Social Icons

Pages

Friday, October 30, 2015

MGOMBEA CCM ATANGAZWA MSHINDI JIMBO LA MBAGALA


Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mbagala, Fortunatus Kagimbo, amemtangaza Issa Mangungo, wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa mshindi wa ubunge Jimbo la Mbagala baada ya kushinda kwa kura 87,249 dhidi ya mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Kondo Juma Bungo, aliyepata kura 77,043.
Baadhi ya wagombea wengine ni Said Rambi (ACT-Wazalendo) kura 4,398, Rajabu Bakari (Tadea) kura 607, Ndonge Said (AFP) kura 737, Rehema Kilai (Chausta) 1,314, Mapande Kassim (NCCR-Mageuzi) kura 2,156, Ramadhani Nassoro (NRA) kura 238 na Marry Daudi (UPDP) kura 81.
Hata hivyo, mgombea ubunge kwa tiketi ya CUF katika jimbo hilo, Juma Kondo, alisema hayatambui matokeo hayo kwa madai kwamba yamefanyika kinyume cha taratibu za uchaguzi na haukuwa wa haki.
Alidai kuwa juzi wakati kazi ya kuhesabu matokeo ya jimbo hilo ikiendelea, Msimamizi wa Uchaguzi aliwaambia mawakala wa vyama na wagombea ubunge kuwa kazi hiyo imesitishwa hadi pale Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) itakapotoa tamko la mwisho kuhusu mgogoro uliopo jimboni hapo.
Alisema wanashangaa walipofika siku inayofuata katika Shule ya Msingi Maji Matitu ambako ndiko majumuisho ya kura za jimbo hilo yalikuwa yakifanyika, waliyakuta matokeo yakiwa yamebandikwa pasipo kushirikishwa.
Aliongeza kuwa wanajipanga kufuata sheria na taratibu za kukata rufaa baada ya kushauriana na mwanasheria wao. “Matokeo haya siyatambui kwa kuwa ni ya uongo. Kwanza Mkurugenzi alikuja kubandika wakati wagombea hatupo na hakuna sehemu yoyote niliyosaini… Siamini kama Mkurugenzi ndiye aliyebandika,” alisema Kondo.
Naye mgombea ubunge kwa chama cha NCCR-Mageuzi, Kassim Mapande, alisema uamuzi alioutoa Mkurugenzi, ni  wake peke yake kwa kuwa hakuwashirikisha wagombea na kwamba matokeo hayo ni ya uongo.
Msimamizi wa Uchaguzi, Kagimbo aliwataka wananchi wa jimbo hilo kuyaheshimu matokeo hayo na kukubali matokeo yaliyotolewa na Nec pasipo kusahau kuimarisha amani.
Alisema idadi ya wapiga kura katika jimbo hilo walioandikishwa walikuwa ni 336,468, idadi halisi ya waliopiga kura ni 183,770 na idadi ya kura halali ni 174,982 huku kura zilizokataliwa zikiwa 8,788.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: