokana na kutetea maslahi binafsi katika kutafuta muafaka wa mgogoro huo.
“Kuna kikundi kidogo cha watu ambacho hakitaki kuona ufumbuzi unapatikana, hawa wanajali maslahi yao binafsi, kuliko maslahi mapana ya nchi na watu wake,” alisema na kuongeza kuwa lazima mshindi halali atangazwe.
Pamoja na hitihada hizo, Maalim Seif aliwataka  wanachama na wafuasi wa CUF wachukue tahadhari kubwakuhusiana na taarifa zinazosambazwa zikiwataka kufanya vurugu kwa kuwa sio za CUF bali zinaenezwa na watu wasioitakia mema Zanzibar na watu wake.
Alisema vyombo vya ulinzi na usalama vinawajibu mkubwa wa kusaidia ili kupatikana ufumbuzi wa tatizo lililopo badala ya kuongeza wasiwasi kwa wananchi kwa kutoa vitisho na kupiga watu bila hatia.
Alisema Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, wana dhamana ya kuikwamua Zazibar na Tanzania katika mgogoro wa uchaguzi uliojitokeza Zanzibar.
Alisema kupelekwa kwa vifaru na magari ya maji ya kuwasha Pemba na Unguja sio ufumbuzi wa mgogoro huo ambao unatokana na kuvunjwa kwa misingi ya demokrasia kupitia uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema viongozi wa CCM Zanzibar hawana sababu ya kuwa na hofu ya maamuzi ya Wazanzibari na kama kuna tofauti zozote za kisiasa na kimtazamo zinaweza kuzungumzwa na maelewano kufikiwa.
“Nawahakikishia viongozi wa CCM na Wazanzibari wote kwamba hakutakuwa na ulipizaji wa kisasi au kufukua makaburi kwa mambo yaliyopita, sote tunafanya kazi pamoja chini ya muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa maslahi ya Zanzibar na wananchi wake bila ya kujali tofauti za itikadi na kisiasa za kabila dini na rangi,” alisisitiza Maalim Seif. 
Wakati huo huo Seikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema Dk. Shein ataendelea kuwa rais wa Zanzibar hadi rais mpya atakapochaguliwa na kuapishwa baada ya matokeo ya uchaguzi kufutwa.
Msimamo huo ulielezwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, kupitia taarifa ya serikali.
Alisema kwa mujibu wa 28(a) cha katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kimeweka sharti kuwa mtu ataendelea kuwa rais mpaka rais ale kiapo cha kuwa rais na kuapishwa na mamlaka ya dola.
Alisema hakuna mgombea au mtu yoyote ya kutangaza matokeo ya uchaguzi zaidi ya Zec kuzingatia kifungu cha 42 (4).
Alisema kwa kuzingatia kifungu cha 42(5) ni kosa la jinai kwa mtu au taasisi yoyote kutangaza matokeo ya uchaguzi kabla ya Tume ya Uchaguzi na kuwataka wanasiasa kutii sheria na kulinda amani ya Zanzibar kwa maendeleo ya Zanzibar na wananchi wake.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: