Aliyekuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa 
Tanzania wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Umoja wa
 Katiba ya Wananchi (Ukawa) Edward Lowassa, amehoji maswali matatu kwa Rais Dk. John 
Magufuli.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam 
jana, Lowassa amemtaka Rais Magufuli baada ya kusema hakuna mtoto 
atakayelipa ada kuanzia Januari, mwakani, atamke mustakabali wa 
wanafunzi walioko shuleni kama wataguswa na hatua hiyo au la.
Lowassa amesema kwa upande wake ahadi ya elimu bure aliyokuwa 
akiinadi wakati wa kampeni, ilikuwa ni kuanzia shule ya awali hadi chuo 
kikuu na kwamba hata wale walioko mashuleni, wangeguswa na hatua hiyo.
“Niliahidi watoto wote walioko na watakaoanza shule kuanzia 
kindergarten (shule ya awali) hadi chuo kikuu, serikali yetu 
ingegharimia. Na nilitangaza kufuta michango yote shuleni ili 
kumpunguzia mzigo mwananchi,” alisisitiza Lowassa ambaye amekataa 
kuyatambua matokeo ya ushindi wa Dk. Magufuli akidai kuwa yeye ndiye 
aliyeshinda kwa asilimia 62 ya kura zote zilizopigwa.
Kuhusu suala la mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, Lowassa 
amesema yeye alishaweka wazi kuwa elimu ingekuwa bure hadi chuo kikuu.
“Vijana hawa wanahangaika na mikopo na nasikia ni asilimia 17 tu 
kati ya wanafunzi 70,000 ndiyo waliopata mikopo. Sera ya Chadema na 
Ukawa kwa ujumla, ni kufuta kabisa shida hizi kwa serikali kufadhili 
elimu yao,” alifafanua Lowassa katika taarifa yake hiyo. Kwa msingi huo,
 Ukawa kupitia kwa aliyekuwa mgombea wao wa urais, Lowassa, umewataka 
wananchi kutofautisha ahadi ya elimu bure iliyotolewa na Rais Magufuli 
na ile iliyotolewa na Ukawa.
Lowassa alisema Magufuli ametoa maelekezo kwa watendaji wa serikali
 kuweka mikakati ya kutekeleza ahadi yake kuanzia Januari, mwakani 
kwamba hakuna mtoto atakayelipa ada.
Hata hivyo, amesema hajaeleza waziwazi hatma ya wanafunzi walioko mashuleni kama wataguswa na hatua hiyo au la.
     CHANZO:
     NIPASHE
    
 

No comments:
Post a Comment