Social Icons

Pages

Friday, October 30, 2015

KWA MAGUFULI SHANGWE TUPU

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji mstaafu Damian Lubuva.
Shangwe, nderemo na vifijo, vilitawala katika mji wa Chato na viunga vyake baada ya mgombea wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, kutangazwa rasmi kuwa mshindi wa kinyang’anyiro cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji mstaafu Damian Lubuva, alimtangaza Dk. Magufuli kuwa mshindi halali wa nafasi hiyo jijini Dar es Salaam jana baada ya kupata kura nyingi kuliko wagombea wenzake. Kwa matokeo hayo, Dk. Magufuli atakuwa Rais wa awamu ya tano. Watangulizi wa Dk. Magufuli ni hayati Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Rais anayemaliza kipindi chake, Jakaya Kikwete.
Shamrashamra za wakazi wa Chato zilisababisha shughuli mbalimbali za kijamii kusimama na wananchi kuingia mitaani kushangilia ushindi wa Dk. Magufuli.
Wakati wakishangilia ushindi huo, wananchi walisikika wakiimba “aliselema, alija huku baadhi yao wakiwa wamebeba bendera za CCM na waendesha bodaboda wakipita mitaani wakiziendesha kwa mbwembwe. “Nina furaha isiyo kifani kusikia Dk. Magufuli ameibuka kidedea,” alisema kwa kifupi, Mary Mathayo, mkazi wa mjini hapa.
Kwa upande wake, Michael Andrew, alisema anajivunia kupata rais anayetoka katika wilaya aliyopo na kwamba anatarajia kuona maendeleo makubwa zaidi kutoka kwa Rais mpya wa awamu ya tano ambaye ni mzaliwa wa Wilaya ya Chato.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: